Ads Top

WANAUME WAASWA KUTOJIMILIKISHA MAENEO YA FAMILIA

Na Antony Sollo

WANAUME katika  halmashauri ya mji wa Kahama Mkoani Shinyanga wametakiwa kuachana na dhana ya kujimilikisha  hati miliki za viwanja vyao, ili kutoa  kipaumbele kwa akinamama ili nao waweze kumiliki ardhi   hali ambayo itaepusha migogoro katika familia.

Akizungumza kabla ya kutambulisha mradi wa upimaji wa viwanja 4,000 katika kata ya Mhongolo  afisa ardhi wa halmashauri ya mji wa Kahama   Mashiri Magasa  alisema kuwa wanaume wilayani Kahama wamekuwa na tabia ya kujimilikisha maeneo yote yenye hati miliki  jambo ambalo siyo haki na kwamba hali kama hiyo pindi mwanaume anapofariki dunia humwacha mwanamke katika wakati mgumu.

Magasa  aliyasema hayo februari 8 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa vitongoji vya sofi, bomani na Nyamhela vilivyoko katika Mtaa wa Mhongolo ambapo aliwaasa wanaume kuachana na dhana ya kujimilikisha maeneo ya familia kwani hali hiyo ndiyo chanzo cha mifarakano katika familia pindi baba wa familia anapoamua kuchukua hati hizo na kuomba mkopo katika taasisi za fedha na kushindwa kurejesha.

“Ifike wakati wanaume muwape fursa ya kumiliki ardhi wanawake kwani kufanya hivyo kunatoa usawa katika familia lakini pia kuna wakati mmoja wa familia hiyo akifariki hasa baba mwanamke hawezi kuhangaika kutokana kuwa tayari anakuwa ana mali halisi inayomfanya aendeleze familia, wanaume wakiachana na mfumo dume mwanamke akashirikishwa ipasavyo katika umiliki huo  hakutakuwepo na migogoro baina yao,” Alisema Magasa.

Katika hatua nyingine Afisa ardhi aliwataka wakazi wa mji wa Kahama kuhakikisha wanapima viwanja vyao kabla ya kufanya ujenzi au shughuli zozote za kimaendeleo na upimaji huo uende sambamba na utafutaji wa hati miliki ili kupunguza migogoro isiyokuwa na tija kwa jamii na kuwafanya waweze kukopesheka kirahisi katika taasisi za fedha.

“Kwa mujibu wa sheria ya Ardhi na mpango miji hakuna mwananchi yoyote hapa nchini anayeruhusiwa kufanya ujenzi wowote wa nyumba za makazi katika kiwanja chake bila ya kupimwa au kujenga nyumba bila ya kufuata ramani za mpango miji tukikuta unajenga kwenye eneo bila kibali tunasitisha ujenzi na kukupiga faini” alisema Magasa.

Kwa mujibu wa mpima ardhi  kutoka kampuni ya  Total Geo survey  Co.Ltd    Emmanuel William   ambaye anayeshughulikia upimaji wa viwanja katika kata hiyo alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuchangia  gharama za upimaji ili kazi iweze kuendelea na kwamba mpaka sasa viwanja   4,000 vimepimwa na viwanja 1000 vimepitishwa na  wizara ya ardhi  Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuwatafutia hati miliki wananchi.

Akizungumzia zoezi hilo William alisema kuwa lengo ni kupima viwanja 12,000 katika Kata hiyo na kuwataka wananchi kuongeza kasi ya kuchangia gharama ya upimaji ambayo ni shilingi elfu tisini 90,000 na kwamba gharama hiyo ni ndogo ukilinganisha na bei elekezi ya serikali ya kuanzia ambayo inaanzia shilingi laki tatu, 3,000,000. Kwa kila kiwanja.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa mtaa wa Mhongolo  Denis  Diocles alisema kuwa lengo la kampuni hiyo ni kupima viwanja elfu 12, lakini viwanja vilivyofikiwa ni 4021, vilivyopewa namba ni 1335, ambavyo havijapewa namba ni 2686 na kutaja mradi wote unagharimu kiasi cha shilingi milioni 361 kati ya hivyo vilivyolipiwa ni 1192 na ambavyo havijalipiwa ni 2828.

Akizungumza katika zoezi la kutamburisha mradi huo Mwenyekiti wa mtaa wa Mhongolo Emmanuel Nangale alisema kuwa kukusanya shilingi milioni 361  kwa wakazi hao siyo kazi ndogo na kudai kuwa kiasi kilichokusanywa hadi sasa kinapswa kupongezwa licha ya watu kutohamasika kikamilifu na kwamba katika halmashauri hiyo ni Mtaa wa Mhongolo pekee umejitutumua katika zoezi hilo.

Mwisho.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.