TAARIFA RASMI YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHADEMA ALIYOITOA LEO KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI SERENA HOTEL JIJINI DAR ES SALAAM
Mbunge wa Kigoma Kaskazini-Chadema Zitto Kabwe
Taarifa ya Zitto Kabwe Kuhusu Kuvuliwa Nafasi za Uongozi Ndani ya Chama Changu Cha CHADEMA
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema, Zitto Kabwe amesema kuwa hana mpango wa kujiondoa Chadema na
kusisitiza kwamba atakuwa mtu wa mwisho kujitoa ndani ya chama hicho kwa
hiari yake.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana katika mkutano aliouandaa kwa pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati
Kuu, Dk Kitila Mkumbo, Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alisema kwamba
amekuwa mwanachama wa Chadema tangu akiwa na umri wa miaka 16 hivyo
haiyumkiniki akikimbia chama hicho.
Zitto na Dk Kitila walivuliwa nyadhifa zao wiki iliyopita wakihutumiwa kukihujumu chama hicho.
“Kuna watu ambao walitegemea kuwa leo hii
ningejibu mapigo, ‘ningezodoa,’ watu wengine kwa majina kama ilivyo
kawaida kwa siasa za Tanzania. Natambua pia kama ilivyo kawaida wakati
wa migogoro kwa vyama hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo
ningetangaza kinachoitwa ‘maamuzi magumu’,” alisema na kuongeza:
“Natambua kuwa wapo ambao wangependa kutumia
nafasi zao kudhoofisha mapambano ya siasa za demokrasia nchini mwetu,
napenda wanachama wa Chadema na wapenda demokrasia wote nchini watambue
kuwa, mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa
mwisho kutoka kwa hiari yangu.”
“Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano
ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya
wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda
siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.”
Alisema kuwa atafuata taratibu zote za ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hilo.
“Mimi sitoki, wanaotaka nitoke, wanitoe wao,” alisema Zitto.
Zitto alisema Chadema ndicho chama kilichomlea na
kumfikisha hapo alipo sasa, hivyo hata siku moja hatokuwa chanzo cha
kuvunjika kwa chama hicho.
“Ningependa hata mtoto wangu akikua, awe pia
mwanachama wa chama hiki, nimejiunga na chama hiki nikiwa na umri wa
miaka 16 mpaka sasa nina miaka 37, nimetumia muda mrefu zaidi Chadema
kuliko kipindi chote cha maisha yangu, Chadema ni kama maisha yangu,
kukivunja chama hiki ni sawa na kujivunja mimi mwenyewe, kitu ambacho
siwezi,” alisema Zitto.
Nyuma ya pazia
Zitto alisema sababu za kumvua uongozi zilizotolewa na chama ni waraka unaojulikana kama ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’.
“Waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa
nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu .
Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati
Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia
zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama,” alisema na kuongeza:
“Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa.”
Tuhuma ya kwanza aliyoitaja Zitto ni ile ya
kudaiwa kutokushiriki kumpigia kampeni mgombea urais wa chama hicho
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Alisema tuhuma hiyo aliitolea ufafanuzi kuwa
pamoja na kuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, alifanya
kampeni kwenye majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwamo Dar
es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa.
“Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni
katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais na kote nilipopita
niliwapigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na urais,”
alisema.
Tuhuma ya pili ni kwamba akiwa mkoani Kigoma
alishindwa kuwapigia kampeni wagombea wengine wa Chadema na ndiyo maana
ni yeye pekee aliyeshinda. Alisema siyo kweli, bali aliwapigia kampeni
wagombea wote lakini kilichotokea ndiyo uliokuwa uamuzi wa wananchi wa
Kigoma.
Zitto alisema tuhuma ya tatu iliyotolewa ni
kushiriki kuwashawishi wagombea wa chama hicho katika baadhi ya majimbo
kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM
wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa.
“Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa
tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama
kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila
uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho,” alisema.
Tuhuma nyingine ni kutokushiriki operesheni
mbalimbali za chama. Alisema siyo kweli na ameshiriki karibu katika
operesheni zote na hivi karibuni alikuwa kwenye operesheni za kujenga
chama kwenye Mikoa ya Tabora na Katavi.
Tuhuma nyingine aliyosema ilichukua muda mrefu
zaidi kujadiliwa na Kamati Kuu ni ile ya kutaka vyama vya siasa
vikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema baadhi ya wajumbe walitaka akitaarifu kwanza chama chake juu ya hatua hiyo kabla ya kuiweka hadharani
“Niliwaambia kuwa, utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi
yangu ya uenyekiti wa PAC (Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali) kulinda
chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia
zilezile ambazo tunazipinga na tunapigania kuzibadilisha,” alisema.
Tuhuma ya mwisho ambayo aliitaja ni ile ya kukataa posho za vikao
Alisema alikataa hizo posho tangu mwaka 2011 na
ataendelea na msimamo huo kwani ni jambo ambalo lipo kwenye ilani ya
chama hicho na kuwataka wabunge wengine wamuunge mkono.
Kuhusu waraka
Alisema licha ya kutokujua juu ya waraka huo,
laiti kama angeufahamu kabla, angetekeleza mara moja yale yaliyo ndani
ya waraka huo.
Alisema pia kuwa kwa sasa hajafanya uamuzi kama
atagombea uenyekiti ndani ya chama hicho lakini wakati utakapofika na
kama atashauriwa kufanya hivyo, atafuata taratibu za chama hicho.
No comments: