Makubaliano ya kusitisha mapigano Syria yavunjika
Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa ajili ya sikukuu ya Eid al-Adha
ambayo ilianza Ijumaa, kimsingi ilikubaliwa na serikali na waasi wa
jeshi linalopigana ili Syria iwe huru, FSA, yalileta uwezekano wa
kusitishwa kwa mara ya kwanza kwa mapigano baada ya mzozo uliodumu miezi
19 sasa.
Baada ya kuzuka kwa mapigano hayo mapya siku ya Ijumaa na Jumamosi ,
waasi pamoja na kundi linaloangalia hali nchini Syria wamesema kuwa
makubaliano hayo ya kusitisha mapigano kwa hakika yamekufa.
Ndege zashambulia
Wakati mapigano baina ya majeshi ya serikali ya
rais Bashar al-Assad na waasi yakiendelea, ndege za kivita za Syria
zilishambulia jengo katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi mashariki ya
mji mkuu wa Damascus , sehemu ambayo imeshuhudia mapigano makali kwa
muda wa wiki kadha, na kusababisha vifo vya watu wanane.
"Haya ni mashambulio ya kwanza ya anga tangu kutangazwa, kusitishwa
mapigano kwa muda wa siku nne katika wakati wa sikukuu ", limesema kundi
linaloangalia haki za binadamu nchini Syria.
"Makubaliano hayo yamekufa," mkurugenzi wa kundi hilo Rami Abdel
Rahman amesema. "Hatuwezi tena kuzungumzia kuhusu kusitishwa mapigano."
Shambulio jingine la anga limefanyika karibu na kituo cha kijeshi cha
Wadi Deif katika jimbo la kaskazini magharibi la Idlib, ambako waasi
wamekuwa wakipambana katika azma ya kuteka kituo hicho, kundi hilo
limesema.
Makubaliano yamekufa
Kamanda wa waasi katika mji wa kaskazini wa
Aleppo amesema kuwa hakuna shaka kuwa juhudi za kusitisha mapigano ,
zilizopendekezwa na mjumbe wa kimataifa wa amani Lakhdar Brahimi ,
zimevunjika.
"Hii ni kushindwa kwa Brahimi. Juhudi hizi zimekufa
kabla hazijaanza," Abdel Jabbar al-Okaidi, mkuu wa baraza la kijeshi la
waasi mjini Aleppo , ameliambia shirika la habari la AFP kwa simu.
Amesisitiza kuwa jeshi la waasi la FSA halijavunja makubaliano hayo ya kusitisha mapigano na linachukua tu hatua za kujihami.
"Nimekuwa katika maeneo mbali mbali ya mstari wa mbele wa mapambano
jana na jeshi la serikali halijaacha mashambulio yake ya makombora,"
Okaidi amesema. "Jukumu letu ni kuwalinda raia, na si sisi ambao
tunashambulia."
Lakini jeshi la serikali limewashutumu waasi kwa kuendelea kukiuka makubaliano na kuapa kuwa litajibu ukiukaji huo.
Jeshi la Syria
"Kwa siku ya pili, makundi ya kigaidi yameendelea
kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa na kuheshimiwa
na uongozi wa jeshi la serikali," jeshi la Syria limesema katika taarifa
iliyosomwa katika televisheni.
"Jeshi litaendelea kufuatilia hatua hii ya ukiukaji wa makubaliano, na kujibu mashambulio dhidi ya vitendo hivi vya wahalifu.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Jihad Maqdisi amesema kuwa jeshi
la nchi hiyo linania ya kuendelea kwa hatua ya kusitisha mapigano, na
kuwalaumu waasi kwa kuchochea hatua ya kulipiza kisasi kutoka jeshi la
serikali.
Mahujaji waandamana
Wakati huo huo, maafisa nchini Saudi Arabia
wamewatawanya haraka waandamanaji kadhaa ambao ni mahujaji kutoka Syria
wanaotaka kuangushwa kwa rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad na kushutumu
kile walichokisema kuwa ni kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuzuwia
umwagikaji wa damu nchini Syria.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters na watu walioshuhudia
waandamanaji walibeba bendera ya waasi na kufanya maandamano kuelekea
daraja la Jamarat katika eneo la Mina, mashariki ya mji mtakatifu wa
Mecca nchini Saudi Arabia, ambako zaidi ya mahujaji wa Kiislamu milioni 3
walikusanyika kwa ajili ya hija inayofanyika kila mwaka.
No comments: