Ads Top

Hali ya afya ya Waziri wa Fedha, Dk Mgimwa hospitalini Milpark nchini Afrika Kusini imeelezwa kuwa mbaya

Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa

HALI ya Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa (63), imeelezwa kuwa mbaya katika Hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini alikolazwa tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, Raia Mwema linafahamu.
Vyanzo kutoka ndani ya serikali vimeliambia gazeti hili kwamba juzi-Jumatatu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, alisafiri kwenda nchini humo kwa ajili ya kufuatilia hali ya waziri wake.
“Kwa kweli mheshimiwa ana hali mbaya. Hivi ninavyozungumza nawe madaktari wanapambana kuhakikisha anarejea katika 
hali yake ya kawaida,” kilisema chanzo chetu hicho cha habari kutoka Wizara ya Fedha.
Akizungumza na gazeti hili, Msemaji Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, alisema taarifa aliyoipata kutoka Afrika Kusini inaeleza waziri anaendelea vizuri na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi wowote.
“Nimezungumza na watu walio naye huko Afrika Kusini na kusema taarifa ni nzuri. Wanazungumza naye na wanasema anaendelea vizuri tu. Hakuna sababu ya kuhofia lolote,” alisema Mduma.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mufindi Kaskazini (CCM), Mahmoud Mgimwa, ambaye kifamilia pia ni mdogo wa Waziri Mgimwa, alisema hawezi kuzungumzia lolote kuhusu ugonjwa wa nduguye huyo kwa vile suala hilo sasa linashughulikiwa kiserikali.
“Kimsingi mimi nafahamu nini kinaendelea lakini kuna watu wa serikali ambao wanamwangalia na wako huko huko hospitali. Ni vizuri kuzungumza na watu walio ‘site’ (kwenye eneo la tukio) kuliko mimi ambaye niko Tanzania.
“Hali ya mgonjwa ina fluctuate (inabadilika-badilika) na hivyo taarifa nitakayokupa sasa inaweza isiwe ya sasa hivi. Hivyo nakushauri uzungumze na watu walio hospitali hivi sasa,” alisema Mgimwa.
Gazeti hili lilifanikiwa kupata mawasiliano na Dk. Likwelile moja kwa moja kutoka hospitalini hapo ambaye alisema amefurahishwa na hali aliyoiona ya mgonjwa.
“Niko hapa hospitali. Waziri anaendelea vizuri sana. Tunaongea naye vizuri, anakula vizuri na madaktari wana matumaini makubwa juu ya afya yake. Anahitaji kupumzika ili kujiimarisha zaidi,”
“Tumwombee, wakati mwafaka tutajulishana. Tuelewe pia kuwa Waziri amefanya kazi nyingi bila kupumzika kwa muda mrefu,” aliandika Likwelile kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms).
Hata hivyo, si Likwelile wala familia ya Dk. Mgimwa ambao walikuwa tayari kueleza ni ugonjwa gani ambao unamsumbua msomi huyo wa masuala ya uchumi ambaye alianza kuwa waziri miaka miwili iliyopita.
Dk. Mgimwa alikuwa mkufunzi katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza, kabla ya kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mkoa wa Iringa, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Hospitali hiyo ya Milpark ndiyo imekuwa ikitumiwa na Serikali ya Tanzania kupeleka watu wanaoumwa na mtu wa karibuni zaidi kuhudumiwa katika hospitali hiyo ni marehemu Dk. Sengondo Mvungi.
Watanzania wengine mashuhuri ambao wamewahi kupelekwa kutibiwa katika hospitali hiyo katika siku za karibuni ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda na Mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Jeshi la Polisi (DCI), Robert Manumba.
Hospitali hiyo ndiyo ambayo alitibiwa pia Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, wakati alipopata matatizo ya upumuaji, Februari mwaka huu.
Hospitali hiyo ni ya binafsi na ipo katika eneo la Parktown West lililopo jijini Johannesburg na inamilikiwa na Kampuni ya Netcare. Ina vitanda 342, huku 90 kati ya hivyo vikitumika katika wodi za wagonjwa mahututi.

No comments:

UHURUTZ. Theme images by hanoded. Powered by Blogger.