Serikali ya Tanzania imesema inatafakari ushiriki wake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na inaweza kujitoa ndani ya Jumuiya hiyo iwapo itaendelea kutengwa katika baadhi ya vikao
Aidha imesema Tanzania haitambui vikao vinavyofanywa na nchi tatu
zilizopo ndani ya Jumuiya hiyo ambazo zimekuwa zikizitenga Tanzania na
Burundi.
Waziri anayehusika na masuala ya
Afrika Mashariki wa Tanzania Samwel Sitta ameliambia Bunge la Tanzania
kuwa makubaliano ya vikao hivyo vinavyofanywa na nchi za Kenya, Rwanda
na Uganda yatatekelezwa na nchi hizo zinazofanya vikao hivyo kwa sababu
vinafanyika nje ya utaratibu wa mkataba wa jumuiya hiyo.
Katika mikutano iliyofanyika hivi karibuni Tanzania na Burundi hazikualikwa kwenye vikao hivyo.
Kwa mujibu wa Waziri Sitta mikutano ya wakuu wa
nchi za Rwanda, Kenya na Uganda ambayo ilianza kwa kuitenga Tanzania
ilifanyika Entebbe nchini Uganda mwezi Juni mwaka huu na kufuatiwa na
mkutano wa pili uliofanyika Agosti mwaka huu huko Mombasa nchini Kenya
ambapo nchi hizo tatu bila kuishirikisha Tanzania walizungumzia
uanzishaji wa himaya moja ya forodha.
Mambo mengine waliyozungumza wakuu hao ilikuwa
uanzishaji wa visa moja ya utalii kwa nchi zao na matumizi ya
vitambulisho vya uraia ambavyo vitatumika kama hati za kusafiria
miongoni mwa nchi hizo.
Aidha Waziri Sitta amesema ndani ya mikutano hiyo pia walizungumzia kuanzisha mchakato wa kuanzisha shirikisho la nchi hizo.
Tayari Tanzania imeanza mazungumzo na nchi za
Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuangalia ni kwa namna gani
zitaanzisha ushirikiano nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama
zinavyofanya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya.
No comments: