Ads Top

Spika Makinda azima hoja ya Mdee kuhusu umiliki wa mashamba makubwa

 
Spika Anne Makinda  

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Anne Makinda jana aliizima hoja ya Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhusu umiliki wa mashamba makubwa yasiyoendelezwa wakati wa kujadili hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo ilihitimishwa bungeni jana.
Mdee alivutana na Spika Makinda wakati wa kujadili bajeti hiyo kifungu kwa kifungu, Mdee alipotaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu kampuni zinazomiliki ardhi bila kuziendeleza na hatua zinazochukua kuhakikisha zinarudishwa kwa wananchi.
Baada ya kuuliza swali hilo huku akisisitiza kutoa shilingi, Spika Makinda alimtaka kukaa chini kwa kuwa hoja yake haina mashiko ya kufanya hivyo na kwamba kama anataka aiwasilishe kama hoja binafsi.
“Kaa chini, nakwambia kaa chini,” alisema Makinda huku Mdee akionekana kuendelea kuzungumza... “Nasema kaa chini,” alirudia na Mdee kukaa huku akikipeperusha karatasi hewani kuonyesha kutokubaliana naye.
Awali, Mdee alisema shamba la Simanjiro ambalo Halmashauri ya wilaya hiyo ilipendekeza mwekezaji kupewa ekari 500 lakini Wizara ya Ardhi iliidhinisha ekari 25,000 ambazo mwekezaji hajaziendeleza zote wakati mashamba ya Kisarawe na mashamba ya mkonge Tanga ambayo wawekezaji wameyakopea fedha nayo hadi sasa hayajaendelezwa.
Alitaka kauli ya Serikali kuhusiana na hali hiyo na jinsi ya kurudisha mashamba hayo katika miliki ya umma. Mbunge mwingine aliyetishia kutoa shilingi ni Dk Faustine Ndungulile wa Kigamboni (CCM), akijikita katika suala la ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni akisema wananchi wake hawakushirikishwa katika mipango ya ujenzi huo.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema wananchi wameshirikishwa kikamilifu katika mchakato mzima na kuahidi kukaa na mbunge huyo pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema kuzungumzia suala la Kigamboni.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye alisema kila mkazi atalipwa Sh35,000 kwa kila mita moja ya mraba na mwenye ekari moja atapata Sh141 milioni na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwa mradi huo utakuwa wa maendeleo kwa kila mmoja.
Baada ya majibu hayo, Dk Ndungulile alisimama na kusema kuwa anakubali kurejesha shilingi hasa baada ya Waziri Tibaijuka kutamka kuwa wananchi wameshirikishwa na watashirikishwa katika kutatua mgogoro wa Kigamboni.
Spika Makinda aliwataka kushirikiana kutatua mgogoro wa Kigamboni ili mradi uanze.  

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.