Ads Top

POLISI GEITA WATUHUMIWA KWA UTESAJI RAIA

Na Antony Sollo Geita

JESHI la Polisi Mkoani Geita limeingia katika kashfa ya utesaji wa Raia kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake ambapo malengo ya kuanzishwa kwa jeshi la polisi nchini siyo kunyanyasa Raia bali ni kulinda raia na mali zake.

Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoani Geita Fabian Mahenge ambaye ni mmoja wa Viongozi 51 wa Chama hicho aliyekaa mahabusu katika Gereza la Biharamulo kwa zaidi ya siku 45 kutokana na kilichoelezwa kuwa ni mapenzi ya viongozi wa Jeshi la Polisi.

Katika mkutano wake na Waandishi wa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro alisema kuwa Jeshi la Polisi halipo kwa ajili ya kumuonea mtu kwa itikadi yake ya kidini wala kisiasa na aliwataka Askari wa Jeshi hilo kufanya kazi zao kwa weledi na kukamata mtu na kufanya uchunguzi na pale watakapobaini kuwa hana kosa wamuachilie mara moja.

Hali hii Mkoani Geita imekuwa tofauti na agizo la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP kwani kumeripotiwa ukiukwaji mkubwa wa maadili ya jeshi la polisi huku kukiwa na madai dhidi ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mganza ambaye alivamia kikao cha ndani cha Viogozi wa CHADEMA Mkoani Geita kilichokuwa kinafanyika katika ukumbi wa Manzagata huko Mganza.
           
Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoani Geita Fabian Mahenge alisema kuwa julai 7 mwaka huu kulikuwa na ratiba ya vikao viwili ambavyo vilipangwa kufanyika katika ukumbi wa Manzagata ulioko Mganza Wilaya ya Chato Mkoani Geita.

Kwa mujibu wa Mahenge kikao cha kwanza kilikuwa ni mkutano mkuu wa chama Kata ya Mganza ambapo mahenge aliwataja wajumbe wa kikao hicho kuwa ni Viongozi wa Matawi ambao walialikwa rasmi kwa ajili ya utambulisho wa Mwenyekiti wa Mkoaambapo baada ya utambulisho angeachana nao na kuendelea na kikao cha Viongozi wa Mkoa ambao idadi yake ni wanane.

Wakati maandalizi ya kuanza kwa vikao hivyo Mahenge alisema kuwa kulikuwa na dalili zote kuwa kungefanyika vurugu ili kuhakikisha vikao hivyo vinavurugwa na Jeshi la Polisi kwani Katibu Mwenezi wa Kata ya Mganza Marco Maduka ambaye aliwahi kushika nadfasi ya udiwani katika Kata ya Mganzaaliitwa kituo cha Polisi na Mkuu wa Kituo cha polisi Mganza wito ambao hata hivyo haukufahamika mara moja.

Kufuatia hali ya wasiwasi iliyoonekana kutokana na wito wenye utata uliotolewa na Mkuu huyo wa Kituo cha polisi Mganza kiongozi huo ilibidi asindikizwe na Viongozi wawili ambao ni Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Chato Mange Sayi Ludomya pamoja na Katibu wa Chadema Mkoa Soud Ntanyagala.

Kwa mujibu wa Mahenge baada ya kufika kituoni hapo viongozi hao hawakurudi na juhudi za kuwafuatilia zilipofanyika walielezwa kuwa Viongozi hao walipelekwa Chato kwa amri ya OCD na baada ya kufika waliwekwa mahabusu bila kuambiwa makosa yao.

Wakati hayo yakifanyika Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa  Fabian Mahenge alikuwa amebaki na viongozi wa Kata ya Mganza ambao ni viongozi wa Mkutano Mkuu wa
Kata pamoja na viongozi wa Mkoa yaani Mwenyekiti wa Balaza la Wazee Mkoa Vitus Makoye,Mwenyekiti,BAVICHA Neema Chozaile pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Geita Masaga Misso.

Baada ya kuitikia wito wa OCS Kituo cha Mganza viongozi waliokwenda huko hawakurudi na ilipotimu majira ya saa 10 jioni viongozi waliobaki na Mwenyekiti huyo walivamiwa na Askari wa Jeshi la Polisi likiwataka kutawanyika huku OCS akiwa amevalia nguo za kiraia na akiwa amelewa chakali alitoa bastola na kuingia ukumbini na kuwatishia viongozi hao.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa alimhoji OCS huyo akitaka kujua yeye ni nani maana alikuwa amevaa kiraia jambo lililowapa shida katika kutambua kuwa yeye ni nani kufuatia kutishiwa na silaha maana si jambo rahisi kwa kiongozi mkubwa kama OCS kukiuka maadili ya matumizi ya silaha kama ilivyokuwa kwa OCS huyo ambapo hata hivyo aliwaambia kwa kejeli kuwa kama hawamjui leo ndiyo wangemjua yeye ni nani.

“Mimi mnataka nijitambulishe kwenu! Hivi hamnijui? Sasa ngoja nadhani baada ya muda mfupi mtanitambua mimi ni nani”alisema OCS.
 Baada ya majibizano hayo OCS alitoka nje ya ukumbi na baada muda mfupi alirudi akiwa na askari wanne na kuanza kupiga mabomu ya machozi ndani ya ukumbi huo uliokuwa na wajumbe wasiopungua 80.

Wakati Askari hao walioongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mganza wakitekeleza hayo,kulikuwa na kundi lingine la askari walioitwa kutoka Chato walifika ukumbini hapo na kuanza kuwashambulia viongozi hao kwa kuwapiga wakitumia silaha mbalimbali ambapo mmoja wa viongozi hao Patrick Kalikawe alichomwa singe ya bunduki huku Masimango akipigwa na kitako cha bunduki mguuni na mtu mwingine ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja akivunjwa mkono.

Katika vurugu hizo viongozi 51 walikamatwa na kupelekwa mahabusu kituo cha polisi Chato na baada ya kufikishwa waliwekwa rumande bila kuambiwa makosa yao, Mahenge  aliongeza  kuwa zoezi la kuwachukua maelezo lilipoanza waliambiwa kuwa kosa waliloshitakiwa nalo viongozi hao ni kufanya kusanyiko lisilo na kibali ndani ya ukumbi wa Manzagata.

Imeelezwa kuwa Viongozi hao walikaa Mahabusu kituo cha polisi Chato kwa saa 72 kabla ya kupandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka ya kufanya kusanyiko lisilo na kibali ndani ya ukumbi wa Manzagata ambapo hata hivyo viongozio hao walikana shitaka hilo.

Baada ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Chato kutoa taarifa juu ya dhamana dhidi ya watuhumiwa hao kuwa wazi,Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi aliweka pingamizi la dhamana kwa washitakiwa hao akidai kuwa iwapo wangeadhaminiwa wangeweza kuhatarisha Amani na kusababisha uvunjifu wa Amani katika maeneo ya Chato ambapo baada ya kuwekewa pingamizi hilo viongozi hao walisafirishwa hadi gereza la Biharamulo ambako walikaa muda wa siku 45.

Yaliyojiri katika Gereza la Biharamulo.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa uongozi wa gereza hilo uliwapokea vizuri kwa maana ya kwamba hawakufanyiwa vitendo vya ukandamizaji kama walivyofanyiwa na jeshi la polisi.

“Tulipokelewa vizuri kama watu ambao tulikuwa tunaingia kuanza maisha mapya,zaidi ya yote Mkuu wa gereza alitenda haki kwa kuwa tayari kutusikiliza pale tulipotaka kuhoji au kupata ufafanuzi wa jambo lolote na kutufariji kwa maneno mazuri akisema kama tuliingia ipo siku tena tutatoka”alisema Mahenge.

Mahenge anazibainisha changamoto walizopambana nazo Mawakili waliokuwa wakiwatetea viongozi hao ambapo walikuwa na kibarua kigumu kutokana na kuwepo kwa hoja
mbili zilizokuwa walizokuwa wamewekewa ili kuhakikisha viongozi hao wanaendelea kusota rumande.

Hoja ya kwanza ilikuwa ni kupambana na mwendesha mashitaka ili kuondoa pingamizi la dhamana na hoja ya pili kusimamia kesi ya msingi yaani kufanya kusanyiko lisilo na kibali.

Mahenge anabainisha kuwa,baada ya Mawakili kushinda hoja ya kwanza kuhusu pingamizi la dhamana ikazaliwa agenda nyingine kwamba ili mtu aweze kupata dhamana,ni lazime apate wadhamini wawili yakiwemo masharti yaliyojaa mkanganyiko uliowafanya wadhamini kukosa sifa ya kuwadhamini viongozi hao.

Mahenge aliendelea kubainisha mbinu na unyanyasaji uliokuwa ukifanywa kuhakikisha yeye na viongozi wenzake wanaendelea kukaa mahabusu pamoja na kukosekana kwa usafiri wa kuwatoa washitakiwa kutoka Biharamulo kuwaleta Mahakama ya Wilaya ya Chato zoezi ambalo lilichukua wiki tatu.

Kufuatia hali hii Jeshi la Polisi kupitia kauli iliyotolewa na IGP kwamba Jeshi la Polisi halitamuonea mtu Viongozi wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita wanaonyesha wazi kupingana na Mkuu wao huyo ,lakini pia hata upande wa Rais Magufuli ambaye aliingia madarakani akisisitiza kuondoa mlundikano wa wafungwa na M,ahabusu katika Magereza.

Changamoto ndani ya Gereza la Biharamulo.

Kuhusu changamoto zilizomo ndani ya gereza Mahenge alisema kuwa kuna changamoto nyingi ndani ya gereza hilo lakini kubwa kuliko zote ni maji,ugonjwa wa kuambukiza kama upele.
Mahabusu wa kubambikizwa kesi na Askari wa Jeshi la Polisi.

Mahenge anasema kuna kundi kubwa la vijana kutoka chato ambao walikamatwa na kubambikizwa kesi za uzembe na uzurulaji jambo ambalo si la kweli maana wengi wa vijana hao walikamatwa wakiwa katika nyumba za kulala wageni,wengine wakiwa vibarua kwa watu kwa ajili ya kujipatia kipato lakini hadi leo hii wako mahabusu wakitumikia vifungo na kibaya zaidi ni vijana wenye umri mdogo yaani chini ya miaka 18.

Mahenge anaenda mbali zaidi kwa kuifananisha chato na nchi nyingine maana mambo yanayofanywa na Askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Chato hayafanani na sehemu yoyote katika nchi hii.

Mahenge ameziomba Taasisi zinazotetea Haki za Binadamu zielekeze nguvu zote chato ili kujionea mambo ya ukatili yanayofanyika huko,ikizingatiwa kuwa hata Mkuu wa nchi hii(Rais Dkt John Pombe Magufuli ) ndiko anakotokea na ilitakiwa Wilaya ya Chato na Geita kwa ujumla iwe mfano kwa maeneo mengine nchini hususani katika masuala mazima ya utawala bora na unaozingatia Sheria na Haki.

MWISHO.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.