Ads Top

Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Busega Chupuchupu kutolewa nje ya Kikao cha Baraza

Na Antony Sollo   Busega.
Julai 27 2014.
Madiwani na  Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega wamenusurika kutolewa nje ya ukumbi wa kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Lunala katika mji wa Lamadi Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu.


Akifungua kikao cha Baeaza la Madiwani na Wataalamu  wa Halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Charles Lukale alitoa onyo kali kufuatia Madiwani na wataalamu wa Halmashauri hiyo kupuuza agizo ambalo amekuwa akilisisitiza mara kwa mara kwao kuhusu kuvaa nguo zenye hadhi katika kikao cha Baraza hilo.


“Ndugu zangu wajumbe, naona mmeshindwa kunielewa! nimekuwa nikiwasisitiza kila mara mvae nguo ambazo zinapaswa kuvaliwa katika kikao kama hiki yaani nguo zenye hadhi na staha, lakini sasa naona hatuelewani napenda niwafahamishe kwamba leo nilikuwa nimepanga kuwatoa nje ya kikao hiki ili iwe fundisho katika vikao vingine muweze kutii maagizo leo nawasamehe! Kikao kijacho sitakuwa na salia mtume nitamtoa nje mtu yeyote ambaye hatakuja amevaa nguo za hadhi ( suit )” alisema Lukale.


Baada ya kutoa kauli hiyo Lukae alikifungua kikao cha baraza hilo na kuendelea kupitisha ajenda zilizokuwa mbele ya wajumbe wa baraza hilo.


Katika hali isiyo ya kawaida na ambayo ilileta changamoto kubwa ni baadi ya wajumbe wa kamati ya fedha kujitokeza kuuliza maswali katika kikao hicho wakati wao ndiyo walitakiwa kumsaidia Mwenyekiti kufafanua baadhi ya mambo ambayo yangeibuliwa katika kikao hicho jambo lililomfanya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Charles Lukale kusimama na kutoa onyo kwa wajumbe hao na kuwaambia ni muhimu wasome kanuni na kuelewa nini ni wajibu wa wajumbe wa kamati.


Swali lililoulizwa na mmoja wa wajumbe wa kamati ya fedha wa baraza hilo ni kuhusu mradi wa Umeme  unaotekelezwa katika jimbo la Busega kwamba utatekelezwa katika vijiji vingapi.


Ambapo swali hilo lilijibiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Yuna Hamis kwamba, Jimbo la Busega lina vijiji 55 lakini vijiji ambavyo vitapatiwa umeme ni 46  ambapo Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika utekelezaji wa mradi wa umeme ni Wilaya ya kwanza nchi nzima kufauru kutekeleza mpango wa kuwapatia wananchi umeme.


Kuhusu vitambulisho vya hudum ya Afya kwa Wazee, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega aliesema, awamu ya kwanza vitatengenezwa vitambulisho 1000  kwa wazee hao Wilayani Busega.


Suala lingine lililotaka kuteka kikao cha Baraza hilo ni kuhusu suala la mbegu feki za Pamba zinazodaiwa kutolewa kwa wakulima zikiwa hazina ubora ambapo Mkurugenzi alisimama na kutolea ufafanuzi kuwa suala hilo akisema  kuwa linakuzwa tu.


 “ ndugu zangu mimi nashangaa sana, suala  hili linakuzwa mno sisi tulimwita mhusika na kujadiliana naye na wataalamu wetu ninavyofahamu mimi, asilimia  98% ya mbegu za pamba ziliota huku asilimia 2% tu ikishindwa kuota mimi naomba muelewe, suala hili linakuzwa tu na halina ukweli” alisema Yuna.


Baraza la Madiwani na Wataalamu  wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega lilihudhuriwa na Madiwani na wataalamu wa Idara mbalimbali lakini pia wanachi wa kawaida walifika kuja kusikiliza ambapo Mbunge wa Jimbo la Busega ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk Titus Kamani alihudhuria Kikao hicho.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.