Kenya imekuwa nchi ya kwanza kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki kuipongeza Tanzania kwa hatua yake ya kutangaza bayana kwamba haiko tayari kutoka katika jumuiya hiyo kama ilivyodhaniwa
Wasiwasi kuwa Tanzania ingejitoa kutoka jumuia ya Afrika Mashariki
ulitokana na hali iliyojitokeza kwa baadhi ya nchi za jumuia hiyo
kuendesha mikutano yao bila kuishirikisha Tanzania na Burundi.
Baadhi ya wanasiasa na wananchi
nchini Tanzania walitaka nchi yao iachane na jumuia hiyo wakizishutumu
Kenya, Rwanda na Uganda kuitenga Tanzania hata katika mikutano ya
masuala yaliyohitaji maamuzi ya jumuia.
Kufuatia mfarakano huo, ulionekana kutishia uhai
wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, wiki
hii alilihutubia bunge la Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, katikati ya
nchi na kutangaza bayana kuwa Tanzania haitatoka katika jumuiya ya
Afrika Mashariki, kwani imefanya kazi kubwa kuifufua na kuiunda upya
baada ya kusambaratika mwaka 1977.
Kwa upande wake, Kenya moja ya nchi waanzilishi
wa Jumuia ya Afrika Mashariki na ambayo ilishutumiwa kushiriki kuibagua
Tanzania, imemtuma waziri wake wa mambo ya nje, Amina Mohammed kwenda
Tanzania na kuwa na mazungumzo na waziri mwenzie wa mambo ya nje Bernard
Membe kuhusu mfarakano huo na nia ya kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi
mbili hizo.
Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam, Jumapili, waziri Amina Mohammed, amesema Kenya inaunga mkono
hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, kuhusu uamuzi wake wa kutojitoa katika
Jumuia ya Afrika Mashariki, huku akisisitiza kuwa bila Tanzania hakuna
Afrika Mashariki na bila Afrika Mashariki hakuna Tanzania.
"Kama unavyojua Kenya na Tanzania tumekuwa
tukiijenga jumuiya ya Afrika Mashariki kwa muda mrefu sana, tuko na
mafanikio mengi sana, kuna mambo mengi tumeyafanya, kuna njia ndefu
imebakia kuna mambo mengi yasiyoweza kupimwa kati ya nchi hizi. Na tuna
tumaini kwamba tutaendelea kuijenga Afrika Mashriki kwa nguvu zote na
tutawasiliana na watu wetu kwa sababu tunataka watu wetu waishi vema na
wawe majirani wazuri na waendelee . Kwa Tunataka uchumi wetu uende
vizuri. Kwa hiyo tutaendelea kushirikiana, sisi ni wale wa kwanza
tuliokuwa pale kwa hiyo tunataka tufanye kile tunachoweza kuendeleza
Afrika Mashariki..... Lakini tumefurahia sana sana hotuba ya Rais
aliyotoa pale bungeni na tunawashukuru pia Watanzania kumuunga mkono."
Pia waziri Amina amesisitiza kuwa hakuna namna
ambavyo Tanzania na Kenya zitatenganishwa, kwa namna ambavyo zimejenga
maingiliano makubwa ya kijamii na kiuchumi, huku akiomba Tanzania
kusaidia kusukuma ombi la Kenya la kutaka kesi ianyomkabili Rais wake,
Uhuru Kenyatta iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi ili kumpa fursa ya
kutekeleza majukumu yake ya kitaifa.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa
Tanzania, Benard Membe amesema serikali yake imefurahi kuona Kenya
imekuwa nchi ya kwanza kuipongeza Tanzania kwa kuinusuru jumuia ya
Afrika Mashariki kama ilivyokuwa mwanzoni na kujenga jumuiya ya watu na
si ya viongozi, na kuahidi kushirikiana na Kenya katika masuala
mbalimbali likiwemo la kutaka kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta
katika mahakama ya ICC iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi.
Waziri Membe amesema waziri mwenzake Amina
kutoka Kenya amesema hotuba ya Rais Kikwete imewazindua kwani hawakujua
kuwa yale waliyokuwa wakiyafanya yalikuwa ni kukiuka taratibu za Jumuia
ya Afrika Mashariki na kuahidi kuwa Kenya itashirikiana kikamilifu na
nchi waanzilishi halisi wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Habari Na BBCSwahili.com
Habari Na BBCSwahili.com
No comments: