Ads Top

BARUA YA WAZI KWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI.

Ndugu Mhariri ,

Kwa heshima na taadhima sisi wananchi wakaaji wa Kitongoji cha Mnyamasi Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi  tunaomba kuwasilisha malalamiko yetu kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kufuatia unyama na manyanyaso tuliyofanyiwa na wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya na Mkoa waKatavi.

Mheshimiwa Rais kwa masikitiko makubwa tunakumbuka kauli ulizowahi kuzitoa  mara kwa mara hata wakati wa mikutano ya kampeni zako ukiomba nafasi hii uliyo nayo ambapo ulijipambanua kuwa Serikali yako itakuwa ni ya kutetea wanyonge.

Ni kweli tumeshuhudia ukishughulikia masuala mbalimbali ikiwemo kutatua migogoro kati ya raia na watendaji wa Serikali,viongozi wa Kisiasa papo kwa papo,tumekuwa tukipata faraja kubwa kutokana na mafanikio wanayopata wahanga wa aina yetu ambao wameweza kutumia njia mbalimbali kuwasilisha malalamiko kwako na kuyapatia suluhu na kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Rais sisi wananchi wakaazi wa Kitongoji cha Mnyamasi Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi,tumefanyiwa ukatili wa kutisha na viongozi uliowaamini na kuwapa nafasi ya kukuwakilisha katika Mkoa wetu wa Katavi lakini tumesikitishwa na usiri mkubwa uliodumu takribani miezi minne sasa bila mafanikio.

Mheshimiwa Rais,tumekuwa na mgogoro mkubwa na wa muda mrefu kati yetu na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Mji ambao wameamua kutunyang’anya maeneo yetu kwa kutumia vyombo vya dola huku wakisababisha majeruhi na mauaji kwa baadhi ya wananchi.

Mheshimiwa Rais ukatili tuliofanyiwa na watendaji waSerikali Mkoani Katavi umetufanya tushindwe kuelewa iwapo na sisi ni raia wa nchi hii tena tuliopiga kura zetu kuchagua viongozi wa kututetea katika masuala ya maendeleo katika nyanja mbalimbali ikwemo Elimu,Afya pamoja na ulinzi na usalama.

Tunatambua kuwa,katika vipindi mbalimbali,Serikali imekuwa na mipango mizuri hasa katika masuala ya mbalimbali ikiwemo Sera ya Taifa kuhusu Uchumi,kilimo,ufugaji na Tanzania ya Viwanda na Biashara huku kukiwa na ushirikishwaji wa wananchi katika maeneo yao.

Kilichotuumiza ni watendaji wa Serikali Mkoa wa Katavi kuamua kuendesha zoezi la kutuondoa kwa nguvu katika maeneo yetu tuliyoishi kwa muda mrefu wakitumia vyombo vya dola tena bila hata kuandaa mpango shirikishi zoezi lililopelekea mauaji na majeruhi kwa vijana wetu ambao hawataweza kufanya kazi tena kutokana na kushambuliwa kwa risasi za moto na Askari wa Jeshi la Polisi bila huruma.

Mheshimiwa Rais tumeshangazwa na matumizi ya nguvu yaliyofanywa na jeshi la Polisi kwa maelekezo ya wateule wako ambapo mpaka sasa hali ya maisha ya wananchi tuliotendewa ni mbaya kwani hatuna mahali pa kuishi kwa miezi minne sasa huku tukilala nje na watoto wetu wadogo na hakuna hata msaada wowote tuliopewa.

Mheshimiwa Rais ,tunapenda kukutaarifu kwambahuku kwetu umefanyika Ukiukwaji mkubwa wa Sheria na Haki za Binadamu pamoja na matumizi mabaya ya madaraka toka kwa viongozi wa Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya na Mkoa wa Katavi ikiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ambao kwa pamoja waliendesha zoezi la kutuondoa kwa nguvu katika maeneo yetu huku kamati wakitumia Askari wenye silaha za moto yakiwemo mabomu ya machozi zoezi lililosababisha mauaji na ulemavu wa kudumu kwa raia ambapo baada ya kufanya mauaji Jeshi la Polisi lililazimisha kufanyika kwa mazishi ya raia aliyeuawa kwa kupigwa risasi bila kufanyika uchunguzi jambo ambalo ni kinyume na Sheria.

Mheshimiwa Rais ni wazi kwamba Viongozi wa Kamati  za Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi walitumia vibaya madaraka yao ambapo walifanya vitendo vya kikatili kwa kupiga raia,kuchoma moto nyumba,kuchoma vyakula  kujihusisha na uporaji wa mali mbalimbali zikiwemo fedha taslimu katika vibanda na maduka ya wafanyabiashara,kupora simu,kuchoma moto mali za wananchi zikiwemo mashine za kusaga nafaka,kupora mifugo,baiskeli,pikiki na kutuzuia kufanya kazi za kilimo,uharibifu unaokadiriwa kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.

Mheshimiwa Rais tangu Oktoba 7 na 8 mwaka 2017 mpaka sasa wananchi tunaishi maisha magumu huku tukilala nje na hatuna huduma mbalimbali za kijamii kutokana na Kamati hizi kufanya uharibifu na sasa tumelazimishwa kulipia maeneo mapya kwa gharama ya shilingi laki moja (100,000) kwa nguvu bila kutushirikisha.

Kabla ya kufanyiwa ukatili huu hapo Septemba 9 mwaka 2017 tuliandika barua ya kuomba kuonana na Waziri wa  Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kupata msaada na mwongozo kuhusu Sheria ya Ardhi inavyoelekeza ambapo barua yetu ilipokelewa na Katibu wa Waziri septemba 12 mwaka 2017,tulielezea jinsi tulivyofanyiwa ukatili na Kamati za Ulinzi na Usalama iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Saleh Mhando.

Mheshimiwa Rais sisi wananchi kwa pamoja tunapinga kitendo cha kuondolewa katika maeneo yetu kwa madai ya kupisha uwekezaji bila kushirikishwa na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi namba 4 na 5 ya 1999,Ardhi ni mali ya Serikali lakini imefafanuliwa vizuri pale Ardhi inapotaka kutwaliwa na Serikali kwa ajili ya matumizi maalumu ya kijamii kwamba Kanuni na taratibu na Sheria lazima zifuatwe ikiwemo kufanyika majadiliano pamoja na kufanyika tathmini ili Serikali au mwekezaji aweze kulipa fidia kwa wananchi waliokuwa wakimiliki maeneo hayo.

Kufuatia hali hii tunapinga pia kitendo kuhamishiwa Luhafwe pamoja na kulazimishwa kulipa  shilingi 100,000 kwa heka moja ambayo hata hivyo haitoshi kukidhi mahitaji ya kilimo,na kwamba hatujaridhishwa na Kitendo cha Viongozi wa Serikali uliowateua kukuwakilisha kutufanyia ukatili kwa kutumia nguvu ya dola bila kufanya majadiliano na maridhiano katika jambo hili.

Zipo taarifa kuwa kwamba  viongozi wa Serikali wanawaleta wafugaji kutoka katika vijiji vingine ambao wameshatoa fedha kiasi cha shilingi mil 100 kwa viongozi wa Serikali ili tuondolewe katika maeneo yetu jambo ambalo linatupa picha kwa nini kuwe na matumizi makubwa ya nguvu ya dola kiasi hiki.

Tumelalamika kwa muda mrefu katika Ofisi mbalimbali  ambapo Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Magharibi pekee  ndiyo iliyoonyesha kutupa ushirikiano mkubwa baada ya kuandika barua yenye kumb Na LD/WZ/0023/25 kwenda kwa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi  akitaka kupatiwa taarifa juu ya ushirikishwaji wa wananchi wa maeneo hayo wakati uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya Ardhi ya vijiji huku akitaka kujua kama kulikuwa na ukweli wa madai ya baadhi ya maeneo kutengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo huku sisi wakulima na wafugaji wa kijiji hicho tukinyimwa fursa ya kuyatumia.

Kitendo cha Kamishna wa Ardhi kilitutia moyo na faraja kubwa sana kufuatilia suala hili na hasa pale Mh Naibu Waziri wa Ardhi alipoomba taarifa juu ya ushirikishwaji wa wananchi wa maeneo hayo wakati wa uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya Ardhi ya vijiji,ambapo pamoja na barua hiyo viongozi wa Wilaya na Mkoa walionyesha dharau kwa kuendelea kufanya vitendo vya ukiukwaji wa Sheria na Haki za Binadamu kwa kukaidi maelekezo toka Ofisi ya Naibu Waziri jambo lililotufanya tujiulize kwamba hivi katika nchi yetu kuna Serikali ngapi.

Baada ya kufika katika Ofisi ya TAMISEMI Mkoani Dodoma 18 Desemba 2017 tulifanya mazungumzo na Wakurugenzi wa Idara wakati tukifuatilia majibu yetu baada ya kuhitaji taarifa za upande wa pili yaani toka kwa Viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Katavi,tukiri wazi kwamba tulipata maelekezo mazuri pamoja na ushauri ambapo tukiwa hapo Ofisini tulipokea taarifa kwamba kulikuwa na watu walienda kufanya kazi siku za jumamosi na jumapili huku wakifanya uharifu pamoja na uporaji wa mali za wananchi pamoja na vipigo.

Baada ya majadiliano na viongozi wa TAMISEMI tulishauriwa tuwasilishe malalamiko yetu tukipitia marejeo mbalimbali ya barua za malalamiko pamoja na matukio ya ukiukwaji wa Sheria na Haki za Binadamu ili yaweze kufanyiwa kazi na kuona hatua za kuchukua dhidi  ya walengwa (Viongozi wa Serikali Katavi).

Mheshimiwa Rais,Kwa kuwa Ofisi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa ndizo zenye jukumu la kutoa Taarifa mbalimbali kuhusu Maafa,sisi wananachi hatuamini kama taarifa zitakazowasilishwa TAMISEMI zitakuwa na uhalisia wa  Malalamiko yetu,na kwamba viongozi walioombwa kutoa taarifa hizi kwa upande wa pili ndiyo watuhumiwa hivyo tuna mashaka kuwa taarifa zitakazotolewa na viongozi hawa siyo sahihi na za kweli kwa kuwa wao ndiyo watuhumiwa.

Kufuatia hali hiyo sisi wananchi (wahanga) wa zoezi hilo tunakuthibitishia kuwa, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika,Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Mkurugenzi viongozi (wateule wako hawa)wameonyesha utovu mkubwa wa nidhamu na matumizi mabaya ya Ofisi.

Hivyo ombi letu kwako Mheshimiwa Rais ,uunde timu ya Maalumu ya Wataalamu watakaofika katika maeneo yetu kufanya Uchunguzi wa kina bila kuwashirikisha viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Katavi pamoja na Halmashauri ili kuepuka upotoshaji unaoweza kufanyika ili kuharibu Uchunguzi. 

1.   Tume hiyo ifike katika maeneo husika na kuzungumza na wananchi kwa uhuru badala ya kuja na kufanya mazungumzo kwa kutumia hila na vitisho wakati wa kukusanya taarifa kwa kuwa kufanya hivyo taarifa hizo hazitaweza kuleta mabadiliko chanya kwetu kutokana na hasara kubwa pamoja na madhara yaliyosababishwa na uendeshaji wa zoezi hili.

2.    Serikali kupitia Tume hiyo ipitie upya na kwa kina Taarifa na malalamiko na Vielelezo vilivyowasilishwa ili kuweza kubaini namna kanuni na Maadili ya Viongozi yalivyokiukwa ili Tume hiyo iweze kuchukua hatua stahiki kwa wahusika kwa kusababisha hasara kubwa na usumbufu kwa raia kufuatia kuendeshwa kwa zoezi hili bila kuzingatia kanuni taratibu na Sheria .

3.Serikali ichunguze kuwepo kwa harufu za ukabila na Rushwa katika uendeshaji wa zoezi hili kwani lengo la kupisha maeneo haya si uwezeshaji bali ni harakati za wazi za uporaji wa haki kwa kuhakikisha wananchi ambao si kabila la wabende tunaondolewa na kunyang’anywa mali zetu pasipo kuzingatia Sheria na Haki.

4. Tunavyo vielelezo vya kuporwa kwa mali zetu,mauaji yaliyofanyika,risiti zinazotumika kulazimisha kwa nguvu kulipa kiasi cha shilingi 100,000 kila raia pamoja na usumbufu ikiwemo kutishiwa kunyang’anywa mashamba yetu ambayo tumeyamiliki kihalali kwa muda mrefu na kwamba kama hatutalipia tunanyang’anywa mashamba yetu ambayo tayari tumeshalima katika msimu huu wa 2017.

5.  Tunaomba kutoa ufafanuzi juu ya hofu iliyoibuka katika Ofisi ya Msajili wa vijiji hapo awali baada ya kuhofia ujio wetu hapo TAMISEMI bila kuwa na Mwenyekiti wa Kijiji kwamba ndiye alama inayotambulisha Serikali ya Kijiji na kuleta uhalali wa madai yetu kuwa kwamba Mwenyekiti wa Kijiji,Diwani na Mbunge wetu Mheshimiwa Kakoso  ndiyo wahusika wakuu katika zoezi hilo na ndiyo waratibu wakuu wa zoezi la kutuondoa katika maeneo yetu huku sababu kubwa ikiwa ni ukabila kama ambavyo tumeeleza katika aya ya (3) kwamba zoezi hili limetawaliwa na ukabila.

Kufuatia hali hii tunaomba Serikali itupatie msaada wa hali na mali pamoja na wadau ili tuweze kupata huduma mbalimbali za kibinadamu maana hadi sasa hatuna chakula,pamoja na mahitaji muhimu ya kibinadamu ikiwemo huduma za Afya,miundombinu,Mahema magodoro na vitu vingine vinavyohitajika kwa ajili ya kujikinga na mvua ambapo hadi sasa kuna kaya zipatazo elfu moja (1000) hazina mahala pa kuishi

Ni mimi Said Seif  Kikobe

Kwa niaba ya Wananchi wahanga wa zoezi la kuondolewa kwa nguvu katika maeneo yetu Mkoani Katavi.


No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.