ZAIDI YA HEKARI 400 ZA MAZAO ZIMEHARIBIWA NA MVUA YA MAWE BUKOMBE.

Zaidi
ya hekari 400 za Mahindi, Mihogo na Pamba zimeharibiwa vibaya na mvua
ya mawe katika kijiji cha Ng’anzo wilaya ya Bukombe mkoani Geita na
kusababisha hasara kubwa kwa wakulima waliokopeshwa pembejeo na mbegu
katika msimu huu wa kilimo.
ITV imeshuhudia shamba la Mahindi katika kitongoji cha Nyakato
kijijini humo likiwa limeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha
wilayani Bukombe, huku diwani wa kata ya Ng’anzo Kipara Siyantemi
akiililia serikali kuwatazama kwa jicho la huruma wakulima hao ambao
mazao yao yameathirika.
Kando na athari hizo za mvua, wakazi wa kijiji hicho cha Ng’anzo
wanalia na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa zahanati, upotevu wa mifuko
100 ya saruji, uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za uchimbaji
wa madini katika mgodi wa Nsagali pamoja na barabara.
Kilio hicho kinapatiwa majibu na mbunge wa jimbo la Bukombe Mh. Dotto Mashaka Biteko.
chanzo na ITV
No comments: