Ads Top

KUSHAMIRI KWA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI

Makala:

Na Antony Sollo 


Zikiwa zimepita siku chache tangu vikao vya Kamati za Bunge vianze
mjini Dodoma hali ya mambo katika maeneo mbalimbali nchini si shwari
kwani kumezuka mijadala mikubwa kutokana na madhira yaliyowapata
wananchi kutokana na kupigwa,kuporwa mali ,kujeruhiwa kwa risasi za
moto na Askari wakati wa utekelezaji wa operesheni za kuwaondoa
wananchi wanaokaa katika maeneo yanayodaiwa kuwa ni Hifadhi pamoja na
Ardhi inayodaiwa kutengwa kwa ajili ya Uwekezaji nk.

Vikao hivyo vilianza jumatatu ya tarehe 15 januari 2018,hii ikiwa ni
kabla ya kuanza kwa Mkutano wa kumi wa Bunge,shughuli zilizopangwa
kutekelezwa katika kipindi cha vikao hivi ni pamoja na ziara za
ufuatiliaji ,uchambuzi wa miswada mbalimbali na kupokea maoni ya wadau
pamoja na kupokea taarifa za utendaji za Wizara.

Kamati tatu za kisekta ambazo zitakuwa na jukumu la uchambuzi wa
miswada mbalimbali ni pamoja na Kamati ya Sheria,Kamati ya
Ardhi,Maliasili na Utalii pamoja na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya
Jamii.

Maoni yangu kwa wadau na wajumbe wa Kamati hizi watumie muda huu
kuangalia namna ya kutatua tatizo lililomuelemea Mheshimiwa Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Wiliam Lukuvi ambaye kama
angekuwa si Kiongozi Mahiri huenda Rais Magufuli angekuwa ameshamuweka
pembeni kutokana na malalamiko likuki yanayoiandama Ofisi
(Wizara)yake.

Kipekee niwapongeze Mawaziri hawa wawili Mheshimiwa Wiliam Lukuvi na
Naibu wake Mheshimiwa Angelina Mabula kwa kazi kubwa wanayofanya
ikiwemo kupokea na kufanyia kazi malalamiko takribani nchi nzima.

Ukweli Wizara hii ni ngumu,ina mianya mingi ya rushwa ambayo kama si
umahiri wa Mawaziri hawa huenda Mahakama na Mabaraza ya ardhi
kungefurika mafaili ya malalamiko zaidi ya haya,lakini kutokana na
uchunguzi nilioufanya naona kabisa na ninaweka bayana kuwa Mawaziri
hawa wamejitoa muhanga kwa ajili ya kupigania haki za wananchi
wanyonge.


katika mkutano wa tisa wa bunge la kumi na moja November 16, 2017
akijibu maswali ya papo kwa papo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhshimiwa Khasim Majaliwa aliulizwa maswali na wabunge
Magdalena Sakaya (Kaliua) aliyetaka kujua Serikali imejipangaje
kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi suala ambalo ni la
kidunia.

Katika majibu yake Waziri Mkuu alisema,
“Mheshimiwa Spika,mabadiliko ya tabia nchi yaliyokumba dunia na
Tanzania ikiwemo,tunaendelea kukabili changamoto kwa  kuweka mipango
mbalimbali kuhakikisha kuwa tunakabiliana na mabadiliko hayo,moja ya
mikakati hiyo ni kusimamia Sheria ya uhifadhi wa Mazingira ili
kuhakikisha Mazingira yanabaki yanasaidia kufanya mabadiliko ya hali
ya hewa ya nchi yanabaki kuwa ya kawaida yanayowezesha binadamu au
viumbe hai vyote ndani ya nchi kufanya kazi zake vizuri na kupata
mahitaji yake vizuri”

Waziri Mkuu pia alisema kuwa Serikali imeendelea kusimamia Sheria za
mazingira ambazo pia zinakinga maeneo mbalimbali hii ni pamoja na
misitu,mito na maeneo mengine yote ili kukabiliana na hali hiyo.

Serikali pia imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuwaelimisha Watanzania
umuhimu wa Kutunza mazingira yetu kwa ujumla,zikiwemo taasisi za
kimataifa zimeendelea pia kusaidia kupambana na tatizo hili.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa watanzania nia wote kutunza mazingira na
kwamba mabadiliko ya tabia nchi duniani hayatafanikiwa iwapo
tutaendelea kuharibu misitu yetu,kuharibu vyanzo vyetu,tunaweza kukosa
huduma za jamii zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi,hivyo ni
muhimu sana kushirikiana na wataalamu kwa pamoja na wananchi wanaoishi
na kila mmoja aliyepewa dhamana katika maeneo yao ili kuweza kushiriki
kwa pamoja kuhifadhi Mazingira yetu.

Waziri Mkuu pia aliulizwa swali na Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale
(CUF) kuhusu shambulio lililofanywa julai 2017 na Askari Polisi ndani
ya msikiti ambapo shambulio hilo lilipelekea kifo cha Shekh Ismail
Weta na kuondolewa jicho kwa Shekh Abdalah Nakindabu ambapo Mbunge
huyo alitaka kujua kama Serikali ina mpango wa kulipa fidia  kwa watu
hao.

Akijibu swali hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kuwa kwanza sina
uhakika kama Askari walimshambulia mtajwa hapo na kumtoa jicho lakini
jukumu la vyombo vya dola na Jeshi la Polisi likiwemo ni kulinda
usalama wa raia na mali zao,si jukumu la polisi kwenda kumshambulia
mtu na hatimaye Serikali ianze kufikiria kumlipa mtu fidia kutokana na
shambulio lililofanywa na Askari Polisi na kama kuna Askari yeyote
amefanya tendo hilo yeye mwenyewe nje ya majukumu yake ya kazi
atachukuliwa hatua kama yeye aliyetenda kosa hilo.

“Serikali haiwajibiki kulipa fidia ikiwa si sehemu ya maagizo na wala
si jukumu la majeshi ya vyombo vya dola bali ikithibitika mmoja kati
ya watumishi wa vyombo vya dola ametenda kosa hilo na ikathibitika
hivyo,yeye mwenyewe atawajibika kuchukuliwa hatua kali na ili kama
kutakuwa na kulipa fidia itakuwa ni moja ya adhabu ambayo itatolewa na
vyombo vinavyotoa hukumu”.alisisitiza Waziri Mkuu.

“Kwa hiyo Mheshimiwa Spika niseme tu kwamba,Serikali wala vyombo vyake
vya dola havilengi kufanya kazi ya kuwatendea makosa wananchi bali ni
kuwalinda wananchi pamoja na mali zao kama tulivyojipanga kufanya
kazi”alisema Waziri Mkuu.

 Swali lingine ambalo nimelenga kulitumia kuthibitisha mambo
yanayoashiria  kushamiri kwa migogoro ya Ardhi nchini liliulizwa mbele
ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa
Ulyankulu Mheshimiwa Kadutu kuhusu kuzuiwa kwa wananchi kufanya
shughuli za kilimo na ufugaji huku maeneo hayo yakiwa yamepimwa na
vijiji vyake vimeandikishwa na wananchi wakiwa na (GN) Tangazo la
Serikali.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Khasim Majaliwa
alisema nchi yetu ina mapori yaliyohifadhiwa kisheria,yana mipaka yake
rasmi kwa mujibu wa Sheria zinazoyalinda,mapori haya yapo katika kila
eneo,na ni budi kila mtanzania kushiriki kuyahifadhi,kumetokea uvamizi
unaofanywa na waliojirani na maeneo hayo,ni kweli maeneo hayo yamekuwa
na migogoro mingi kati ya mapori yetu na vijiji,kati ya mapori na
wananchi ambao wanaoenda kufanya shughuli za kijamii huko ndani ambapo
pia Serikali hairuhusu kufanyika kwa shughuli za kijamii.

Kutokana na migogoro hii ya muda mrefu,Waziri Mkuu alitoa agizo kwa
Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya mapitio ya mipaka na kuweka
alama kwenye mipaka ya mapori yote.

Kilichobainika,Serikali ilikuwa imeshasajili vijiji hivyo na kulianza
migogoro hiyo baada ya wataalamu walioanza kwenda kufanya kazi ya
kubaini mipaka katika mapori hayo tuliwasihi wananchi walio kwenye
vijiji vilivyo ndani ya mapori hayo wawaache wataalamu wafanye mapitio
na waweke alama hizo zinazobainisha mipaka ya ramani baada ya hapo
Serikali itakuja kuona ni kijiji gani kilicho ndani na je pale palipo
kijiji malengo yetu ya uhifadhi yamefikiwa na bado ni Mahitaji sahihi
ili baadaye tuje kufanya maamuzi ya au kupunguza maeneo ambayo kwa
sasa kwa uhifadhi huo hauna tija ili kuondoa migogoro.

Waziri Mkuu alisema kuwa kazi hiyo inaendelea na aliagiza kuwa ifikapo
tarehe 30 mwezi wa kumi na mbili 2017 wataalam hao wawe wamekamilisha
kupima mapori ambayo bado  baada ya hapo Serikali iangalie ni vijiji
vingapi vilisajiliwa na Serikali na viko ndani ya hifadhi/mapori hayo
na kama vijiji hivyo bado viko kwenye maeneo yaliyo na tija kwa
malengo ya uhifadhi au la ili Serikali itoe maamuzi mengine.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi ambao wako kwenye hifadhi ambazo
zimetambuliwa baada ya uwekaji wa alama uliofanywa na wataalam
waendelee na kazi hiyo baada ya kazi hiyo Serikali ifanye mapitio na
kufanya maamuzi kwa maslahi ya nchiikiwemo kufuta kijiji au
kubadilisha mipaka ambapo mpaka hapo Mahusiano kati ya Serikali na
wananchi yatakuwa yameenda vizuri na wananchi watashiriki kulinda
mapori na hifadhi hizo.
Nakubaliana na majibu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Khasim Majaliwa,sasa
kero zilizoko katika maeneo mbalimbali Nchini ni namna wahusika
walioagizwa kufanya kazi hiyo walivyogeuza zoezi hilo kuwa uwanja wa
vita!

Iwapo Serikali imeweza kubaini mapungufu yaliyosababishwa na watendaji
mbalimbali wa Serikali katika Taasisi zake kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar
Es salaam kuingia mikataba vivyo hivyo wapo watendaji wa Serikali
walioamua kufanya wanayotaka katika agizo hili la Mheshimiwa Waziri
Mkuu hivyo ,kamati ya Maliasili ifuatilie maeneo mbalimbali na maeneo
ya kuanza nayo iwe ni Mikoa ya Tabora na Katavi ambapo mpaka hivi sasa
vikao vya Kamati za Bunge vinavyoendelea vinaweza kuona ni jinsi gani
watendaji wakiwemo wateule wa Mheshimiwa Rais walivyofanya unyama kwa
wananchi wa maeneo hayo bila huruma kwa kuchoma vyakula,nyumba,na mali
mbalimbali za wananchi jambo linalofanya wananchi waingie mgogoro na
Serikali bila sababu.

Kuna aibu kubwa juu ya mambo waliyofanyiwa wananchi kwani wananchi
wamefikia hatua za kutozwa fedha kiasi cha shilingi laki moja kabla
hata ya utaratibu ulioelezewa vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambapo
ingefanyika hivyo,wananchi wasingeweza kupata madhara kiasi cha
kusababishwa kwa vifo ,majeruhi,upotevu wa mali na kukosa makazi na
aibu ni kwa vijiji vilivyosajiliwa.

Kwa kauli nzuri iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba
atambue kuwa viongozi wa Serikali ngazi za chini wamefanya vitu vya
kushangaza mpaka wananchi wanajiuliza wana haki gani kwa Serikali yao
waliyoiweka madarakani na baada ya muda imewageuka na kuwaona hawana
thamani na kwa ujumla wake ushirikishwaji kwa wananchi katika mambo
haya ikiwemo matumizi bora ya ardhi haukufanyika hivyo yote
yaliyofanyika kuhusu utesaji,uporaji na mengine ilikuwa ni hulka kwa
wateule wa Rais ambao walilewa madaraka na kuamua kufanya watakavyo
jambo lililosababisha familia za wananchi katika maeneo mbalimbali
nchini kuishi maisha magumu ikiwamo kutokuwa na makazi,huduma za
kijamii nk.

Nashauri viongozi waweke utaratibu mzuri wa kufuatilia maagizo
waliyotoa ili kuona utekelezaji maana pindi wanapoondoka katika maeneo
hayo viongozi wa chini yao hugeuka miungu watu na kusahau maelekezo
waliyopewa.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.