Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amesema baadhi ya mawaziri wamekuwa wakaidi kufuata ushauri wa kisheria ambao amekuwa akiutoa
Wakati Jaji Werema akiwananga mawaziri, kwa upande mwingine amemsifia Rais Jakaya Kikwete akisema kuwa yeye si kama mawaziri wake kwani ni msikivu na anayeshaurika. Akizungumza na mwandishi wetu jana, Jaji Werema alisema endapo ushauri ambao amekuwa akiutoa mara kadhaa kwa mawaziri ungezingatiwa, kilichotokea bungeni mwishoni mwa wiki cha mawaziri kung’oka kisingekuwapo.
“Tunatakiwa kuiga msemo wa Mkuu wa Jeshi la
Polisi, Said Mwema kuwa ‘tii sheria bila shuruti’, Rais tunamshauri na
anashaurika kwa nini mawaziri wakatae kuzingatia ushauri?” alisema
Werema na kuongeza:
“Mawaziri hawatakiwi kujifanyia tu mambo yao.
Tunawaandikia barua lakini zinakwenda na yanafanyika yaleyale... Hata
mimi nikionekana kukiuka sheria na kanuni naweza kuwajibishwa kwa kuwa
hakuna aliye juu ya sheria.”
Jaji Werema alisema watu wanaweza kutofautiana
kisiasa lakini katika mambo yanayohusu haki za binadamu lazima
kuunganisha nguvu pamoja ili kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa bila
kupindishwa.
Alikuwa akizungumzia kuhusu kung’oka kwa mawaziri
wanne kutokana na matokeo ya uchunguzi wa Operesheni Tokomeza Ujangili
ambao ulifanywa na Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira.
Ripoti ya Kamati hiyo ilisababisha Rais Kikwete
kutengua uteuzi wa Mawaziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha, Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo na Maliasili na Utalii, Balozi
Khamis Kagasheki.
Tume ya Kimahakama
Kadhalika, Jaji Werema alisema Tume ya Kimahakama
itakayochunguza kwa kina madhara yaliyojitokeza katika Operesheni
Tokomeza Ujangili iliyosababisha vifo, majeraha, utesaji wa kinyama,
uharibifu wa mali na upotevu wa mifugo, itaundwa na Rais Kikwete.
“Tume hii itakwenda mbali zaidi ya taarifa ya
kamati, itachunguza waliohusika, waliosemwa katika ripoti kwa juujuu
watatafutwa, kuangalia matumizi ya nguvu kiasi hicho na mwisho
mapendekezo ya tume hiyo juu ya kipi kifanyike kwa wahusika
itazingatiwa,” alisema na kuongeza:
“Hawa Mawakili wa Serikali waliokuwa katika
operesheni hiyo, DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) atatakiwa kutoa maelezo,
hao mawakili wake walikwenda huko kwa misingi gani pamoja na mahakimu
waliokuwa huko.”
Hata hivyo, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo alisema
hakuna haja ya kuundwa kwa tume hiyo na kinachotakiwa ni kutumika kwa
sheria ya kutafiti sababu za vifo.
KWA HABARI ZAID BOFYA HAPA
KWA HABARI ZAID BOFYA HAPA
No comments: