Shahidi wa kwanza kutoka upande wa mashtaka, amefika mbele ya mahakama ya kimataifa ICC kutoa ushahidi dhidi ya naibu Rais wa Kenya William Ruto
Mahakama inamlinda shahidi huyo kwa kutoonyosha sura yake.
Shahidi alianza kwa kuahidi kusema
ukweli. Alielezea ambavyo familia yake ilijiunga na mamia ya watu wa
kabila la Kikuyu wakiwa na magodoro yao pamoja na blanketi.
Walikuwa wanatafuta hifadhi katika kanisa la
Assemblies of God church katika kijiji cha Kiambaa karibu na mji wa
Eldoret ambalo liliteketezwa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu
thelathini waliokuwa wamekimbilia usalama wao.
Hii ilikuwa baada ya wenyeji wa kabila la
Kalenjin kuwaonya kuwa wangeadhibiwa vikali ikiwa wangekosa kupigia kura
chama cha kisiasa cha ODM kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila
Odinga.
Shahidi huyo anatoa ushahidi wake akiwa nyuma ya
kitambaa cha dirisha ndani ya mahakama huku kwenye TV sura yake ikiwa
imezuiwa kuonekana ili kulinda usalama wake.
Naibu Rais William Ruto naye alitizama kutoka upande wa kushoto lakini sura yake imebanwa kabisa, hawezi kuonekana,.
Ushahidi wake unagusia siku ya tarehe mosi mwezi
Januari. Aliambia mahakama kuwa maelfu ya watu walikuwa wanakuja
kuizingira kanisa hiyo wakiimba huku wakiwa wamefunika nyuso zao kwa
matope, wengi walikuwa wanavalia vitambaa kwenye vichwa vyao.
Alisema kuwa walikuwa wamjihami kwa mapanga na
silaha zengine za kijadi , panga , shoka na viboko huku akisema kuwa
aliweza kumtambua mwansiasa mmoja miongoni mwa vijana hao kutoka chama
cha ODM.
Ruto anakabiliwa na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007-2008
Kesi dhidi ya Ruto na mshtakiwa mwenzake Joshua
Arap Sang, ilianza tarehe 10 mwezi Septemba, baada ya wawili hao
kutuhumiwa kuhusika na ghasia hizo, kwa njia ya kuzipanga na kutekeleza.
Kumekuwa na wasiwasi kuhusu mashahidi kujiondoa
kwenye kesi hiyo wakihofia usalama wao. Mwishoni mwa wiki, mashahidi
wanne walijiondoa katika kesi hiyo baada ya kuelezea wasiwasi kuhusu
usalama wao ikiwa watatoa ushahidi mbele ya mahakama hiyo.
Wiki jana jaji mkuu kwenye kesi hiyo,
aliiakhirisha kesi kwa sababu mashahidi hawakuwa wamefika kwenye
mahakama hiyo kutoa ushahidi wao.
Rais Uhuru Kenyatta, anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo mwezi Novmba kwa mashtaka sawa na hayo.
Habari na BBCSwahili.com
No comments: