Ads Top

Ngassa atua Jangwani, asaini mkataba wa miaka miwili


Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako (kushoto) akimkabidhi Mrisho Ngassa jezi wakati akimtambulisha rasmi jana, baada ya kusaini Yanga mkataba wa miaka miwili.Picha na Michael Matemanga  

Dar es Salaam.Wakati winga Mrisho Ngassa akisaini mkataba wa miaka miwili wa kuicheza Yanga, kiungo Haruna Niyonzima ametoa saa 24, kwa uongozi wa mabingwa hao kumalizana naye kabla ya kutimkia timu nyingine.
Uongozi wa Yanga jana umemtambulisha rasmi Ngassa kumrejea kundini baada ya kumaliza mkataba wake na Azam ambao walimpeleka kwa mkopo Simba kwa muda wa mwaka mmoja.
Habari ambazo Mwananchi ilizipata zimesema kuwa tayari uongozi wa Yanga umeshampa kitita cha Dola 10,000 kati ya Dola 30,000, mshambuliaji huyo ambaye aliondoka kwa mbwembwe kwenda Azam kwa dau la Sh50,000 milioni.
Chanzo hicho kimedai kuwa Ngassa bado anaidai klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani kitita cha Dola 20,000 ambacho aliahidiwa kukabidhiwa mara atakapotua rasmi ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Ngassa ambaye alikabidhiwa jezi iliyokuwa na jina lake na Katibu mkuu wa klabu hiyo Lwaurance Mwalusako alisema, “Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kurudi tena Yanga, klabu ambayo nina mapenzi nayo
tangu utoto, nawashukuru viongozi wa Yanga waliopigana hasa rais Kifukwe (Francis) kuhakikisha wananirudisha kundini.
“Nilipokuwa Azam, Simba nilicheza kwa uaminifu mkubwa, lakini viongozi hawakuwa na imani na mimi kwa vile nina mapenzi na Yanga, ni kweli naipenda Yanga, lakini hata siku moja sikucheza kiuunazi, nilicheza kwa uaminifu kwa vile mpira ni ajira yangu, mapenzi yanafuata lakini viongozi hawakuliona hilo.
Kuhusu kusaini mkataba na Simba ambao alipewa dola 25,000 pamoja na gari aina ya Verosa Ngasa alisema “Sina mkataba na Simba na sijawahi kusaini mkataba na Simba, mkataba wangu ni Azam na Azam waliomnipeleka Simba kwa mkopo.
Akifafanua jambo hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Binkreb alisema “Sh 25 milioni zilizotolewa na Simba ilikuwa ni ada ya kumtoa Azam kwenda Simba na gari alilopewa ilikuwa ni ushawishi tu ili akubali kucheza Simba klabu ambayo hakuwa na mapenzi nayo.”Naye
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspop
alisema,“Mkataba wetu na Ngassa upo wazi tena unasema wazi utaanza pale ambapo mkataba wake na Azam utakapomalizika, hatujaingia mkataba juu ya mkataba kama Yanga wanavyodhani.
“Yanga wamezoea fujo wanafanya mambo kama vile TFF ni mali yao wanajua watabebwa, kwanza wao ndio waliomwambia Ngassa siyo mali kitu, ameshuka
thamani wakati ule sisi tulitaka kutoa milioni 20 wao wakaambiwa waongeze tano iwe sh 25 milioni ili wamchukue, walikataa na kusema hana thamani ya hela hiyo imekuwaje sasa? alisema kwa kuhoji.
Wakati Ngassa akitua Jangwani kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima alisema ametimiza malengo yake ya kuipatia Yanga ubingwa na kilichobaki sasa ni kutimiza malengo yake ya kutafuta mafanikio mengine.
“Nilipokuja Tanzania nilikuwa na ndoto ya kuipatia Yanga ubingwa, hilo limetimia sasa ninaanza ndoto za kutafuta masilahi yangu,” alisema Niyonzima. na kuongeza:
“Tumekuwa katika mazungumzo na Yanga kwa wiki mbili sasa lakini, tukayasitisha kwa sababu ya mechi ya Simba, niliwapa siku mbili baada ya mechi hii ili wanipe jibu kamili vinginevyo natimkia timu nyingine.”
Niyonzima alisema si chezi soka la mapenzi ingawa ameishi na wanayanga vizuri, kila mtu nampenda na hata familia yake inapenda kuishi na wanayanga.
“Mimi sina tatizo na Yanga, nimeishi nao vizuri, ila masilahi yangu ni zaidi ya Yanga, wakishindwa, kunipa ninachokitaka, nitakwenda popote nitakapopata masilahi, iwe Simba ama Azam niko tayari kwenda kama tu wataweka dau kubwa mezani,” alifafanua Niyonzima.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.