Mgogoro ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeingia katika sura mpya
baada ya viongozi wake wawili waandamizi, Naibu Katibu Mkuu,
Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo kuuandikia uongozi
wa chama hicho wakitaka uikane taarifa inayowachafua mitandaoni.
Zitto na Dk Mkumbo wanatuhumiwa kupokea fedha na
kushirikiana na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa na wale wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kuivuruga Chadema.
Taarifa hiyo yenye kichwa cha habari `Ripoti ya
siri juu ya Zitto Kabwe’, ambayo imesambaa katika mitandao mbalimbali ya
kijamii katika siku za karibuni inadaiwa kuwa iliandaliwa na Kitengo
cha Upelelezi cha Chadema baada ya uchunguzi wa mwenendo wa Zitto ndani
na nje ya nchi kuanzia mwaka 2008.
Sehemu ya taarifa hiyo ya mtandaoni inadai kuwa
Zitto alipelekewa kiasi cha Dola za Marekani 266,000 (Sh416 milioni)
huko Ujerumani na maofisa wa Usalama wa Tanzania, Desemba 16, 2009.
Ripoti hiyo inadai kuwa fedha hizo zilipitishwa
katika Benki ya Berliner ya Ujerumani kwenye akaunti ya raia wa nchi
hiyo, Andrea Cordes, ambaye anadaiwa kumpelelekea Zitto.
Taarifa zaidi zinadai kuwa fedha hizo ziligawiwa kwa wafuasi mbalimbali wa chama hicho na miongoni mwao ni Dk Mkumbo.
Zitto amlima barua Dk Slaa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana,
Zitto alisema amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod
Slaa kumwomba athibitishe ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ kama ni ya kweli
au chama hicho kiikanushe ili aweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
waandishi wa kile alichokiita ‘hekaya.’
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho
(chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008
hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema,” alisema Zitto kwenye taarifa
yake.
Zitto alisema taarifa hiyo ni ya kutunga na
iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imemfedhehesha, imemsikitisha na
kumkasirisha.
Alisema taarifa hiyo iliibuliwa katika kipindi
ambacho alikuwa ziarani barani Ulaya katika nchi za Uswisi na Uingereza
ambako alikuwa anafuatilia fedha zilizofichwa na Watanzania katika nchi
hizo.
“Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka
kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka
Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo
waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu,” alieleza
Zitto katika taarifa yake
“Idara ingetoa ufafanuzi zaidi. Mjadala huu usikuzwe bila sababu za msingi na kufunika masuala mengine muhimu ya kitaifa,” alisema Mnyika.
Dk Mkumbo alia na uenezi
Dk Mkumbo alieleza kusikitishwa na Idara ya Uenezi ya Chadema kwa kukaa kimya bila kutoa maelezo juu ya suala hilo.
“Hasa pale ambapo tumeambiwa waraka huu umetoka
makao makuu. Hii si kawaida kwa idara yetu hii nyeti iliyosheheni watu
mahiri. Mara zote huwa wepesi kabisa kwa vijana wetu katika idara hii
kutoa ufafanuzi, tena kwa mambo mepesi kabisa yanayokigusa chama, vipi
makamanda kwenye jambo hili imekuwaje?” aliandika Dk Mkumbo kwenye
ukurasa wake wa mtandao wa Facebook jana na kuthibitisha kwa simu.
Dk Kitila alisema pamoja na umaskini wake, hajawahi kuhongwa popote na wala hatarajii.
“Taarifa zinazosambazwa kuhusu mimi ni za uongo wa
kijinga na uzushi wa kitoto kwa malengo ya siasa nyepesi. Ni wazi
kwamba wanaosambaza habari chafu kunihusu hawanijui na ndiyo maana
wanaweza kudiriki kuzusha kwamba mimi Kitila Mkumbo naweza kuhongwa
Sh200,000.”
Alihoji pia Chadema ilikuwa na siri gani za hatari
kiasi cha kumfanya Zitto, ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi kuhongwa
kiasi hicho kikubwa cha fedha.
Mnyika awajibu
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa Chadema, John Mnyika ameikana ripoti hiyo na kueleza kuwa haijaandikwa na makao makuu ya Chadema.
Mnyika alisema Zitto ameibua kitu ambacho anafahamu kuwa kimeshughulikiwa na uongozi wa chama hicho.
“Zitto anajua kuwa Andrea Cordes aliniandikia
baruapepe na nakala kwake nikawajibu kuwa ripoti hiyo haijaandikwa na
makao makuu ya chama na tukipokea malalamiko rasmi tutachunguza kwa sasa
chama kinaichukulia ripoti hiyo kama ripoti nyingine zinazosambazwa
mitandaoni,” alifafanua Mnyika.
Akizungumzia malalamiko ya Dk Mkumbo, Mnyika alisema alikuwa anapaswa kufuata taratibu za chama kama alikuwa na malalamiko.
Alisema baada ya taarifa hiyo ya siri kusambaa
mtandaoni, Zitto alitoa kauli na kama Dk Mkumbo hakuridhika, alipaswa
kuonana na watu wa Idara ya Uenezi ya Chadema “Idara ingetoa ufafanuzi zaidi. Mjadala huu usikuzwe bila sababu za msingi na kufunika masuala mengine muhimu ya kitaifa,” alisema Mnyika.
No comments: