JOHN MNYIKA :MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO KUPITIA TIKETI YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) AWASILISHA MUSWADA BINAFSI WA SHERIA YA KUUNDA BARAZA LA TAIFA LA VIJANA
Mbunge wa Jimbo la Ubungo-CHADEMA,Mh John Mnyika
Juzi tarehe 4 Januari 2012 niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge taarifa ya muswada binafsi wa Sheria ya kuunda Baraza la Taifa
la Vijana (The National Youth Council Bill, 2013) kwa mujibu wa Kanuni ya 81
(1) na Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
Nimechukua
hatua hiyo kwa kuwa kwa miaka zaidi ya kumi Serikali imekuwa ikiahidi karibu
kila mwaka bungeni kuwa itawasilisha muswada wa kuunda baraza la vijana la
taifa lakini haijawahi kutekeleza ahadi hiyo; nimeamua kuitekeleza ahadi hiyo
kwa kupeleka bungeni muswada binafsi wa kuunda baraza la vijana la taifa.
Katika taarifa hiyo ya muswada
nimewasilisha madhumuni, sababu pamoja na nakala ya muswada wenyewe wa
sheria ya kuanzisha Baraza la Vijana la
Taifa kwa madhumuni ya kuanzisha chombo cha kuwaratibu vijana wa Tanzania katika kutekeleza shughuli zao
kijamii, kuuchumi, kiutamaduni na kimichezo, na kuchagiza hali ya utambulisho
wa Kitaifa wa pamoja na uzalendo.
Baraza
litawawezesha vijana kukutana na kushughulikia masuala ya kisera na kisheria
yanayogusa maslahi ya vijana kupitia njia mbalimbali kama zinavyopendekezwa
katika muswada huo katika ngazi na maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika
kitaifa, kiwilaya, kikata na kivijiji/kimitaa.
Muswada
pia utawezesha vijana kuwa na mfuko wa fedha ambazo kwazo vijana wataweza
kutekeleza shughuli hili kufikia malengo ya Baraza ikiwemo ya kuwezesha
utekelezaji wa sera ya taifa ya maendeleo ya vijana.
Muswada
huo umegawanyika katika sehemu nane kama ifuatavyo: Sehemu ya Kwanza ya muswada huu inatoa
utangulizi kwa kutamka jina la sheria na mipaka ya sheria na tafsiri za maneno
yanayotumika kwenye muswada.
Sehemu
ya Pili ya muswada huo inapendekeza
kuundwa kwa Baraza la Vijana, kazi na majukumu yake, na zaidi kuanzisha nafasi
ya mwenyekiti wa Baraza.
Sehemu
ya Tatu ya muswada huo inapendekeza
kuundwa kwa Bunge la Baraza, Bodi ya Baraza na Bodi ya Washauri wa chama kama
sehemu Baraza pamoja na vyombo vingine.
Sehemu
ya Nne ya muswada huo inapendekeza kuazishwa mfuko wa fedha
wa Baraza kwa madhumuni ya kuwezesha utekelezaji wa kazi za Baraza kama
zilivyoainishwa kwenye muswada.
Sehemu
ya Tano, ya muswada huo inapendekeza kuundwa kwa sekretarieti kwa madhumuni ya
kuwa watekelezaji wa shughuli za siku kwa siku za Baraza.
Sehemu
ya Sita, ya muswada huo inapendekeza
kuanzishwa kwa Majukwaa ya Vijana katika ngazi ya Halmashauri, na Kamati za
Vijana za Kata, Vijiji na Mitaa kwa madhumuni ya kuzishusha chini shughuli za
vijana kwenye ngazi ya chini kabisa.
Sehemu
ya Saba, ya muswada inapendekeza
kusajili asasi na taasisi shiriki za Baraza zinazoongozwa na vijana na vigezo
vitakavyotumika kusajili asasi na taasisi hizo.
Sehemu
ya Nane, ya muswada inapendekeza
kuanzishwa kwa siku na juma la vijana, na zaidi inampa nguvu waziri kutunga
kanuni kwa uendeshaji bora wa shughuli za Baraza.
Itakumbukwa
hata kabla kuwa mbunge kwa nyakati mbalimbali nimeungana na vijana wengine kwa
zaidi ya miaka kumi kutaka kuundwe Baraza la Taifa la Maendeleo ya Vijana kwa lengo la
kuwaunganisha vijana bila kujali tofauti zao zingine katika kushughulikia
vipaumbele mbalimbali vya vijana ikiwemo katika masuala ya elimu, ajira, afya,
michezo na maisha ya vijana kwa ujumla.
Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge
niliungana na wabunge wengine kuhoji bungeni na serikali iliahidi kwamba
mchakato wa kuundwa kwa baraza hilo ungekamilika katika mwaka wa fedha
2011/2012, hata hivyo mpaka kipindi hicho kinamalizika mwezi Juni 2012 na
kuanza kwa mwaka mwingine wa fedha 2012/2013 ahadi hiyo haijatekelezwa.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John
Mnyika
Mbunge
wa Jimbo la Ubungo
05
Januari 2012
No comments: