POLISI YANASA KUMI NA NANE ZIWA VICTORIA
Na Antony Sollo Mwanza
JESHI la polisi Mkoani Mwanza
liwanashikilia watu kumi na nane (18 kwa makosa mabalimbali ya kiuhalifu katika
operesheni maalumu iliyofanyika Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza na katika
maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa
Polisi Mkoani Mwanza DCP: Ahmed Msangi imeeleza kuwa,Operesheni hiyo ilianza
August 02.08.2018 hadi tarehe 03.08.2018 katika maeneo mbalimbali ya ndani ya
ziwa Victoria na katika vijiji vilivyopo pembezoni mwa ziwa hilo wilayani
Sengerema Mkoani Mwanza.
Operesheni hiyo maalumu
ilishirikisha kikosi maalumu cha askari polisi Mkoa, Polisi Wanamaji (Police
Marine) pamoja na Askari polisi toka Wilaya ya Sengerema kilichoongozwa na
Operesheni Afisa Mkoa wa Mwanza SSP: Audax Majaliwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya
Sengerema SSP: Mairi Wassaga na kufanikiwa kukamata watuhumiwa kumi na nane
(18) wa makosa mbalimbali ambayo ni pamoja na
kupatikana na samaki wachanga kilo 125, kupatikana na nyavu haramu
hamsini (50) za kuvulia samaki aina ya timba na kupatikana na bangi kilo mbili
(2)pamoja na kupatikana na pombe ya moshi (gongo) lita 265, kupatikana na
pikipiki moja izaniwayo kuwa ya wizi yenye namba MC 242 BDK na nyavu haramu 600
za kuvulia dagaa.
Imeelezwa kuwa kabla ya zoezi
hilo jeshi la polisi walipokea taarifa toka kwa raia wema kwamba katika baadhi
ya maeneo ya vijijini, pembezoni mwa ziwa Victoria na baadhi ya visiwa
vilivyopo Wilayani Sengerema kulikuwa na watu waliokuwa wakijihusisha na
biashara haramu ya pombe aina ya gongo, uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya
aina ya bangi, wizi wa vitu mbalimbali, uvuvi wa kutumia nyavu haramu makokoro,
uvuvi wa samaki wachanga na vitendo vingine vya kiuhalifu.
Baada ya kupatikana kwa taarifa
hizo kuliandaliwa kikosi kazi Maalumu cha Askari polisi Mkoa kilichoshirikiana
na polisi wanamaji mwanza na askari polisi toka Wilaya Sengerema hivyo msako
mkali ulifanywa kwa pamoja katika maeneo yote ya majini na nchi kavu na baadae
askari waliweza kufanikiwa kukamata wahalifu kumi na nane wa makosa mbalimbali.
Mpaka sasa Jeshi la Polisi lipo
katika upelelezi na mahojiano na watuhumiwa wote, ili kuweza kuwabaini wale
wote wanaoishirikiana nao kwa namna moja
au nyingine katika kutenda uhalifu huo ambapo Kamanda Msangi amesema kuwa uchunguzi
ukikamilika watuhumiwa wote kumi na nane watafikishwa Mahakamani.
Vilevile msako mkali wa
kuwatafuta watu wanaojihusisha na uhalifu wa aina kama hii katika maeneo yote
ya jiji na Mkoa wa Mwanza bado unaendelea ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi ametoa wito kwa wakazi wa Jiji na
Mkoa wa Mwanza kuacha tabia ya kujihusisha na uhalifu kwani utawaletea matatizo
na baadae kufungwa na kupelekea kutengana na familia huku akiwataka kufanya
halali zitakazoweza kuwaingizia kipato sambamba na hilo Msangi amewaomba
wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu
na wahalifu mapema ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya Sheria.
MWISHO
No comments: