WAZIRI BITEKO ATEMBELEA SOKO KUU LA DHAHABU GEITA
Aahidi kuongeza Madawati Manne kuboresha huduma
Na Antony Sollo Geita.
WAZIRI wa Madini Mheshimiwa Dotto
Mashaka Biteko akiongozana na Ofisa Madini Mkoa wa Geita Bwana Daniel Mapunda
leo julai 23 wametembelea Soko Kuu la Dhahabu lililopo katika Halmashauri ya
Mji wa Geita na kujionea namna wadau wa Sekta ya Madini walivyoitikia wito wa
Serikali wa kuwataka wadau kuuzia Madini katika Soko hilo ili kuiwezesha
Serikali kupata taarifa za Mapato pamoja na kuwatambua wadau wa Sekta hiyo.
Baada ya kuwasili katika Soko
hilo Waziri Biteko pamoja na Ofisa Madini walikuta umati mkubwa wa watu
waliofurika katika viunga vya Soko hilo kwa ajili ya kupata vibali ili waweze
kuuza Madini yao kwa njia ya halali ambapo Waziri Biteko aliwapongeza kwa namna
walivyoitikia wito wa Serikali na kuwaahidi kuongeza Madawati (4) kwa ajili ya
upimaji kwenye Soko Kuu ili waweze kuboresha huduma kwa wateja.
“Nimefurahishwa na namna
mlivyojitokeza na kuitikia wito wa Serikali,niwaombe ndugu zangu muwe
wavumilivu wakati Serikali inafanya mchakato wa kuongeza Madawati (4) ambayo
yatasaidia kuhudumiwa kwa haraka”alisema Biteko.
Kwa sasa Soko Kuu la Madini la
Mkoa wa Geita lina dawati (1) linalohudumia wateja kati ya 30 hadi 80 kwa siku
ambapo idadi hiyo imeongezeka kwa kasi jambo linalowapa usumbufu wateja na hilo
ndilo limepelekea kumshawishi Waziri Biteko kuona kuwa kuna haja ya kuongeza
Madawati manne ili kuboresha huduma.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Ofisi ya
Madini Mkoa wa Geita,idadi ya wateja imeongezeka sana kwa kipindi cha kuanzia
julai 20 mwaka huu ambapo kuanzia tarehe 20 hadi 23 julai mwaka huu wateja
wameongezeka kufikia 280 kwa siku tofauti na kipindi cha nyuma ambapo kulikuwa
na idadi ndogo ya wateja kati ya 30 hadi (70) kwa siku.
Ujio wa Waziri Biteko umeleta
faraja kwa wadau wa Sekta ya Madini ambapo wamesema utaondoa kero za wadau wa
Sekta hiyo na kwamba mwishoni mwa wiki hii wachimbaji wadogo waliliambia
Tanzania Daima kuwa kuna changamoto ya Masoko na watumishi wanaowahudumia
katika maeneo mbalimbali yanapopatikana Madini ya Dhahabu Mkoani Geita na
kuiomba Serikali iongeze watumishi ili kuboresha huduma hiyo.
MWISHO
No comments: