Ads Top

BINTI HUYU KAPATA AJALI YA KUGONGWA NA GARI AOMBA MSAAADA


Dada aitwaye Mariamu Omari, 22, amelazwa katika Taasisi ya Mifupa (Moi) Muhimbili Wodi ya Mwaisela namba 2 baada ya kuumia kichwani kutokana na kugongwa na gari katika Barabara ya Kawawa eneo la Morocco, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, Mariamu alisema kuwa yeye ni mkazi wa Kijiji cha Uzogole, Kata ya Ibadakule, Shinyanga na alipata ajali hiyo wakati akihangaika kutafuta maisha jijini Dar es Salaam.
Akisimulia mkasa huo Mariamu alisema; “Ninachojua ni kwamba hakuna ndugu anayejua niko wapi kwani niliondoka bila kuaga, baada ya kuwasili hapa jijini nilipata kazi ya ndani kwa mama aitwaye Salome anayeishi Mbezi.
“Nilifanya kazi kwa miezi sita baadaye walitokea watu ambao nilizoeana nao wakanishawishi niondoke kwa mama huyo na kwenda kufanya kazi kwa mtu mwingine kwa malipo mazuri. Nikakubali.
“Nilitoroka kwa mama Salome lakini kule nilikopelekwa sikujua ninafanya kazi gani bali niliwakuta akina dada wengi, hali ambayo ilinichanganya.
“Baada ya kuona hali kama hiyo niliona aibu kurudi kwa mama Salome ambaye niliishi naye kwa upendo.
“Naomba kama kuna ndugu yangu yeyote aje anione katika wodi ya Mwaisela namba mbili na ninawaomba Watanzania wanichangie ili nikiruhusiwa nirudi nyumbani Shinyanga. Hadi sasa sijui kama wazazi wangu wako hai maana niliondoka huko miaka miwili iliyopita,” alisema Mariam huku akitokwa machozi.
Kwa upande wake Kaimu Ofisa Habari Moi, Mary Ochieng aliiomba jamii imsaidie Mariam kwa sababu yupo hospitalini hapo kwa miezi miwili sasa na hajawahi kutembelewa na mtu yeyote.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.