Ads Top

HAYA NDO MAISHA YA MAISHA YA WATUMIAJI WA MADAWA YA KULEVYA MAALUFU KAMA UNGA

Amesimama kwenye kituo cha mabasi cha Manyanya kilichoko Kinondoni.  Fulana yake ya rangi ya bluu aliyoivaa inaonekana kama imetundikwa katika mti, kutokana na mwili wake kukonda sana na kubaki mifupa.
Nywele zake zimejaa vumbi, zimejisokota, huku wadudu ambao pengine ni chawa wakionekana kucheza wakiyafurahia makao hayo. Kona za midomo yake zimezungukwa na utando mweupe, huku michirizi ya mate ikimwagika, kila azungumzapo.
Amevaa suruali aina ya jeans, na viatu aina ya makubazi visiyoshabihiana kiaina.
Mkononi, Hussein ameshika chupa tupu kadhaa za maji ya kunywa, lakini, kila baada ya dakika mbili au tatu, anasinzia … ilhali amesimama.
Ashtukapo, ama atanadi basi lililoko safarini, atainama chini kutafuta-tafuta chupa tupu na si ajabu akacheza muziki unaosikika katika baa zilizopo katika eneo hilo.
 Ingawa yupo uraiani, lakini Hussein anajiona yungali kifungoni. Kifungo hicho ni cha utumiaji wa dawa za kulevya, ambao umemuwia vigumu kuuacha.
 Mazungumzo yake na mwandishi wa Mwananchi yanachukua muda mrefu, kwa sababu, ya kusinzia kwake mara kwa mara.
Lakini, si haba, kila azindukapo, anaendelea na mazungumzo na anasema, alianza kuvuta dawa hizo mwaka 1996 akiwa na rafiki yake, Choka ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Wazazi wangu walifariki mwaka 1990, maisha yalipokuwa magumu, nilijifunza kutumia dawa, hapa hapa Kinondoni, nikiwa na Choka,” anasema.
 Anaongeza kuwa maisha yake baada ya hapo yalifumbatwa na bangi, dawa na pombe.
“Baadaye nilikuwa situmii pombe kabisa, nikawa natumia dawa peke yake,” anaeleza.
Anaongeza kuwa, ulifika wakati alikuwa anadiriki hata kuiba fedha ili tu apate fedha ya kununulia  dawa hizo.
 Hussein anaelezea jinsi ambavyo dawa za kulevya zinawagharimu maisha na kusema, pindi azikosapo huharisha, kujisikia kichefuchefu au kuwashwa.
“Dawa ni kama shetani, mwili unadai tu, unadai tu, zikiisha unaumwa kabisaaa!” anasimulia.
Kwa hali hiyo Hussein anapata ujasiri wa kutamka bayana kuwa, yupo kifungoni, kwa sababu kwa miaka mingi sasa amekuwa mtumwa wa dawa hizo na ameshindwa kuziacha.
“Nikipata mtu wa kunipeleka kambini nikatibiwe, mimi nitaacha kabisa, nataka niwe na familia” anasema.
Kijana huyu, nguvu kazi ya taifa inayoteketea  anasema, yu radhi afanye kazi, lakini kwa  kila ‘rupia’ apatayo  ni bora akanunue dawa hizo, ili aupe raha mwili wake.
Siku ie ya mahojiano, Hussein anaeleza kuwa amekula kete za Sh 2000, lakini hawezi kusahau siku fulani … juma lililopita.
“Nilikula kete za  Sh 16,000 nililala kitandani kwa karibu siku mbili,” anasema.
 Chakula kwake si hoja ya muhimu, huweza kupata mlo wa asubuhi na ukamtosheleza, lakini ‘cocaine’ ndiyo muhimu zaidi.
“Kwa mfano, leo mchana, nimekula viazi vya kukaanga viwili, asubuhi nimekula maharage, mavumba mengine nimenunua kete,” anasema.
Anataja vyanzo vyake vya mapato kuwa ni ‘kupiga debe’ na kuuza chupa tupu za maji.
 Hussein ni kijana rijali, ambaye anakiri  kuwa wakati mwingine hushikwa na matamanio ya kimapenzi.
Suluhisho la tamaa zake za mwili analo, akielezaa kuwa hupatikana eneo la Mwanyamala A.
“Pale ‘A’ kuna danguro, ukitaka mwanamke unalipa Sh 2000 kwa ‘shorttime’, nikipata hela  mara moja moja mi huenda huko,” anasema.
Ipo sababu inayomfanya Hussein kwenda danguroni, nayo ni hii: “Najua siwezi kupata ‘demu’ (mwanamke) wa kudumu kutokana na nini ujue? Hali yangu hii, mchafu, wasichana hawawezi kunikubali,” anasema.
 Hussein anakana kuwa, wanaotumia dawa za kulevya, hawana nguvu za kiume.
Anasema: “Tuna nguvu kama kawaida, lakini hatuwezi kuwa na mke au msichana  wa kudumu,”
 Pamoja na kutoa ujira, anadai kuwa, hata wanawake wanaofanya biasharaya ngono, huwafukuza na kuwaambia wakaoge kabla ya kuanza kufanya nao mapenzi.
Hussein kama walivyo wenzake hulala katika nyumba na magari mabovu au katika vibaraza vya maduka.
Mwingine ni Rashid Mkubwa au Chidi, yeye anasema, kutumia dawa za kulevya ni starehe yake, wala hategemei kuacha.
“Ukweli dada yangu siwezi kuacha kete, hata iweje, hii ndiyo inayonipa raha, kila mtu na starehe yake,” anasema.
 Kijana  huyo ambaye hakuwahi kwenda shule, anasema, alizaliwa mkoani Morogoro na baadaye akiwa na umri wa miaka 10 alitoroka na kuja jijini.
“Nilifika nikiwa mdogo, wakaniita mtoto wa mitaani, lakini sasa hivi nishakuwa mtu mzima siyo?” anasema  huku akicheka.
Anasema ameshazoea kuishi maisha ya kulala katika vibaraza, katika mapagala (majengo yasiyoisha ujenzi ) au hata mahabusu.
“Nimeshawahi kufungwa jela mara kadhaa, nimeshawahi kupigwa na wananchi, kila tabu nimepitia,” anasema
Kijana huyu, mwenye umbile la miraba minne, ambaye sura yake imejawa na makovu, hana wasiwasi na anajiamini kwa kila asemalo.
Hanipi muda mrefu wa kuzungumza naye na anaondoka, akiendelea kunadi mabasi ya abiria.
Vilevile, yupo Joel kwa maelezo ya wenzake, ametokea katika familia inayojiweza, lakini pengine ni ujana au utukutu ndiyo uliomweka hapa.
“Nilitoroka ‘home’ nikaenda afrika kusini, huko nikajifunza kula unga,” anasema Joel.
 Joel, pamoja na familia yake kuwa inayojiweza, lakini kutwa hushinda eneo la  Tabata, Mawenzi, jijini Dar es Salaam akinadi au kuosha mabasi ya abiria.
 Anasema, kwa kuwa wazazi hawawezi kumpa fedha ya kununua unga na hana kazi ya kumuingizia kipato ndiyo maana amejiajiri kwa kupiga debe.
Marafiki zao wa karibu ni makondakta wa mabasi ya abiria (daladala), hawa ama huwapa Sh 200 kwa ajili ya kuwahurumia au kama ujira.
Robert Kihuna anasema: “Mateja wana matatizo yao, na wana wema wao, hatuwezi kusema ni wabaya kwa asilimia 100”
 Anasema,  ubaya  wao ni  kuwa baadhi yao ni wezi, lakini wanachokifanya kwao ni huruma tu, si kwa sababu mateja wanafanya kazi kubwa au ya muhimu.
“Kama ni kupiga debe, mimi mwenyewe napiga, sasa yeye wa kazi gani, tunawapa hizi 200 za bure tu,” anasema.
 Matumizi ya dawa za kulevya yanaongezeka siku hadi siku.
Ripoti  kutoka  tume ya udhibiti dawa za kulevya inasema, dawa hizi hutumiwa na watu kati ya milioni 155 na 250.
Dawa za kulevya duniani,  ni biashara kubwa inayokadiriwa kufikia dola bilioni 320 kwa mwaka, kiasi ambacho ni karibu asilimia moja ya pato lote la dunia.
Taarifa za ukamataji kutoka Jeshi la Polisi, mwaka 2010 zinaonyesha kilo 185 za heroin na nyingine 62 za cocaine zilikamatwa, kiasi ambacho ni zaidi ya kile kilichokamatwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

 Wilaya au Manispaa ya Kinondoni inatajwa kuongoza kwa kuwa na watumiaji wengi wa dawa hizi ukilinganisha na wilaya nyingine mkoani Dar es Salaam.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.