SIMBA YATINGA KATIKA NAFASI YA TATU
Kiungo Amri Kiemba alifunga bao moja na kutengeneza moja wakati
Simba ilipoisambaratisha Ruvu Shooting kwa mabao 3-1 jana kwenye Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam katika harakati zake za kusaka nafasi ya tatu.
Kiemba alifunga bao lake kwa shuti la
umbali wa mita 25 katika dakika ya 14, ambapo Shooting walisawazisha bao
hilo katika dakika ya 52 kupitia Abdulrahman Musa kabla ya Kiemba
kutengeneza bao la tatu lililofungwa na Rashid Mkoko katika dakika ya
89, wakati Christopher Edward alipachika bao la pili la Simba akimalizia
mpira uliotemwa na kipa Benjamani Haule katika dakika ya 87.
Kwa matokeo hayo Simba imepanda hadi nafasi
ya tatu ikiwa na pointi 42 na kuiacha Kagera Sugar katika nafasi ya nne
katika msimamo wa ligi hiyo.
Kocha wa Simba, Patrick Liewig akizungumza
baada ya mechi hiyo aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri na
kufanikiwa kupata matokeo hayo mazuri.
“Vijana wangu wanafuata maelekezo yangu vizuri, nadhani hiyo ndiyo siri ya mafanikio yetu kwa sasa,” alisema Liewig.
Ruvu Shooting waliianza mechi ya jana kwa
kasi na kufika langoni kwa Simba katika dakika ya saba baada ya shuti la
Musa kutoka sentimita chake katika lango la Simba.
Simba walijibu mapigo katika dakika ya 14
na kufanikiwa kupata bao la kuongoza lililofungwa na Kiemba kwa shuti la
umbali wa mita 25, akimalizia vizuri pasi ya Felix Sunzu aliyempokonya
mpira beki wa Shooting, Shaaban Suzan.
Kama hiyo haitoshi, Sunzu nusura
aipatie Simba bao baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Kiemba na
kugongesha mwamba katika dakika ya 21.
Katika mechi hiyo kipa wa Shooting, Benjamin Haule alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti la Haruna Chanongo katika dakika ya 34.
Pia beki Said Madega wa Shooting alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Chanongo katika dakika ya 45.
Simba katika mechi hiyo walitumia zaidi
winga zao mbili zinazoongozwa na Chanongo na Ramadhan Singano kupitisha
krosi za juu kwa Sunzu, wakati Shooting wenyewe walicheza pasi fupifupi
kwa kasi, lakini walikosa umakini kwenye umaliziaji.
Kurejea kwa Sunzu kunazidi kuimarisha safu
ya ushambuliaji ya Simba kabla ya mchezo wao wa mwisho wa msimu huu
dhidi ya mahasimu wao Yanga hapo Mei 18.
Shooting walisawazisha bao hilo katika dakika ya 52 baada ya Musa kuwahadaa mabeki wa Simba kabla ya kufunga bao hilo.
Kocha Liewig alimpumzisha Sunzu na
kumwingiza Mrisho Ngassa mwanzoni mwa kipindi cha pili mabadiliko
yaliyokuwa na faida kubwa kwa Simba vijana hao wa Msimbazi.
Katika dakika ya 87 Simba
walifanikiwa kupata bao kupitia kwa Edward akimalizia mpira uliotemwa na
kipa Haule, ambapo wakati Shooting wakijiuliza Mkoko aliipatia Simba
bao la tatu katika dakika ya 89 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Kiemba.
Simba sasa imebakiza mechi dhidi ya Mgambo JKT hapo Jumatano kabla ya kuivaa Yanga hapo Mei 18
No comments: