Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekubali kusitisha maandamano
Yaliyokuwa yafanyike leo
kushinikiza kujiuzulu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne ya 2012.
Makubaliano yalifikiwa baada ya kikao cha Mkuu wa
Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Said Mwema na viongozi wa Chadema
walioongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kilichofanyika
makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, IGP Mwema alikuwa na Kamishna
wa Operesheni wa Polisi, Paul Chagonja, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar
es Salaam, Suleimani Kova na maofisa wengine wa ngazi za juu wa jeshi
hilo.
Mbowe katika ujumbe wa Chadema aliambatana na
Katibu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Deogratius Munishi
na Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Taarifa ya pamoja ya polisi na Chadema
iliyosainiwa na Makene na Msemaji wa Mkuu wa Polisi, Advera Senso
ilisema baada ya kushauriana, walikubaliana kusitisha maandamano hayo
ili kutoa nafasi ya wananchi kushiriki katika mapokezi ya ugeni wa Rais
wa Jamhuri wa Watu wa China, Xi Jinping.
“Pia katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Chadema na
IGP Mwema walikubaliana kufanya kikao cha pamoja ndani ya siku 14 ili
kuona utaratibu mzuri utakaoweka namna nzuri ya kuwasiliana na
kushirikiana pasipo migogoro kwa pande zote mbili, huku kila upande
ukitimiza wajibu wake kwa masilahi ya taifa, “ ilisema sehemu ya taarifa
hiyo.
Chadema waliingia katika mvutano mkali na
polisi kutokana na kuzuiwa kwa maandamano yao, ambapo kabla ya
makubaliano ya jana walikuwa wamesisitiza kwamba yangefanyika hata kama
polisi wangetumia nguvu kuyazuia.
No comments: