Ads Top

Wakati Tanzania imejiandaa kupokea ugeni mkubwa kimataifa kwa siku mbili kuanzia leo, kumekuwa na maswali mengi ambayo wananchi pamoja na wachambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa wamekuwa wakijiuliza juu ya ujio wa Rais Obama wa Marekani katika ardhi ya Tanzania

 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe  

Miongoni mwa maswali hayo ni pamoja na anakuja Tanzania kufanya nini? Kwa nini hatembelei Kenya ambako ndiko hasa asili yake? Pamoja na wale ambao wamekuwa na wasiwasi juu ya rasilimali za nchi hasa gesi. Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anafafanua zaidi kuhusu ziara hiyo , umuhimu na manufaa yake.
Urafiki wa Tanzania na Marekani
Waziri Membe anasema nchi hizi mbili zimekuwa na urafiki wa karibu sana katika kipindi cha muongo mmoja na nusu (miaka 15) ushirikiano baina ya nchi hizi mbili umeongezeka. Anasema urafiki huo ulianza kuimarika baada ya kulipuliwa kwa ubalozi wa Marekani nchini mwaka 1998.
Anakumbuka baada ya kutokea mlipuko katika ubalozi huo jijini Dar es Salaam, Tanzania ilishirikiana kwa karibu na Marekani katika kuhakisha kwamba watuhumiwa wanasakwa, kukamatwa na kushtakiwa, huku katika mataifa mengine haikufanyika hivyo.
Anasema kitendo hicho kiliongeza ‘uaminifu’ kwa  Serikali ya Marekani ambayo katika kipindi hicho iliongozwa na Bill Clinton. Ukarimu wa Watanzania ukaifanya nchi yao ipendwe  na utawala wa George W. Bush na sasa Obama.
Demokrasia na Utawala Bora
Katika hilo, Membe anasema Tanzania kwa kiwango kikubwa imekuwa inatekeleza misingi ya utawala bora, uhuru wa kupata habari, haki za binadamu. Anasema hata kama kumekuwa na malalamiko juu ya suala la utekelezaji wa haki za binadamu na utawala bora nchini bado Tanzania iko katika nafasi nzuri zaidi katika takwimu kidunia ukilinganisha na nchi nyingine barani Afrika.
“Ni kweli kwamba tumekuwa tunafanya vizuri katika kigezo cha demokrasia na utawala bora ukilinganisha na nchi nyingine Afrika….katika ‘Peace Index’ (kiwango cha Amani) tunashika nafasi ya 53 duniani , Kenya wapo nafasi ya 135, Rwanda 136 na Burundi 144,” anasema Membe.
Nafasi ya Tanzania Ukanda wa Maziwa Makuu, Kimataifa
Akizungumzia nafasi ya Tanzania katika kutatua migogoro, Membe anasema nchi imekuwa kinara katika utatuzi wa migogoro katika nchi jirani, mfano ,Kenya, Zimbabwe, Comoro  pamoja na Madagascar
Lakini, pia waziri huyo anasema kwamba msimamo wa Tanzania katika masuala ya kimataifa umekuwa unaeleweka bayana.
“Msimamo wetu kuhusu masuala ya kimataifa umekuwa unaeleweka bayana tena bila kuyumbishwa na mtu wala taifa lolote…..msimamo wetu kuhusu Israel na Palestinaunaeleweka siku zote pamoja na Kosovo.,” anasena.
Akaongeza:“Tanzania ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC), lakini pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth) pamoja na hayo tumekuwa mwenyekiti wa Baraza la Ulinzi na Usalama la Umoja wa Afrika mpaka Aprili mwaka huu.”
‘Power Africa’
Rais Barack Obama anataka kuacha kitu ambacho bara la Afrika litamkumbuka ‘legacy’ katika kuhakikisha kwamba mbali na kuwa bara la giza kwa maana ya kukosa nishati ya kutosha. Kuhusu hilo, Membe anasema lengo la ‘Power Africa’ ni kuhakikisha kwamba bara hili linazalisha umeme wa kutosha.
Waziri huyo anasema kama kutakuwa na umeme wa kutosha na sio ule wa kuwasha taa za majumbani, kutakuwa na mabadiliko makubwa sana ya kiuchumi. Anasema yeye anaamini kwamba umeme ni uchumi, hivyo kutakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuongeza thamani ya mazao kutoka kwa wakulima na kuyauza kwa bei itakayompatia manufaa mkulima. “Hii dhana ya Power Africa kwa Tanzania ina maana kubwa sana….tumekuwa na tatizo kubwa sana la umeme. Ila sasa katika mipango iliyopo kuna kila dalili kwamba tutaondokewa na tatizo hilo kwa kuzalisha umeme wa uhakika na wa kutosha,” anasema
Miradi ya MCC
 Membe anasema kwamba, Tanzania ni nchi ya pili baada ya Morocco katika kupokea fedha za akaunti ya changamoto za milenia kutoka  Serikali ya Marekani.
Anasema katika awamu ya kwanza Tanzania ilipokea dola za Marekani milioni 698 ili kutekeleza miradi ya maendeleo. Marekani kupitia MCC inagharimia miradi ikiwamo  ya maji, umeme na barabara.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.