POLISI GEITA WATUHUMIWA KWA UTESAJI RAIA
Na Antony Sollo Geita
JESHI la Polisi Mkoani Geita limeingia katika
kashfa ya utesaji wa Raia kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake ambapo malengo
ya kuanzishwa kwa jeshi la polisi nchini siyo kunyanyasa Raia bali ni kulinda
raia na mali zake.
Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoani Geita Fabian Mahenge ambaye ni
mmoja wa Viongozi 51 wa Chama hicho aliyekaa mahabusu katika Gereza la
Biharamulo kwa zaidi ya siku 45 kutokana na kilichoelezwa kuwa ni mapenzi ya
viongozi wa Jeshi la Polisi.
Katika mkutano wake na Waandishi wa Habari Mkuu
wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro alisema kuwa Jeshi la Polisi halipo
kwa ajili ya kumuonea mtu kwa itikadi yake ya kidini wala kisiasa na aliwataka
Askari wa Jeshi hilo kufanya kazi zao kwa weledi na kukamata mtu na kufanya
uchunguzi na pale watakapobaini kuwa hana kosa wamuachilie mara moja.
Hali hii Mkoani Geita imekuwa tofauti na agizo
la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP kwani kumeripotiwa ukiukwaji mkubwa wa
maadili ya jeshi la polisi huku kukiwa na madai dhidi ya Mkuu wa Kituo cha
Polisi Mganza ambaye alivamia kikao cha ndani cha Viogozi wa CHADEMA Mkoani
Geita kilichokuwa kinafanyika katika ukumbi wa Manzagata huko Mganza.
Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa
CHADEMA Mkoani Geita Fabian Mahenge alisema kuwa julai 7 mwaka huu kulikuwa na
ratiba ya vikao viwili ambavyo vilipangwa kufanyika katika ukumbi wa Manzagata
ulioko Mganza Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
Kwa mujibu wa Mahenge kikao cha kwanza kilikuwa
ni mkutano mkuu wa chama Kata ya Mganza ambapo mahenge aliwataja wajumbe wa
kikao hicho kuwa ni Viongozi wa Matawi ambao walialikwa rasmi kwa ajili ya
utambulisho wa Mwenyekiti wa Mkoaambapo baada ya utambulisho angeachana nao na
kuendelea na kikao cha Viongozi wa Mkoa ambao idadi yake ni wanane.
Wakati maandalizi ya kuanza kwa vikao hivyo
Mahenge alisema kuwa kulikuwa na dalili zote kuwa kungefanyika vurugu ili
kuhakikisha vikao hivyo vinavurugwa na Jeshi la Polisi kwani Katibu Mwenezi wa
Kata ya Mganza Marco Maduka ambaye aliwahi kushika nadfasi ya udiwani katika
Kata ya Mganzaaliitwa kituo cha Polisi na Mkuu wa Kituo cha polisi Mganza wito
ambao hata hivyo haukufahamika mara moja.
Kufuatia hali ya wasiwasi iliyoonekana kutokana
na wito wenye utata uliotolewa na Mkuu huyo wa Kituo cha polisi Mganza kiongozi
huo ilibidi asindikizwe na Viongozi wawili ambao ni Katibu wa CHADEMA Wilaya ya
Chato Mange Sayi Ludomya pamoja na Katibu wa Chadema Mkoa Soud Ntanyagala.
Kwa mujibu wa Mahenge baada ya kufika kituoni
hapo viongozi hao hawakurudi na juhudi za kuwafuatilia zilipofanyika walielezwa
kuwa Viongozi hao walipelekwa Chato kwa amri ya OCD na baada ya kufika
waliwekwa mahabusu bila kuambiwa makosa yao.
Wakati hayo yakifanyika Mwenyekiti wa CHADEMA
Mkoa Fabian Mahenge alikuwa amebaki na
viongozi wa Kata ya Mganza ambao ni viongozi wa Mkutano Mkuu wa
Kata pamoja na viongozi wa Mkoa yaani
Mwenyekiti wa Balaza la Wazee Mkoa Vitus Makoye,Mwenyekiti,BAVICHA Neema Chozaile
pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Geita
Masaga Misso.
Baada ya kuitikia wito wa OCS Kituo cha Mganza
viongozi waliokwenda huko hawakurudi na ilipotimu majira ya saa 10 jioni
viongozi waliobaki na Mwenyekiti huyo walivamiwa na Askari wa Jeshi la Polisi
likiwataka kutawanyika huku OCS akiwa amevalia nguo za kiraia na akiwa amelewa
chakali alitoa bastola na kuingia ukumbini na kuwatishia viongozi hao.
Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa alimhoji OCS huyo akitaka kujua yeye ni nani maana alikuwa
amevaa kiraia jambo lililowapa shida katika kutambua kuwa yeye ni nani kufuatia
kutishiwa na silaha maana si jambo rahisi kwa kiongozi mkubwa kama OCS kukiuka
maadili ya matumizi ya silaha kama ilivyokuwa kwa OCS huyo ambapo hata hivyo
aliwaambia kwa kejeli kuwa kama hawamjui leo ndiyo wangemjua yeye ni nani.
“Mimi mnataka nijitambulishe kwenu! Hivi
hamnijui? Sasa ngoja nadhani baada ya muda mfupi mtanitambua mimi ni
nani”alisema OCS.
Baada ya
majibizano hayo OCS alitoka nje ya ukumbi na baada muda mfupi alirudi akiwa na
askari wanne na kuanza kupiga mabomu ya machozi ndani ya ukumbi huo uliokuwa na
wajumbe wasiopungua 80.
Wakati Askari hao walioongozwa na Mkuu wa Kituo
cha Polisi Mganza wakitekeleza hayo,kulikuwa na kundi lingine la askari
walioitwa kutoka Chato walifika ukumbini hapo na kuanza kuwashambulia viongozi
hao kwa kuwapiga wakitumia silaha mbalimbali ambapo mmoja wa viongozi hao Patrick
Kalikawe alichomwa singe ya bunduki huku Masimango akipigwa na kitako cha
bunduki mguuni na mtu mwingine ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja
akivunjwa mkono.
Katika vurugu hizo viongozi 51 walikamatwa na
kupelekwa mahabusu kituo cha polisi Chato na baada ya kufikishwa waliwekwa
rumande bila kuambiwa makosa yao, Mahenge aliongeza
kuwa zoezi la kuwachukua maelezo lilipoanza waliambiwa kuwa kosa
waliloshitakiwa nalo viongozi hao ni kufanya kusanyiko lisilo na kibali ndani
ya ukumbi wa Manzagata.
Imeelezwa kuwa Viongozi hao walikaa Mahabusu
kituo cha polisi Chato kwa saa 72 kabla ya kupandishwa kizimbani na kusomewa
mashitaka ya kufanya kusanyiko lisilo na kibali ndani ya ukumbi wa Manzagata
ambapo hata hivyo viongozio hao walikana shitaka hilo.
Baada ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Chato
kutoa taarifa juu ya dhamana dhidi ya watuhumiwa hao kuwa wazi,Mwendesha
Mashitaka wa Jeshi la Polisi aliweka pingamizi la dhamana kwa washitakiwa hao
akidai kuwa iwapo wangeadhaminiwa wangeweza kuhatarisha Amani na kusababisha
uvunjifu wa Amani katika maeneo ya Chato ambapo baada ya kuwekewa pingamizi
hilo viongozi hao walisafirishwa hadi gereza la Biharamulo ambako walikaa muda
wa siku 45.
Yaliyojiri katika
Gereza la Biharamulo.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa uongozi wa gereza
hilo uliwapokea vizuri kwa maana ya kwamba hawakufanyiwa vitendo vya
ukandamizaji kama walivyofanyiwa na jeshi la polisi.
“Tulipokelewa vizuri kama watu ambao tulikuwa
tunaingia kuanza maisha mapya,zaidi ya yote Mkuu wa gereza alitenda haki kwa
kuwa tayari kutusikiliza pale tulipotaka kuhoji au kupata ufafanuzi wa jambo
lolote na kutufariji kwa maneno mazuri akisema kama tuliingia ipo siku tena
tutatoka”alisema Mahenge.
Mahenge anazibainisha changamoto walizopambana
nazo Mawakili waliokuwa wakiwatetea viongozi hao ambapo walikuwa na kibarua
kigumu kutokana na kuwepo kwa hoja
mbili zilizokuwa walizokuwa wamewekewa ili
kuhakikisha viongozi hao wanaendelea kusota rumande.
Hoja ya kwanza ilikuwa ni kupambana na
mwendesha mashitaka ili kuondoa pingamizi la dhamana na hoja ya pili kusimamia
kesi ya msingi yaani kufanya kusanyiko lisilo na kibali.
Mahenge anabainisha kuwa,baada ya Mawakili
kushinda hoja ya kwanza kuhusu pingamizi la dhamana ikazaliwa agenda nyingine
kwamba ili mtu aweze kupata dhamana,ni lazime apate wadhamini wawili yakiwemo
masharti yaliyojaa mkanganyiko uliowafanya wadhamini kukosa sifa ya kuwadhamini
viongozi hao.
Mahenge aliendelea kubainisha mbinu na
unyanyasaji uliokuwa ukifanywa kuhakikisha yeye na viongozi wenzake wanaendelea
kukaa mahabusu pamoja na kukosekana kwa usafiri wa kuwatoa washitakiwa kutoka
Biharamulo kuwaleta Mahakama ya Wilaya ya Chato zoezi ambalo lilichukua wiki
tatu.
Kufuatia hali hii Jeshi la Polisi kupitia kauli
iliyotolewa na IGP kwamba Jeshi la Polisi halitamuonea mtu Viongozi wa Jeshi la
Polisi Mkoani Geita wanaonyesha wazi kupingana na Mkuu wao huyo ,lakini pia
hata upande wa Rais Magufuli ambaye aliingia madarakani akisisitiza kuondoa
mlundikano wa wafungwa na M,ahabusu katika Magereza.
Changamoto ndani ya
Gereza la Biharamulo.
Kuhusu
changamoto zilizomo ndani ya gereza Mahenge alisema kuwa kuna changamoto nyingi
ndani ya gereza hilo lakini kubwa kuliko zote ni maji,ugonjwa wa kuambukiza
kama upele.
Mahabusu wa kubambikizwa kesi na Askari wa Jeshi la Polisi.
Mahenge
anasema kuna kundi kubwa la vijana kutoka chato ambao walikamatwa na
kubambikizwa kesi za uzembe na uzurulaji jambo ambalo si la kweli maana wengi
wa vijana hao walikamatwa wakiwa katika nyumba za kulala wageni,wengine wakiwa
vibarua kwa watu kwa ajili ya kujipatia kipato lakini hadi leo hii wako
mahabusu wakitumikia vifungo na kibaya zaidi ni vijana wenye umri mdogo yaani
chini ya miaka 18.
Mahenge
anaenda mbali zaidi kwa kuifananisha chato na nchi nyingine maana mambo
yanayofanywa na Askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Chato hayafanani na sehemu
yoyote katika nchi hii.
Mahenge
ameziomba Taasisi zinazotetea Haki za Binadamu zielekeze nguvu zote chato ili
kujionea mambo ya ukatili yanayofanyika huko,ikizingatiwa kuwa hata Mkuu wa nchi
hii(Rais Dkt John Pombe Magufuli ) ndiko anakotokea na ilitakiwa Wilaya ya Chato
na Geita kwa ujumla iwe mfano kwa maeneo mengine nchini hususani katika masuala
mazima ya utawala bora na unaozingatia Sheria na Haki.
MWISHO.
No comments: