Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki nchini Afrika Kusini zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili nchini siku ya Ijumaa, Novemba 15, 2013.
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akitia saini kitabu
cha maombelezo ya kifo cha Mjumbe wa Tume hiyo Dkt. Sengondo Mvungi
nyumbani kwake Kibamba jijini Dar es Salaam.
Rais
Jakaya Kikwete (katikati) akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba (kushoto) nyumbani kwa
marehemu Dkt. Sengondo Mvungi walipokwenda kuipa pole familia. Kulia ni
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia na Mjumbe wa Tume Waziri Mkuu
Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba wakifurahia jambo
na Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe (kushoto), Makamu
Mwenyekiti wa Tume Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani na Mjumbe wa
Tume Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim (kulia) walipokutana
nyumbani kwa marehemu Dkt. Sengondo Mvungi Kibamba jijini Dar es Salaam.
Mjumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Richard Lyimo akimpa pole mke wa
marehemu Dkt. Sengondo Mvungi, Bi. Anna Mvungi wakati Wajumbe wa Tume
walipokwenda kumpa pole.Picha na Tume ya Katiba
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa taratibu za
kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi aliyefariki
nchini Afrika Kusini zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili
nchini siku ya Ijumaa, Novemba 15, 2013.
Baada ya kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Aidha,
siku ya Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika Ibada ya mazishi katika
Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kuanzia saa
4:00 asubuhi. Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja vya
Karimjee kuanzia saa 6:30 mchana siku hiyohiyo ya Jumamosi, Novemba 16,
2013.
Aidha,
Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa siku ya Jumapili, Novemba
17, 2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa
ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu, Novemba 18,
2013.
Dkt.
Mvungi alifariki juzi (Jumanne, Novemba 12, 2013) katika Hospitali ya
Millpark jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili
ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea Kitengo cha Mifupa Muhimbili
(MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Kibamba, wilaya
ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi vibaya kichwani
usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.
Wakati
huohuo, Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na
Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba leo (Jumatano, Novemba 13, 2013)
wameungana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete kufika nyumbani kwa marehemu Dkt. Mvungi eneo la
Kibamba jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa pole kwa familia, ndugu
na jamaa wa marehemu Dkt. Mvungi.
No comments: