Orodha ya Watanzania wenye akaunti Uswiss inakuja
Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(CHADEMA), Zitto Kabwe
“ Kwa nchi za wenzetu magazeti ya uchunguzi yanafanya kazi
hizi. Kwetu magazeti yanasubiri wanasiasa wafanye. Orodha ya Watanzania wenye
akaunti Uswiss inakuja. Hoja Binafsi kuhusu suala hili imeruhusiwa na sasa
naandaa maelezo ya Hoja. Sio suala la kutaja orodha tu bali pia hatua za
kuchukua dhidi ya fedha hizo na wenye fedha haramu zilizofichwa huko.
Zitto Kabwe Kuna baadhi ya Watanzania wenzangu wanabeza kazi
hii. Ninachowaambia sitakata tamaa. Ninaifanya kazi hii kwa umakini mkubwa kwa
kuwa najua uhatari wake. Sikurupuki tu. Ninafanya kazi hii kwa niaba ya Kambi
ya Upinzani nikiwa Waziri kivuli wa fedha. Hii ni kazi ya CHADEMA, sio kazi ya
Zitto. Wengine wanasema mbona 'list of shame' tulitaja majina. Ni kweli. Lakini
ilituchukua wiki kadhaa kutaja majina. Katika mkutano wa Jangwani wakati
napokelewa kutoka Bungeni baada ya kusimamishwa ubunge kufuatia hoja ya
Buzwagi, tuliahidi mbele ya umma kutaja orodha ya mafisadi. Tukataja wiki 3
baadaye mnamo Septemba 15, 2007. Tulifanya kazi ile kwa umakini sana.
Tutaifanya kazi hii ya Watanzania wenye akaunti huko uswiss kwa umakini zaidi.
Tutaweka wazi majina ya Watanzania wenye akaunti Uswiss kwa
utaratibu na umakini. Nitataja orodha hiyo Bungeni na kamwe sitataja nje ya
Bunge. Hii ni kazi kubwa inahitaji utulivu. ” ~ Zitto Kabwe
WAKATI serikali
ikishindwa kuwataja vigogo walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi, Mbunge
wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, anatarajia kuwasilisha hoja binafsi
katika mkutano wa tisa unaotarajiwa kuanza wiki ijayo mjini Dodoma, kutaka
serikali irejeshe fedha hizo.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, amesema
tayari hoja hiyo imeshapata baraka za Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Mbunge huyo wa CHADEMA alisema hayo jana wakati wa akifunga
mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Nanjarareha,
wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika leo, CHADEMA
imemsimamisha, Frank Salakana. Alisema sh bilioni 349 zilizofichwa Uswisi na
baadhi ya vigogo wa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), lazima zirejeshwe
nchini, huku akimtaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU), Edward Hosea, kueleza umma barua aliyoituma nchini humo kwa ajili
ya kashfa hiyo ilikuwa na lengo gani.
Alisema barua ya Dk. Hosea imesababisha ugumu wa upatikanaji
wa taarifa za mabenki ya nchini Uswisi ambayo yameshindwa kutoa ushirikiano kwa
kamati inayofuatilia kashfa hiyo.
Huku akishangiliwa na maelfu ya wanachama wa CHADEMA
waliofurika kusikiliza mkutano huo, Zitto alisema wizi wa mabilioni hayo
umetokana na kuporomoka kwa maadili ya viongozi nchini ambao wengi wanajali
zaidi masilahi binafsi badala ya umma.
Mbunge huyo machachari wa CHADEMA, alisema kuna haja kama
taifa kurejesha maadili ya uongozi kama enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere ili
viongozi wachague kitu kimoja, kati ya biashara na siasa.
Alisema CHADEMA imepania kuhakikisha mabilioni hayo
yanarejeshwa ili yaweze kutumika kuwasaidia Watanzania katika kujenga na
kuboresha miundombinu ya barabara, maji na afya.
Aliwataka viongozi walioficha mabilioni hayo kujitokeza
mapema na kueleza jinsi walivyozipata badala ya kusubiri kuumbuliwa.
“Nawataka viongozi waliohusika wajitokeze wenyewe, waeleze
walivyozipata na kisha wazirejeshe nchini, vinginevyo patachimbika, kwani
nitahakikisha kama chama tunashirikiana na Benki ya Dunia kuhakikisha fedha
hizo zinarudi nchini,” alisema Zitto.
Alisema CHADEMA inapigania fedha hizo zirejeshwe kwani
zimetokana na wizi wa rasilimali za Watanzania kupitia mikataba mibovu ya
mafuta na wizi wa madini na nyingine.
Katika ripoti ya Swiss Central Bank, iliyotolewa hivi karibuni,
inaonesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 barani Afrika ambazo vigogo
wake wa kibiashara, kitawala na kisiasa wameficha kwa siri mabilioni ya fedha
katika mabenki ya Uswisi.
Nchini nyingine za Afrika zilizoficha fedha hizo ni Kenya,
Uganda, Zimbabwe, Misri, Shelisheli, Afrika Kusini, Rwanda, Sierra Leone,
Somalia na Sudan.
Kwa upande wa Tanzania, mapesa ambayo yamefichwa huko ni
dola milioni 196.87, sawa na shilingi za Tanzania bilioni 315.5!
Hebu jiulize; mapesa haya tuliyoibiwa yangetusaidia kiasi
gani kama yangerejeshwa nchini na kutumbukizwa kwenye miradi ya kuboresha
huduma za jamii?
Pia jiulize swali jingine: Je, hata baada ya Benki Kuu ya
Uswisi kuturahisishia mambo kwa kututobolea ukweli kwamba tumeibiwa, na kwamba
wezi wetu wameficha hizo fedha nchini mwao, watawala wetu wana dhamira ya
kuanzisha mchakato ili wahusika wafikishwe mahakamani na fedha hizo zirejeshwe
nchini?
No comments: