MBUNGE MUKASA APONGEZWA KWA KUSAIDIA SHULE YA SEKONDARI
Na Antony Sollo Biharamulo.
MBUNGE wa Jimbo la Biharamulo Magharibi Oscar Mukasa
amepongezwa na Bodi ya Shule ya Sekondari ya Kagango iliyopo
Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera baada ya kufanikisha kuitafutia
ufadhili wa Shule hiyo ili kukamilisha ujenzi wa Bweni la Wavulana kidato
cha Sita.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa niaba ya Bodi ya
Shule hiyo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kagango Tumaini France
alisema Bodi hiyo imefurahishwa na namna Mbunge huyo alivyoshiriki
kikamilifu kuitafutia msaada Shule hiyo ili iweze kufanikisha ujenzi wa
bweni la wanafunzi hao.
“Kwa niaba ya Bodi ya Shule hii napenda kumpongeza
kwa dhati Mbunge
wetu kwa kuona umuhimu wa Elimu na kupigania kwa
hali na mali upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi
wa bweni hili,tumeuona mchango wake tunauthamini na
tutaendelea kuuenzi”alisema Mwalimu France.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo ujenzi wa bweni
hilo umekamilika kwa gharama ya Shilingi Mil 10,000,000 fedha ambazo
zilitolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) baada ya Mbunge huyo
kutafuta ufadhili kutoka katika Mfuko wa Mamlaka ya Elimu (TEA) na kuongeza
kuwa tayari Bweni hilo limekamilika na limeshaanza kutumika.
Changamoto zingine zinazoikabili Shule hiyo ni
viwanja vya michezo,vyumba vya madarasa,mabweni matatu,ukumbi wa
mikutano kwa ajili ya watoto pamoja na Samani zake,(Usafiri )Basi
la Shule kwa ajili ya Safari za Mafunzo .
France amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza na
kuisaidia Shule hiyo
kutokana na changamoto nyingi zinazoikabili.
“Tunawaomba wadau mbalimbali wa Elimu Wilayani
pamoja na Mkoa mzima wa Kagera kujitokeza ili kuisaidia Shule hii kwani
inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni pamoja na upungufu wa
matundu ya vyoo,Zahanati ya Shule,kutokana na idadi kubwa ya
wanafunzi”alisema France.
Hata hivyo kutokana na umri wa Shule hiyo
unahitajika ukarabati mkubwa pamoja na kuongeza majengo na Maktaba pamoja na
vitabu mbalimbali kwa ajili ya kuwaongezea uelewa wanafunzi katika Shule
hiyo.
Jiwe la Msingi la Shule ya Kagango liliwekwa Feb15
1990 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya pili
ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Ally Hassan
Mwinyi ambaye kwa sasa ni Rais Mstaafu takribani miaka 29 iliyopita.
Katika kutafuta kujua Mbunge Mukasa atakabiliana
vipi na changamoto zilizopo katika Shule hiyo Tanzania Daima
lilimtafuta ili kuzungumza ambapo alisema kwa sasa hawezi kuzungumzia ahadi kwa
kuwa anahitaji kuja kukaa na uongozi ili kujaili kwa kina na kuona
namna ya kutafuta wafadhili watakaotoa fedha kwa ajili ya kuboresha
mapungufu hayo.
“Siwezi kuzungumzia juu ya nini nitafanya kwa sasa
hadi nitakapokaa na uongozi ili kujadili kwa kina na kuona namna ya
kutafuta wafadhili wengine watakaotoa fedha kwa ajili ya kuboresha
mapungufu hayo” alisema Mukassa.
MWISHO.
No comments: