Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Kamati
Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokutana Ubungo
Plaza, Dar es Salaam kuanzia asubuhi ya siku ya Jumatano ya tarehe 20
Novemba, 2013 hadi alfajiri ya leo Ijumaa tarehe 22 Novemba, 2013
imetafakari na kujadili kwa kina taarifa mbali mbali juu ya hali ya
kisiasa ndani na nje ya Chama chetu ambayo kwa muda mrefu imegubikwa na
tuhuma kubwa na nzito dhidi ya Chama chetu na viongozi wake wakuu, yaani
Mwenyekiti wa Taifa, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (MB), na Katibu
Mkuu, Dk. Wilbrod Peter Slaa. Tuhuma hizi zilikuwa na malengo na athari
ya kuwapaka matope na kuwachafua viongozi wakuu wa Chama na Chama
chenyewe, kutengeneza mtandao wa siri ndani na nje ya Chama ambao
hatimaye ungefanikisha sio tu lengo la kufanya mapinduzi nje ya
utaratibu wa kikatiba wa Chama, bali pia ungekipasua Chama vipande
vipande na hivyo kuua matumaini ya Watanzania juu ya uwezekano wa
kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi na kijamii katika nchi yetu
kwa kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Uchunguzi
wa Kamati Kuu umebaini kuwepo kwa mkakati mkubwa wa kutimiza malengo
hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko
2013.’ Mkakati huu uliandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa
Ushindi’ ambacho vinara wake wakuu ni wanne, yaani Naibu Katibu Mkuu na
Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Zitto
Zuberi Kabwe ambaye kwenye waraka huo anajulikana pia kama ‘MM’ au
‘Mhusika Mkuu’; mjumbe wa Kamati Kuu na mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo ambaye kwenye waraka anajulikana pia
kama M1; Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha ambaye kwa sasa
amesimamishwa uongozi, Bwana Samson Mwigamba na ambaye kwenye waraka
anaitwa M3; na mtu mwingine ambaye hadi sasa jina lake halijajulikana
lakini kwenye waraka anajulikana kama M2 na anatajwa kuwa yuko ‘ukingoni
kupigwa nje’ katika mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea katika
Sekretariat ya Chama hapa Makao Makuu.
Kwa
mujibu wa waraka wenyewe, “Mkakati huu umeandaliwa kwa pamoja na M2 na
M3 na kupitiwa na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya
mwisho na kuanza utekelezaji.” Mbele ya Kamati Kuu, Dk. Mkumbo alikiri
kwamba MM au Mhusika Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe; M1 ni yeye
mwenyewe Dk. Mkumbo na M3 ni Bwana Mwigamba. Dk. Mkumbo alikataa kata
kata kumfahamu M2. Aidha, Dk. Mkumbo alikiri mbele ya Kamati Kuu kwamba
yote yaliyoandikwa katika ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ yametoka kwenye
‘Mtandao wa Ushindi’ na hayajabadilishwa.
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Mkakati
wa Mabadiliko 2013 ni mpango wa kuipasua pasua CHADEMA na kuiangamiza
kabisa kwenye uso wa siasa za Tanzania. Huu sio mkakati wa kufanya
mabadiliko ya kiuongozi ndani ya Chama kwa njia za kidemokrasia na za
kikatiba. Ni mpango wa kukiteka nyara Chama na kukiua. Ndio maana
watunzi wa waraka huu wamesema kwenye waraka wao: “Tunahitaji kutekeleza
mkakati huu kwa siri kubwa ili mkuu aliyepo aendelee kubweteka na ndio
maana hata lugha iliyotumika ndani hapa ni ya pekee.” Kamati Kuu
inaamini mkakati wenye malengo halali ya kufanya mabadiliko ndani ya
Chama kwa njia halali za kikatiba usingependekeza kwamba:
“Vikao vyetu
na yeye (MM aka Mhusika Mkuu aka Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe)
vitafanyika mara chache sana na mahali pa faragha kupita kiasi
ikiwezekana hata nchi jirani.” Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba kama
mkakati huu ungekuwa na malengo mazuri ya kukijenga Chama na sio
kukiteka nyara na kukiua, wanamtandao hawa wasingependekeza utaratibu
ufuatao wa utekelezaji wa mpango: “M1 (Dk. Mkumbo) ndiye atakayekuwa
anawasiliana na tunayemtaka ambaye ataitwa MM (Mhusika Mkuu).
Tumepanga
kwamba kusiwe na mawasiliano mengi kati ya kamati na mhusika mkuu
kuepuka tracking ya wapinzani wetu. M1 ni mtu wa karibu na MM kwa hiyo
mawasiliano yao hayataweza kutiliwa shaka na mtu yeyote hata
wangewasiliana mara nyingi kiasi gani. Hata hivyo, linapokuja suala la
mkakati huu tunasihi mawasiliano yawe kwa kuonana uso kwa uso ama kwa
simu na si sms. M1 ndiye atakayewasilisha mambo yote yanayotoka kwenye
kamati ya kitaifa na endapo kuna haja ya MM kukutana na kamati ya
kitaifa, mipango yote ya kikao itafanywa na M1 kwa usiri mkubwa.”
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Mkakati
wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichana chana Katiba ya
Chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya Chama chetu na utaratibu wetu
wa kikatiba. Wakati
ibara ya 10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama ambazo ni
sehemu ya Katiba ya Chama chetu ya mwaka 2006 inamkataza kiongozi wa
CHADEMA asijihusishe na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au
ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa
jamii kisiasa au kijamii”, wanaMtandao wa Ushindi wameonyesha wazi kuwa
wanaendekeza siasa za udini kwa kusema yafuatayo juu ya waliemwita ‘mtu
tunayemtaka’, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe: “Kwa kuwa ni
Mwislamu, hii ni fursa katika kupata kuungwa mkono na wanachama waislamu
ambao wamekuwa na kigugumizi wakidhani waislamu hawatakiwi katika
uongozi wa taasisi yetu.”
Wakati
ibara ya 10.1(viii) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka kila kiongozi wa
CHADEMA “... kuwa mkweli na muwazi wakati wote ... na aachane na vikundi
vya majungu na wadanganyifu (rumour mongers) ...”, wanaMtandao wa
Ushindi wameeleza kwenye waraka wao kwamba mipango yao ya utekelezaji wa
Mkakati wa Mabadiliko 2013 ‘itafanyika kwa usiri mkubwa.’ Wakati
ibara ya 10.1(ix) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama inamtaka
“kiongozi asijihusishe na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au kuzua
migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”, wanaMtandao wa
Ushindi wamesambaza tuhuma za uongo dhidi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa
(ambaye wanamwita kwenye waraka wao kuwa ni ‘Mpinzani wetu’) kuwa “...
hana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa ngazi za chini kutokana na
dharau nyingi anazozionyesha pale anapokutana na viongozi wa ngazi za
chini akiwa katika kuijenga taasisi hii.... Hii imemfanya kutopendwa na
viongozi wengi wa ngazi za chini hivi sasa na kutoa fursa ya pekee kwa
tunayemtaka.”
Wakati
ibara ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka “kiongozi asitoe
tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na
kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni”, tuhuma zote
zilizotolewa na wanaMtandao hawa dhidi ya viongozi wakuu wa Chama chetu
hazijawahi kutolewa na yeyote kati ya wanaMtandao hawa katika kikao
chochote halali cha Chama cha ngazi yoyote.
Wakati
ibara ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji inaeleza kwamba “itakuwa
marufuku kwa kiongozi wa CHADEMA kukashifu Chama, kiongozi au mwanachama
yeyote wa Chama ...”, Mkakati wa Mabadiliko 2013 umejaa kashfa kubwa,
matusi mengi na udhalilishaji mkubwa wa Chama, viongozi wake wakuu na
wanachama kwa ujumla. Hivyo, kwa mfano, Mwenyekiti wa Chama Taifa
ametuhumiwa na wanaMtandao hawa kuwa ni mtu mwenye ‘uzalendo unaotia
shaka’, mwenye ‘elimu ya magumashi’, ‘mzito kujieleza’, ‘mtu mwenye
akili ndogo’, n.k.
Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Hakuna
chama au taasisi yoyote duniani inayoweza kunyamazia mkakati wa aina
hii dhidi yake na viongozi wake wakuu na ikadumu au kubaki salama. Chama
au taasisi yoyote inayoendekeza vitendo vya aina hii miongoni mwa
viongozi wake wa ngazi yoyote au miongoni mwa wanachama wake wa kawaida
inakaribisha kifo na mauti. Chama chetu na viongozi wake wa juu wamekaa
kimya kwa muda mrefu sana; wamevumilia mashambulizi na kashfa nyingi
sana dhidi yao binafsi na dhidi ya Chama; wamestahimili matusi makubwa
sana dhidi yao. Chama chetu kimevumilia yote haya na viongozi wake
wamevumilia yote haya sio kwa sababu walitaka Chama chetu kiuwawe na
wanaMtandao hawa. Uvumilivu wote huu ulitokana na haja ya kuwapa
wanaMtandao wa Ushindi fursa ya kugundua hatari ya siasa zao na kuwapa
muda wa kujirekebisha na kujirudi.
Kama
ilivyo kwa binadamu au taasisi yoyote ile, uvumilivu wa Chama chetu na
viongozi wake wakuu una kikomo. Na hiki ndio kikomo cha uvumilivu wa
Chama chetu, viongozi wake na wanachama wake kama wanavyowakilishwa na
Kamati Kuu ya Chama chetu. Hivyo basi, katika kikao chake tajwa, Kamati
Kuu ya Chama chetu, kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba ya dharura
chini ya ibara ya 6.5.2(d) ya Katiba ya Chama, imeazimia yafuatayo
kuhusu Mkakati wa Mabadiliko 2013 na hao wanaojiita wanaMtandao wa
Ushindi:
Kwamba,
kuanzia sasa, viongozi wote waliohusika ama kuhusishwa na mkakati huu,
yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla
Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba wavuliwe nyadhifa
zao zote za uongozi ndani ya Chama; Kwamba
timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa Sekretariat ya Makao Makuu ya
Chama na wajumbe wa Kamati Kuu ifanye uchunguzi wa haraka ili kumtambua
mtu anayeitwa M2 na ambaye anadaiwa kuwa mtumishi wa Makao Makuu ya
Chama ili hatua stahiki na za haraka zichukuliwe dhidi yake, pamoja na
watu wengine wote watakaobainika kuhusika na mpango huu wa uhaini dhidi
ya Chama chetu; Kwamba
Kamati ya Chama ya Wabunge inaelekezwa kuchukua hatua za haraka za
kuhakikisha Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe anavuliwa madaraka yake yote
kama Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, with immediate
effect;
Kwamba
viongozi waliotajwa katika aya ya (a) waandikiwe hati zenye tuhuma
dhidi yao haraka iwezekanavyo na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe
kwenye Chama kwa vitendo vyao na wapatiwe fursa kamili ya kujitetea
kama inavyotakiwa na ibara ya 6.5.2(a), (b) na (c) ya Katiba ya Chama; Kwamba
mara baada ya utekelezaji wa azimio (d), Kamati Kuu ikutane kwa dharura
kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatma ya watuhumiwa na hatua
nyingine zitakazofuata; Kwamba
waraka wa wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi uwekwe hadharani na
usambazwe kwa vyombo vya habari vya aina zote ili wananchi wa Tanzania,
wanachama na viongozi wa Chama chetu na dunia nzima kwa ujumla iweze
kupima uzito wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 na uhalali wa maamuzi haya ya
Kamati Kuu.
Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Naibu
Katibu Mkuu Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla Mkumbo
waliiomba Kamati Kuu iwaruhusu kujiuzulu nyadhifa zao baada ya Mkakati
wao wa kukiteka nyara Chama na kukiangamiza kujulikana mbele ya Kamati
Kuu. Kwa kuzingatia uzito wa makosa waliyokifanyia Chama, viongozi wake
wakuu na wanachama wake kwa ujumla; na kwa kuzingatia uzito na umuhimu
wa nyadhifa kubwa walizo nazo ndani ya Chama; na kwa kuzingatia uelewa
wao wa Katiba, Kanuni na taratibu za Chama na uzoefu wao katika safu za
juu za uongozi wa Chama, Kamati Kuu ilikataa kwa kauli moja kuridhia
maombi hayo ya kujiuzulu. Kufanya hivyo ingekuwa ni sawa na kuwaruhusu
wajiondoe kwenye uongozi wa Chama wakiwa na heshima wasizostahili hata
kidogo.
Chama
chetu ni tumaini pekee la Watanzania wote wanaotaka mabadiliko ya kweli
na ya kimsingi katika mfumo wa kiutawala, kiuchumi na kijamii wa nchi
yetu. Hii ndiyo sababu kubwa na ya pekee iliyosababisha vita kubwa na
chafu inayopigwa dhidi ya Chama chetu na viongozi wetu wakuu. Lengo kuu
ni kuwachafua viongozi wakuu, kuleta mgogoro na mgawanyiko ndani ya
wanachama, viongozi wake na hivyo kukichafua Chama mbele ya macho ya
Watanzania. Chama chetu kikishachafuka kwa mtindo huu, matumaini ya
Watanzania wanaotaka mabadiliko yatakufa. Vita hii kubwa haijaanza jana,
na haitaisha kesho. Kama ambavyo tumekabiliana nayo na kuishinda siku
za nyuma, vivyo hivyo tutakabiliana nayo mara hii na kuishinda. Kama
Chama chetu kilivyoibuka na nguvu na heshima kubwa zaidi katika
mapambano ya siku za nyuma, vivyo hivyo Chama chetu kitaibuka na nguvu
na heshima kubwa zaidi katika awamu hii ya mapambano.
Tunawaomba
Watanzania, wanachama na viongozi wetu wasife moyo, bali waendelee
kukiunga mkono chama chao cha ukombozi. Tunawaomba Watanzania, wanachama
na viongozi wetu waendelee kulilinda tumaini lao pekee la mabadiliko ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Badala ya kukatishwa
tama, kila mmoja wetu aongeze bidii maradufu ili kuwashinda wale
wanaotaka kuleta majanga katika Chama chetu na kwa Taifa letu.
------------------------------------------
FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) - MWENYEKITI, TAIFA
------------------------------------------
WILBROD PETER SLAA - KATIBU MKUU
No comments: