Mbunge wa Kigoma Kaskazini -Chadema Zitto Kabwe Atua Mkoani Kigoma Kwa Kishindo,Apokewa na Maadamano Makubwa.. Soma Hotuba Yake
Sehemu ya Vijana wakiandaman kwa furaha muda mfupi baada ya kumpokea
mbunge wa kigoma kaskazini-Chadema Zitto Kabwe muda mfupi baada ya
kuwasili kigoma leo
Baaadhi
ya Madreva bodaboda mkoani kigoma wakiongoza msafara wa mbunge wa
kigoma kaskazini-Chadema Zitto Kabwe muda mfupu baada ya kuwasili
Sehemu ya Vijana wakiandaman kwa furaha muda mfupi baada ya kumpokea
mbunge wa kigoma kaskazini-Chadema Zitto Kabwe muda mfupi baada ya
kuwasili kigoma leo
Mbunge
wa kigoma kaskazini-Chadema Zitto Kabwe(wa tatu kulia)akilakiwa na
baadhi ya viongozi wa chadema mkoani Kigoma muda mfupu baada ya kuwasili
na kupokewa na maandamano makubwa
Mbunge
wa kigoma kaskazini-Chadema akisalimiana na mamiaaaaa ya wanakigoma
muda mfupi baada ya kuwasili na kupokelewa na maandamano makubwa mjini
kigoma leo
SOMA HOTUBA YA MBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI-CHADEMA MH ZITTO Z. KABWE - KIGOMA LEO– 21 DESEMBA 2013
Leo
nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto nimerudi
nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si salamu za kawaida bali nawasalimu
kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji. Nawasalimu si kama
mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote niendapo najivunia kujitambulisha
kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.
Tuna
mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee
katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa nchi yetu
mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza
kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa
miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995. Kabla
ya hapo mlitoa madiwani wengi mwaka 1994.
Wakati Watanzania wengine wakiwa
wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa,
watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza
maisha yao, wengine kazi zao na wengine hata ndoa zao katika kupata mbegu ya
mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika
kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu
haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.
Na
nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana,
kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si maneno tu ambayo
ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na maisha niliyoyaishi kwa mifano
nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule ya Msingi Kigoma na baadaye Shule ya
Sekondari Kigoma. Malezi yangu yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma.
Nimekuwa nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa
kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu. Viatu
hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa na Kampuni ya Bora
Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye tulikuwa tunakaa mtaa
mmoja wa Kisangani Mwanga. Mama Coretha hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa
ana uwezo mkubwa, la hasha! Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya
darasa la pili kwenda la tatu.
Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa
uungwana, upendo na hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania. Uwajibikaji
kwani alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona kuwa
kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote. Jamii hii ya
watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa bidii kwenye masomo
na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili katika maisha yangu na ni
somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia
kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya juu sana.
Nikiwa
nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka niwakumbushe kwa
nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia. Demokrasia ina maana
pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wananchi.
Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha mwananchi kupata huduma zake stahili
kama Elimu, Afya, Maji na miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi
wanakufa njaa kwa kukosa ajira na kukuza umasikini. Demokrasia inahusu
maendeleo. Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma kutoka mikoa
isiyo na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano
kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa ndege wa
Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa bandari ndogo
mpya na ujenzi wa kituo cha Usafirishaji Mwandiga. Asije mtu akasema yeye ndio
kafanya haya.
Haya ni matunda ya nyinyi watu wa Kigoma kupokea demokrasia na
bila woga kuchagua viongozi wenu bila kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo.
Haya ni matunda ya viongozi wenu kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa,
Bunge. Haya ni matunda ya uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo.
Juhudi hizi lazima ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya
mkoa wa Kigoma katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea
maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa makuu.
Lakini
tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi cha utumishi wangu
kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka kwenu,nimekuwa mstari wa mbele
kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa Wananchi. Nakumbuka wakati napambana
kuhusu sheria mbovu ya madini kuna watu hapa nyumbani walisema 'sasa huyu kawa
mbunge wa Taifa' lakini watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea
Watanzania wote na sio Kigoma tu. Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya
mabadiliko makubwa sana kwenye sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi
ya mambo ambayo yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali
kuwa na hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya
asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani.
Uwajibikaji
ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri
kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana. Hii ilitokana sio tu na hoja ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia
simu na mitandao ya kijamii ambapo wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye
karatasi za kumtoa Waziri Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa
ambapo wabunge hawaoni taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu
wa fedha za Umma. Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na
kufukuzwa kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa
na ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika kuimarisha
demokrasia yetu.
Pamoja
na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.
Changamoto
kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.
Kutoaminiana. Ni dhahiri
kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi kikubwa. Taarifa za
kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania kumi, wanane hawaaminiani. Ni
changamoto kubwa sana. Wananchi wameacha kutuamini wanasiasa na wanasiasa
wameacha kuaminiana wenyewe kwa wenyewe. Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli
na ukweli umekuwa ni uongo. Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi
ujue kudanganya na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli.
Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa zetu.
Itachukua muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi yetu kama
hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa ukweli
na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa unatengenezwa badala ya
kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza
shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na kamati maalum iliyoundwa na Bunge
kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba chini ya kiapo nilisema sina majina ya
watu wenye akaunti huko Uswisi. Huu ulikuwa ni uongo. Ni uongo kwa sababu
niliitika wito wa kamati hata nilipokuwa katika mafunzo ya mgambo huko Tanga na
nilikutana nao mara nne.
Ni uongo kwa sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum
maelezo na taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na
umiliki wa mali nje ya nchi kinyumecha sheria. Ni uongo kwa sababu mimi
kutotaja majina haya haina maana sina majina, bali ni kwamba ninaheshimu
utaratibu na nimeachia vyombo husika vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu
binafsi nikianza kuchukua majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati
hizi muhimu na hata kupelekea mchakato mzima kuvurugika.
Sitaingia mtego huu!
Lakini hatua hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa
mfano uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi
ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya KUTOAMINIANA.
Lakini
mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na mawazo
tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii ni uhaini. Lakini bila kuenzi
tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama imara wala Taifa imara. Demokrasia
imara ni zao la tofauti za mawazo na uhuru wa mawazo.
Kama hatuwezi kujenga
vyamavinavyorutubisha uhuru wa mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga Taifa
lenye watu wenye kuogopa na waliojaawoga.Wanachamawanapoogopa uongozi ni udikteta,
lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia. Bila demokrasia ya
uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta. Lazima vyama vya siasa, viongozwe
kwa namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.
Demokrasia bila kuaminiana,
demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli.
Juzi
nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa yanayoendelea
ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu. Wabunge wengine
walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na mazungumzo. Hii
ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule. Mmenifunza kutojenga chuki na watu
na badala yake kuchukua kila tukio kama changamoto ya maisha.
Siasa ni kupambanisha
mawazo tofauti na hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina misingi yake
ambayo sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa siasa ni kuwa inapaswa
kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya kurushiana maneno na
kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa. Siasa si kuwekeana chuki na
kuonyeshana ubabe.
Na
hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni
ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo!
Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu,
ni uongo! Kinachonisukuma kufanya
vyote hivi ni ninyi. Ninasukuwa kila
ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu;kila ninapoona akina mama
wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana ambao hawana uhakika
wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma
kukosa hata shilingi mia moja kununua chai asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma
bali mamilioni ya watanzania wakiishi katika hali hii.
Alafu nalinganisha na
taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na utoroshwaji wa pesa zetu. Hebu sasa
linganisheni na ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni
imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za kimarekani milioni 1315
(bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni
2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania.
Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za kitanzania
zipatazo trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo
inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi katika
miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani milioni 4526 (bilioni 4.5)
sawa na shilingi za kitanzania trilioni 7,286,860,000,000 (trilioni 7.3).
Nimewatajia hapa namba chungu nzima na
matrilioni na mabilioni hayaleti maana. Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha
pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa - robo yake tuingeweza kujenga
barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka Kigoma mpaka Dar-es-salaam! Pesa
hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi
wengine ili kuhakikisha tunapata huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa
vijana wetu. Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya maelfu
ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi.
Pesa hizi zingeweza
kuwanunulia watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya viatu. Sasa
nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia macho utoroshwaji
wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia ya sisi wabunge kujilipia
posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi
au msaliti!
Lakini
naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za kisiasa jambo la
msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea bila sababu. Licha ya
kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika mambo haya lakini pia kuna
wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana mawazo yao, ndani na nje ya chama
chetu;ndani na nje ya Serikali na ndani nanje ya nchi yetu. Ndio maana lazima
kuibadili nchi yetu ili kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa
mawazo na fikra zake zinakuwa huru.
Maisha
ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa sababu bila
mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna maendeleo. Mabadiliko ni kiu
kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko huleta matumaini. Na kiu hii ni
kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi hiki kipya. Siasa za kizazi kipya cha
viongozi ni siasa za majawabu ya kero za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa
za kujenga na kuimarisha; ni siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale
mnapopingana kimawazo. Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za
mabadiliko; siasa zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na
kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania.
Mungu ibariki Tanzania.
No comments: