Ads Top

ADHABU YA MRAMBA, YONA YAZUA KIZAAZAA HOSPITALINI.

Waziri wa zamani wa Wizara ya Fedha, Basil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Kizaazaa kiliibuka jana wakati Waziri wa zamani wa Wizara ya Fedha, Basil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, walipowasili katika Hospitali ya Sinza Palestina, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza kutumikia adhabu ya kifungo cha nje ya kufanya usafi.



Mramba na Yona ambao walikuwa wakitumikia kifungo cha gerezani cha miaka miwili, walibadilishiwa kifungo hicho na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kutakiwa kutekeleza adhabu ya kifungo cha nje baada ya wakili wao kuandika barua ya kuomba wateja wake kutumikia adhabu hiyo kwa kufanya usafi katika hispitali hiyo hadi Novemba, mwaka huu.
 


Kizaazaa hicho kilizuka hospitalini hapo jana na kusababisha walinzi wa hospitali hiyo kuponea chupuchupu kutwagwa makonde na wananchi waliokuwa wakiwalazimisha Yona na Mramba wakabidhiwe fagio.


Wananchi hao ambao walidai walikuwa na wagonjwa katika hospitali hiyo, waliibua vurugu majira ya saa 4:10, wakati Yona na Mramba wakiingia katika ofisi za hospitali hiyo kwa ajili ya kupata maelekezo ya kuanza kufanya usafi.



Wananchi watatu waliokuwa hospitalini hapo waliibuka na kuchukua fagio lililokuwa nje na kumlazimisha Mramba alichukue ili afanye usafi badala ya kuingia ofisini.


“Kama nyie mmeshapewa adhabu ya kufagia kwa nini msifagie, ofisini mnafuata nini?. Chukueni mafagio mfagie,” alisema  kijana mmoja aliyekuwa akimkabidhi Mramba fagio.


Mramba ambaye alikuwa akiingia kwenye ofisi hizo alilazimika kuushika ufagio huo huku walinzi wakijitahidi kudhibiti hali hiyo isiendelee.


Wakati hayo yakiendelea, wananchi waliokuwa wamesimama mlango mkuu wa kuingia ofisi za utawala nao walilazimisha kuingia kwenye varanda za ofisi hiyo ili kushuhudia tukio hilo, hali iliyowapa shida askari waliokuwa mlangoni.


Yona na Mramba walipofanikiwa kuingia katika ofisi hizo, huku mlinzi aliyekuwa katika mlango huo aliyetambulika kwa jina moja la Haji akiwazuia watu wengine wasiingie, hali iliyowafanya vijana waliokuwa karibu na mlango huo kuanza kumshambulia kwa maneno na kumtishia kumpiga.


Vurugu hizo zilizodumu kwa dakika mbili kabla ya kutulizwa na askari wengine wa hospitali hiyo na kumuokoa askari aliyekuwa akitaka kushambuliwa.


POLISI WAWASILI

Majira ya saa 4:33 asubuhi, askari polisi waliwasili katika ofisi hizo baada ya kupigiwa simu na uongozi wa hospitali hiyo na kukuta hali ikiwa imetulia.


Askari hao walikuwa watatu, wawili wakiwa wamevalia kiraia na mmoja sare za polisi, waliwasili wakiwa kwenye gari namba za usajili PT 3945.


KUWASILI YONA NA MRAMBA

Awali, Yona na Mramba waliwasili katika viunga vya hospitali hiyo majira ya saa 3:45, wakiwa kwenye gari aina ya Landcruiser Fortuner yenye namba za usajili T222 DCL.


Yona akiwa amekaa mbele ya gari hiyo huku Mramba akiwa siti ya nyuma upande wa dereva, walitumia takribani dakika 15 kabla ya kushuka kwenye gari hilo.


Majira ya saa 3:48 wakiwa ndani ya gari hilo, dereva aliyekuwa akiwaendesha alishuka na kupewa maelekezo na askari wa hospitali hiyo.


Kabla ya Yona na Mramba kushuka kwenye gari hilo majira ya saa 3:59, waliendelea kubaki kwenye gari wakati askari wa hospitali hiyo wakiandaa utaratibu wa kuwaonyesha maeneo ya kufanya usafi.


Wakati wa kushuka kwenye gari hilo, Yona alitangulia huku akionekana kucheka muda wote na Mramba alifuata nyuma akipunga mkono kwa kutumia 'notibuku' aliyokuwa ameishika mkononi.


SHUGHULI ZASIMAMA

Wakati wa kuwasili kwa Yona na Mramba,  kundi kubwa la waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari liliibuka na wananchi waliokuwa katika hospitali hiyo walianza kushangaa tukio hilo.


Shughuli zilisimama kwa takribani dakika 20 wakati Yona na Mramba wakiwasili na kuzingirwa na kundi hilo la waandishi waliokuwa wakiwasubiri.


Wananchi waliokuwa eneo hilo kila mmoja alikuwa akizungumza lake, huku wakitamani kuwaona viongozi hao pamoja na kushuhudia namna watakavyofanya usafi.


WAKABIdHIWA VIFAA VYA USAFI

Saa 4:36, Yona na Mramba walitoka nje ya ofisi hizo na kuelekea maeneo walikopangiwa kufanya usafi, huku wakiwa wameambatana na Matroni wa hospitali hiyo, Agness Mgaya, aliyewaonyesha eneo la kontena ambako kuna huduma za utoaji damu ambako walikabidhiwa mafagio na mafyekeo.


Eneo la pili lilikuwa ni la huduma za mama na watoto, ambako walikabidhiwa makoti, buti na soksi za kuvaa mkonobi (gloves) pamoja na vifaa vya kufunika pua.


MRAMBA: HAPA KAZI TU

Akikabidhiwa vifaa vya usafi, Mramba alipokea huku akisema "hapa kazi tu".


Mramba pia alisifia vifaa hivyo kuwa ni visafi baada ya kuvinusa.


Wakati shughuli hizo zote zikiendelea alikuwa akizungumza na baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo na kuonyesha kushangazwa na kundi kubwa la watu kuacha shughuli zao na kuwashangaa.


“Hawana sababu za kuacha kufanya kazi zao kundi lote hili na kuanza kutushangaa sisi,” alisema Mramba.


OFISA: KUANZA KAZI YA USAFI LEO 

Ofisa Huduma za Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Deogratias Shirima, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, adhabu ya viongozi hao ilianza mara mahakama ilipotoa hukumu hiyo.


Alisema jana waliwasili kituo cha kazi kwa ajili ya kupewa maelekezo ya kazi na kuonyeshwa maeneo watakayofanya usafi.


“Leo (jana) wameshaanza kazi, kwani waliripoti ofisini kwetu saa 2:00 asabuhi na kupewa ushauri wa namna ya kutumikia kifungo na adhabu yao na wakaelezwa kama watakiuka adhabu hiyo, watapewa adhabu nyingine,” alisema.


Alisema kwa mujibu wa sheria namba 6,  kifungu kidogo cha tatu, mtuhumiwa aliyetiwa hatiani kwa makosa ya jinai anaweza kutumikia adhabu ya nje.


Alisema adhabu hiyo wataifanya maeneo waliyoelekezwa kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana.
 


Baada ya shughuli hiyo, Yona na Mramba waliondoka katika hospitali hiyo saa 5:19 asubuhi wakiwa ndani ya gari lao huku wakisindikizwa na gari la polisi.


Mramba na Yona wameanza kutumikia adhabu hiyo baada ya mawakili wao kuwasilisha barua yenye kumbukumbu namba 151/DA/3/11/223 Desemba 5, mwaka jana katika Mahakama ya Kisitu kutoka magereza kuomba kutumikia kifungo cha nje.


Januari 5, mwaka huu, Yona na Mramba walihukumiwa adhabu hiyo ya kifungo cha nje na kupewa adhabu ya kufanya usafi katika maeneo ya jamii.


Kabla ya kubadilishiwa adhabu ya kifungo cha nje, Mramba na Yona walikuwa wakitumikia kifungo cha miaka mwili kila mmoja gerezani baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11 kutoa msamaha wa kodi.
chanzo nipashe 

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.