Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwafokea wafanyakazi wawili
wa kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation kutoka China
baada ya kufumwa na msafara wake wakiiba mafuta ya Diesel kwenye tanki
la lori la la kumwagilia maji (Boza) la kampuni hiyo tarehe 19 Novemba
2013 Katika kijiji cha Ntendo Manispaa ya Sumbawanga. Mkuu huyo wa Mkoa
alikemea tabia hiyo ya wafanyakazi wezi na kusema umekua ni ugonjwa wa
mda mrefu unaozorotesha kukamilika kwa ujenzi wa barabara za lami
zinazoendelea kujengwa Mkoani Rukwa.
Wafanyakazi hao waliokamatwa ni dereva William Ebron (kulia pichani)
na
kibarua Isaya Godwin ambao walifumwa majira ya saa nne asubuhi
wakinyonya mafuta kwenye tanki la Lori hilo lenye namba za usajili T-518
BDV mali ya kampuni hiyo kwa kutumia mpira wa kupitishia maji na
kumuwekea mteja kwenye dumu la lita tano, hata hivyo mteja huyo
alifanikiwa kukimbia. Baada ya kuhojiwa walidai kuwa mteja wao huyo
angelipia lita hizo tano kwa Tsh. 3500/= bei ambayo kihalali haiwezi
kununua japo lita mbili za mafuta hayo katika soko.
Msafara
wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ulikua ukielekea katika kata ya Mtowisa kwa
ajili ya shughuli za kuhamasisha maendeleo ambapo ulikumbana na mkasa
huo njiani katika Kijiji cha Ntendo. Barabara ya Sumbawanga - Namayere
inajenga kwa kiwango cha lami na mkandarasi Jiangxi Geo-Engineering
(Group) Corporation kutoka China chini ya Mhandisi Mshauri Nicholas
O’Dwyer and Company Limited kutoka Ireland akishirikiana na Apex
Engineering Ltd. kutoka Tanzania kwa gharama ya Sh. bilioni 78.8
ambazo ni fedha za ndani.
Watuhumiwa William Ebron (kulia) na kibarua Isaya Godwin (kushoto) muda mfupi baada ya fumanizi wakiwa hawana cha kujitetea.
Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya akiwakabidhi wezi hao kwa
vyombo vya usalama ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Watuhumiwa wakiwa mikononi mwa Polisi.
Mashuhuda wa tukio hilo.
Baada
ya kuanza ziara yake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa akimuapisha Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Adam Misana (wapili kulia) na baadhi
ya watendaji wa Kata ya Mtowisa na Kijiji cha Muze juu ya utekelezaji
wa maazimio na makubaliano waliowekeana. Maazimio hayo ni pamoja na
kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shuguli za maendeleo ya
vijana, kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wakulima na wafugaji katika
kila kijiji kuepusha migogoro ya wakulima na wafugaji, kuwekeana
utaratibu maalum wa idadi ya mifugo inayotakiwa kufugwa kulingana
na ukubwa wa maeneo husika, uhifadhi wa mazingira hususani ujenzi wa
vyoo kuepukana na maradhi ya milipuko pamoja na maagizo mengine
mbalimbali yaliyotolewa na Mkuu huyo wa Mkoa.
Katika
ziara yake hiyo alifanya mikutano minne ikiwepo miwili ya nje na miwili
ya ndani ambapo maagizo mbalimbali kwa ngazi ya Wilaya, Halmashauri na
vijiji yalitolewa kwa watendaji husika.Picha na Hamza Temba - Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa Rukwa
No comments: