Hakuna shaka yoyote kuwa Rais wa Marekani akisafiri kokote duniani akitumia ndege ya kijeshi, basi hupewa jina la ‘Air Force One’.
Rais Obama akiwasiliana na wasaidizi wake safarini ndani ya Air Force
One. Hiyo ni ishara ya kuwa ndege yake inajitofautisha na nyinginezo za
abiria. Picha ya Maktaba
Ukweli si ndege maalumu yenye jina hilo, lakini ndege inayopewa jina hili ni alama ya ndege ya rais wa nchi hiyo.
Jina hilo hutumika kwa ndege mbili kubwa aina ya
Boeing 747-200B zenye namba 28000 na 29000, zinazotumiwa na rais akiwa
safarini ndani na nje ya Marekani na moja anayosafiria ndiyo huitwa kwa
jina hilo.
Ndege zote hizo husimamiwa na Jeshi la Anga la nchi hiyo. Kwa jeshi la nchi hiyo ishara kwa ndege hizo ni VC-25A.
Air Force One ni moja ya ishara maarufu kwa urais
wa Marekani na si kwa Marekani pekee, bali imekuwa kwa ulimwengu mzima.
Ndege zote zimeandikwa maandishi makubwa “United States of America,”
bendera ya nchi hiyo na nembo ya rais wa nchi hiyo.
Ndege hii tofauti na za kawaida zilizozoeleka,
inao uwezo wa kujazwa mafuta ikiwa angani kwani haina kiwango ama urefu
maalumu wa kusafiri unaweza kumfikisha rais huyo popote duniani kwa
usalama wa hali ya juu.
Ndani ya ndege vifaa vya umeme vimetengenezwa kwa
ugumu ambao haviwezi kusababisha hitilafu ambayo inaweza kuhatarisha
maisha ya abiria. Ina vifaa vizito vya mawasiliano vyenye teknolojia ya
hali ya juu inayowezesha kufanya kazi kama sehemu ya kamandi ya kijeshi
ikiwa angani kama kuna shambulio nchini mwao.
Ndani yake rais na abiria wengine wanafaidi nafasi
kubwa ambayo ni kama futi 4,000 za mraba zilizo katika ghorofa tatu
ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa kwa ajili ya Rais, yenye chumba cha
kifahari cha kulala, ofisi, choo, chumba cha mikutano.
Pia, kuna sehemu ya matibabu ambayo ina chumba cha
upasuaji na daktari angalau mmoja anatakiwa kuwa ndani wakati ndege
hiyo ikiwa safarini, pamoja na wahudumu wengine wa afya. Kuna sehemu
mbili za jiko ambazo zinaweza kutumika kuandaa chakula cha watu 100 kwa
wakati mmoja.
Air Force One pia ina sehemu kwa ajili ya
wasaidizi walinzi na watu wengine wanaoongozana na rais safarini ikiwamo
waandishi wa habari ama wageni wengine. Kuna ndege kadhaa za mizigo
ambazo zinaongozana na ndege hiyo zikiwamo za kuongeza mafuta ili kuweza
kumuhudumia Rais iwapo atakuwa angani kwa muda mrefu.
Air Force One inahudumiwa na Kikosi cha Safari za
Rais ikiwa ni sehemu ya maofisa usalama wa Ikulu ya Marekani
kilichoanzishwa mwaka 1944 chini ya Rais Franklin D. Roosevelt.
No comments: