Ads Top

Uongozi wa kijiji cha Fella Walalamikiwa

Na Antony Sollo  Mwanza
August 01 2014.
UONGOZI wa kijiji cha Fella Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza unalalamikiwa kuuza shamba la  Bernadeta Valentine lenye ukubwa ekari 15 kwa mwekezaji wa kichina kwa shilingi milioni sitini   60,000,000.


Wanaolalamikiwa kuuza shamba hilo ni Kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Ngeleka Donald Mongo akishirikiana na Halmashauri ya kijiji hicho pamoja na Afisa Mtendaji wa Kata ya Fella ambaye pia ni Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ngeleka Thomas Shunashu.


Akizungumza na Tanzania Daima Bernadeta  alisema kuwa, njama zote za kuchukua eneo lake hilo zilifanywa na viongozi wa baraza la Ardhi la Kata ya Usagara enzi hizo wakati wa  kusikiliza shauri lake namba 17/2010 kipindi cha 2009/2012 lililokuwa likiongozwa na Mwenyekiti aliyestaafu Nestory Majige.


Bernadeta  alidai kuwa kulikuwa na njama za maksudi zilizofanywa na viongozi wa  baraza hilo kwa kumnyima hukumu yake, ili kufanikisha mpango wa kupora shamba na kuliuza kama ilivyofanyika sasa. 


Tanzania Daima lilifanikiwa kupata nakala ya barua yenye kumbukumbu namb FELLA/MDC/5.01/010 ya 22/10/2010 iliyokuwa ikimjibu Bernadeta kuwa hana haki na shamba hilo majibu ambayo hakuridhika nayo.


Bernadeta alilalamikia kitendo cha baraza la Kata ya Usagara kukaa zaidi ya miaka miwili bila kumpa nakala yake ya hukumu ili aweze kukata rufaa ambapo alipeleka malalamiko yake ya kutopatiwa nakala ya hukumu kwa Afisa Tarafa ya Usagara Perpetua Chonja.


 Afisa Tarafa  Chonja alimwita Afisa Mtendaji wa Kata ya Fella kwa barua yenye kumb namb KTU/CS.20/19/13 ya tarehe 25/09/2013 hii ikiwa ni jitihada za kusaidia kutatua mgogoro huo bila mafanikio


Wakati akitafuta msaada sehemu mbalimbali Bernadeta alisikia kuwa shamba lake limegawiwa kitongoji cha Ngeleka na mali zote zimekuwa ni za kijiji cha Ngeleka bila hata kushirikishwa huku viongozi wa kijiji hicho wakiuza kipande cha shamba hilo kwa Wakala wa Barabara Tanroads na hivyo Bernadeta alirudi tena kwa Afisa Tarafa ili asaidiwe kupata msaada juu ya kuuzwa kwa shamba lake na kutopatiwa nakala ya hukumu yake Mwenyekiti wa baraza hilo Nestory Majige.


Imedaiwa kuwa Chonja alitoa maelekezo kwa baraza hilo ambapo Baada ya viongozi wa baraza hilo kupokea maelekezo hayo Mwenyekiti wa Baraza hilo Nestory Majige alimpatia Bernadeta hukumu ambayo haikusainiwa  na wajumbe wa baraza pamoja na Mwenyekiti wa baraza hilo.


Tanzania Daima lilimtafuta Afisa Mtendaji wa Kata ya Fella ambaye pia ni Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Fella Thomas Shunashu kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na viongozi wa Kijiji cha Fella ambapo Shunashu alikiri kusikia jambo hilo lakini akadai kuwa hakuwahi kuonana na Bernadeta kiofisi.


“Ndugu Mwandishi mimi sina tatizo na huyu mama niko tayari kukutana naye ili niweze kumsikiliza na kumsaidia lakini nasikia maneno mengi mno mitaani mimi yananiumiza moyoni na ninaogopa kukutana naye tukiwa wawili kwa kuwa nahofia usalama wangu.”


Kuhusu kuuzwa kwa shamba hilo Shunashu alisema kuwa yeye hahusiki na jambo lolote ila maamuzi ya kuuzwa kwa shamba hilo ni ya Halmashauri ya Kijiji cha Ngeleka ambao waliamua kuuza mali za Kijiji kwa ajili ya Maendeleo yaKijiji chao.
 “ ni kweli shamba hilo limeuzwa kwa mwekezaji jumla ya shilingi milioni sitini 60,000,000 ambazo ziko katika Akaunti ya Kijiji cha Ngeleka huku akikana kujinufaisha kwa namna yoyote ile na kuuzwa kwa shamba hilo.


Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Kata ya Usagara kipindi cha 2009/2012 alipotafutwa kujibu tuhuma hizo alitoa kauli ya kejeli  “huyu mama ni mwendawazimu na ningejua kuwa ulikuwa unanitafuta kwa ajili ya kuzungumzia suala hili nisingekuja”.


Tanzania Daima liliwatafuta wajumbe wa halmashauri ya Serikali ya Kijiji cha Ngeleka kuzungumzia tuhuma hizo wao walikataa kuzungumza lolote na kusema kuwa wanaoweza kulizungumza suala hili  ni Afisa Mtendaji Thomas Shunashu kwa madai kwamba ndiye aliyeratibu zoezi hili.


Afisa Ardhi wa Wilaya ya Misungwi Fredy Nyoka alikiri kupokea malalamiko ya Bernadeta na kusema kuwa anazo taarifa suala hilo kuwa lilipelekwa katika Mahakama zinazohusika na thamani ya madaiya mlalamikaji.


Nyoka alidai pia kupata taarifa za Afisa Mtendaji wa Kata ya Fella Thomas Shunashu kufanya taratibu za uuzaji wa mali za Kijiji hicho kinyemela na kumuonya kuwa mambo haya yanaweza kumletea matatizo. 


“Afisa Mtendaji huyo alikuwa akifanya mambo haya bila kutushirikisha sasa siku moja alitaka kuhamisha fedha zilizoingizwa katika Akaunti ya Serkali ya Kijiji shilingi milioni sitini 60,000,000 akazuiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Nathan Mshana akiambiwa kuwa fedha yoyote ikiingia kwenye Akaunti ya serikali ya Kijiji mwenye mamlaka na uhamishaji wa fedha hizo ni Mkurugenzi pekee ambapo mpangowa kuhamisha fedha hizo uligonga mwamba alisema Nyoka.”

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.