Ads Top

GARI la Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara

Na Antony Sollo Geita.

GARI la Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara lenye namba za usajili STK 9565 aina ya Toyota Landcruiser likiendeshwa na Dereva Lucas Charles limepata ajali na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi wanne likitokea Mkoani Kagera likielekea Jijini Mwanza.

Ajali hiyo imetokea majira ya saa saba mchana katika kijiji cha Minkoto Kata ya Bwanga Wilaya ya Chato Mkoani Geita ambapo kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo gari hilo lilikuwa likimkwepa mtoto wa miaka saba aliyekuwa akikatisha barabara hali iliyosababisha dereva kushindwa kulimudu vyema gari jambo lililosabibisha gari kupoteza mwelekeo na kupinduka na kisha kumgonga mtembea kwa miguu mwanamke aliyejulikana kwa jina la Semeni Kibiriti (36) mkazi Songambele.

Katika ajali hiyo watu wanne walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita ambapo mmoja wa Majeruhi hao ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar Es Salaam na ambaye alikuwa ni Afisa Habari wa Wizara ya Viwanda na Biashara na Uwekezaji Shadrack Sagati alifariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoani Geita Mponjoli Mwabulambo aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Shadrack Sagati 44 na mtembea kwa miguu Semeni Kibiriti 36 mkazi wa Songambele na kusema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari hilo kumkwepa mtoto aliyekuwa anakatisha barabara.

“Dereva alionyesha umahili mkubwa katika kuhakikisha kuwa anaokoa kutokea kwa ajali hiyo lakini gari lilimshinda na kusabisha kupoteza mwelekeo na kumgonga mtembea kwa miguu Semeni Kibiriti na kusababisha kifo huku watu watano waliokuwa ndani ya gari hilo wakijeruhiwa vibaya na mmoja kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita”alisema Kamanda Mwabulambo.

Kamanda Mwabulambo aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Ludovick James Yusuf Mbarwe Mkaguzi wa Ndani wa Wizara hiyo,Nickson Matembo Mchumi wa Wizara hiyo,Lucas Charles Dereva wa Gari hilo pamoja na Shadrack Sagati aliyekuwa Afisa Habari wa Wizara hiyo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita Brian Mawala alithibitisha kupokea majeruhi watano ambapo mmoja wa Majeruhi hao Shadrack Sagati 44 alipoteza maisha akipatiwa matibabu katika Hospitali hiyo huku Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Ludovick James Yusuf Mbarwe Lucas Charles na huku Nickson Matembo akiwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa Mahututi akiendelea kwa uangalizi wa karibu.

MWISHO.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.