Huzuni na simanzi viliyateka maeneo ya Mthatha na Qunu katika Jimbo la Eastern Cape, Afrika Kusini baada ya kuwasili kwa mwili wa rais wa kwanza mzalendo wa nchi, Nelson Mandela
Jeneza lililobeba mwili wa aliyekuwa Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika
Kusini, Nelson Mandela lilipofikishwa Uwanja wa Ndege wa Mthatha jana.
Maziko yanafanyika leo kijijini kwao, Qunu kwa taratibu za kimila
Mwili wa Mandela uliwasili jana katika Uwanja wa Ndege wa Mthatha saa 7:40 mchana (kwa saa za huku) dakika 20 kabla ya muda uliotarajiwa, ukiwa umesafirishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Waterkloof, Pretoria.
Mwili wa Mandela uliwasili jana katika Uwanja wa Ndege wa Mthatha saa 7:40 mchana (kwa saa za huku) dakika 20 kabla ya muda uliotarajiwa, ukiwa umesafirishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Waterkloof, Pretoria.
Ulisindikizwa na maofisa waandamizi wa Jeshi la
Afrika Kusini (SANDF), maofisa kutoka Serikali, wawakilishi wa familia
yake na viongozi wa mila kutoka kabila la abaThembu.
Mandela anazikwa leo katika makaburi ya familia
yaliyopo katika Kijiji cha Qunu ambako alikulia, katika mazishi ambayo
yatakuwa mchanganyiko wa mila na desturi, dini yake ya Kikristo ikifuata
taratibu za kimethodisti na kijeshi kwa maana ya Serikali,
Alizaliwa katika Kijiji cha Mvezo, Julai 18, 1918
na alifariki dunia Desemba 5, mwaka huu nyumbani kwake, Houghton,
Johannesburg akiwa na umri wa miaka 95 baada ya kuugua magonjwa ya figo
kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Maziko yake yanamaanisha kuhitimishwa kwa siku 10
za maombolezo ya kitaifa, ambayo yalishuhudia mamia ya viongozi kutoka
pande zote za dunia, waliofika Afrika Kusini kushiriki Ibada ya Kitaifa
iliyofanyika katika Uwanja wa FNB, Soweto Jumanne iliyopita.
Kadhalika mwili wa kiongozi huyo kwa siku tatu
mfululizo; Jumatano hadi Ijumaa wiki hii ulikuwa ukiwekwa katika Ikulu
ya Pretoria iliyopo Majengo ya Umoja (Union Buildings) ambako
waombolezaji zaidi ya 100,000 walipata nafasi ya kutoa heshima zao za
mwisho.
Serikali ya Afrika Kusini imetaganza kuwa leo ni
siku ya mapumziko huku wamiliki wa maduka makubwa nao wakitangaza kwamba
hawatafungua biashara zao kama hatua ya kuienzi siku ya mwisho ya
Mandela.
Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Malawi, Joyce
Banda ni wakuu wa nchi pekee ambao watahudhuria mazishi ya Mandela na
wote wamepangiwa kutoa salaamu za rambirambi wakati wa mazishi.
Watawaongoza viongozi wengine kadhaa wakiwamo wale wanaowakilisha
mashirika ya kimataifa.
Simanzi uwanjani
Uwanja wa Ndege wa Mthatha ulikuwa kimya hasa
baada ya ndugu wa karibu wa Mandela, wakiongoza na mjane Graca Machel
kuwasili saa 6:44 mchana na kulakiwa na viogozi mbalimbali wakiongozwa
na Waziri wa Ulinzi, Nosiviwe Mapisa Nqakula.
Mara baada ya jeneza kushushwa kutoka kwenye ndege
ya jeshi Namba C-130, wimbo wa taifa ulipigwa, pia kupokea heshima
kutoka kwa askari wa SANDF ambao walikuwa uwanjani hapo mapema
Kabla ya safari ya Mthatha, mtalaka wa Mandela, Winnie
Medekileza alikuwa akimsaidia Graca kwa kumshika na wakitembea pamoja
taratibu, ambaye alikuwa katika majonzi makubwa.
Safari ya kwenda Qunu ilianza saa 8:15 kwa msafara
uliokuwa na magari yapatayo 100. Vijana wa ANC walikuwa wamejipanga
pembezoni mwa barabara wakiwa wametengeneza uzio wa kuwazuia watu
wasiingie barabarani wakati msafara huo ukiwa unapita.
Inakadiriwa kuwa vijana hao ni zaidi ya 6,500 na
walijipanga umbali wa kilometa 35 kutoka Uwanja wa Ndege, Mthatha hadi
Qunu nyumbani kwa Mandela ambako mwili wake ulikabidhiwa kwa viongozi wa
kimila.
Kama ilivyokuwa Pretoria, wananchi waliokuwa
wamejipanga pembezoni mwa barabara walikuwa wakipunga mikono na wengine
walisikika wakiangua vilio na kuomboleza.
Mapema jana asubuhi katika Uwanja wa Waterkloof,
mwili wa Mandela uliagwa na viongozi waandamizi wa Chama Tawala cha
Afrika Kusini, African National Congress (ANC) na ilipotimu saa 3:00
walikabidhi mwili huo kwa uongozi wa SANDF.
Kabla ya kupandishwa kwenye ndege, wimbo wa Taifa
ulipigwa na gwaride la heshima lililokuwa limeandaliwa. Mamia ya wakazi
wa Pretoria wakionekana wenye simanzi, walipunga mikono wakati ndege
hiyo ikiondoka, na wengine walitokwa na machozi.
Ulinzi mkali
Uwanja wa Qunu ambao umekabidhiwa kwa SANDF hivi
sasa, umetengwa kwa ajili ya wageni mashuhuri wakiwamo wakuu wa nchi na
wawakilishi wa mashirika ya kimataifa hivyo hakuna ndege za kiraia
zinazoruhusiwa kuutumia.
Waziri wa Usafirishaji, Dipuo Peters alisisitiza
kwamba ndege nyingine zitumie viwanja vya East London na Port Elizabeth
ili kuondoa uwezekano wa kusababisha msongamano.
Mkuu wa Jimbo la Eastern Cape, Noxolo Kiviet
alisema watu mashuhuri watakaotua Mthatha watachukuliwa katika mabasi
maalumu, hivyo hakutakuwa na usafiri binafsi hata kwa wakuu wa nchi.
Ulinzi umeimarishwa katika eneo lote la Eastern
Cape ambako askari polisi na wale wa SANDF walikuwa wakiendesha doria
katika maeneo mbalimbali. Helikopta za jeshi na polisi pia zilikuwa
zikizunguka eneo lote la Mthatha tangu juzi.
Msemaji wa Polisi, Kanali Mzukisi Fatyela alisema
polisi na wanajeshi wamejiandaa kuhakikisha kuwa mambo yote yanakwenda
sawa kwa maana ya usalama na mchakato wa mazishi
Kanali Fatyela alisema baadhi ya barabara zimefungwa kwa sababu
za kiusalama na kwamba askari watatoa maelekezo jinsi ya kutumia zile
zilizopo kwa lengo la kuepusha msongamano.
Taratibu za kimila
Katika kutekeleza mila na desturi, jana asubuhi
ng’ombe dume (fahali) alichinjwa na WaXosa wanaamini kwamba roho yake
inasindikiza roho ya Mandela katika Ulimwengu wa mizimu. Ng’ombe huyo
alichinjwa kabla ya mwili kuwasili.
Bila kuwekwa viungo vyovyote, nyama ya ng’ombe
huyo ilichemshwa katika chungu cheusi cha chuma, kwenye moto ambao
uliwashwa nje, hadharani.
Juzi mmoja wa viongozi wa kimila, Chifu Mfundo
Mtirara alisema: “Baada ya mwili kuwasili, viongozi wetu wa mila
watafanya matambiko na mwili huo utalala hapa ndani mpaka asubuhi”.
Mapema leo asubuhi, ng’ombe mwingine alitarajiwa
kuchinjwa kabla ya taratibu za maziko kuanza kama sehemu ya taratibu za
kimila za kusema buriani kwa Mandela.
Baada ya taratibu hizo, mwili unatarajajiwa
kukabidhiwa kwa viongozi wa Kanisa na baada ya ibada ya kidini na baada
ya taratibu hizo, utakabidhiwa kwa Rais Jacob Zuma kwa ajili ya mazishi
ya kitaifa.
Mazishi hayo yatahitimishwa na taratibu nyingine
za kimila zitakazoongozwa na Mfalme wa abaThembu, Buyelekhaya Dalindyebo
anayetoka katika Ukoo wa Mandela.
Mfalme huyo ataongoza taratibu za kuukabidhi mwili wa Mandela katika Ulimwengu wa mizimu.
Wasaidizi wake wataungana naye katika tukio hilo
na baada ya hapo, watatawanyika na kurejesa nyumbani ambako watanawa
mikono kisha kupata chakula cha mchana.
Baada ya wiki moja, familia hiyo itakuwa na
tambiko jingine la kusafisha beleshi (koleo) na vifaa vingine ambavyo
vilitumika katika kuchimba kaburi atakamozikwa Mandela.
Baada ya mwaka mmoja, Desemba 15, 2014 ng’ombe
dume mwingine anachinjwa kwa ajili ya hafla ya kuwavua wanafamilia
mavazi ya maombolezo.
No comments: