BUNDI ATUA HALMASHAURI YA WILAYA YA USHETU
Na Antony Sollo Ushetu.
MGOGORO mkubwa umeibuka
baina ya Emmanuel Makashi ambaye ni Diwani wa Kata na Christopher Rwagasanga
Lyogelo ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Sabasabini iliyopo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoni Shinyanga,hali iliyopelekea diwani huyo
kuangua kilio katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo
akimtuhumu Afisa mtendaji huyo kuhujumu shughuli za maendeleo ya Kata yake.
Akiwasilisha malalamiko
yake mbele ya baraza la Madiwani kilichofanyika Februali 14 mwaka huu huko
Ushetu Makashi lisema kuwa Afisa Mtendaji huyo amekuwa akibeza kila kitu
kinachofanywa na Diwani huyo.
“Mheshimiwa mwenyekiti
Afisa Mtendaji huyu amekuwa akinichonganisha na wananchi huku akisema kwamba
mimi sijasoma,na kuwaambia kuwa yeye ndiye anafaa kuwa kiongozi wao akidai kuwa
anashahada ya elimu ya juu huku akiwaambia kwamba mimi sina uwezo wa kuwaletea
maendeleo,amekuwa akiwashawishi watendaji wa vijiji kutojishughulisha katika
masuala mbalimbali ikiwemo uchangiaji wa shughuli za maendeleo”alisema Makashi.
Kutokana na uchungu
aliokuwa nao Makashi aliangua kilio mbele ya viongozi mbalimbali waliohudhuria
kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichoketi kwa lengo la
kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwamo miradi ya maendeleo kwa wananchi
wa Ushetu.
Baraza hilo
lilihudhuriwa na viongozi mbambli mbali wa Chama na serikali akiwemo mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa pamoja na katibu Tawala wa Wilaya ya
Kahama, Timoth Ndanya ambapo Diwani huyo aliamua kumshtaki Mtendaji huyo kwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga huku akisema.
“Ndugu mwenyekiti kuna
tatizo la kiutendaji katika Kata yangu ya Sabasabini kwamba, Afisa Mtendaji wa
Kata amekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa wananchi wangu, tangu aanze kazi
kwenye Kata yangu mwaka 2016 hakuna maendeleo yoyote kwani amekuwa akiwagomesha
wananchi kuchangia shughuli za maendeleo,” alilalamika Makashi.
Katika jitihada za
kutatua mgogoro huo Makashi alimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo
Matomola Michael kufika katika Kata hiyo kwa lengo la kuwapatanisha waendelee
kuwatumikia wananchi huku akisema tangu kuanza kwa figisu figisu za Afisa
Mtendaji huyo hadi sasa hakuna kitu kinachofanyika kutokana na mgogoro huo.
“Mheshimiwa mwenyekiti
kibaya zaidi Afisa Mtendaji huyo amekuwa akiwashawishi na watendaji wengine wa
vijiji wasinipe ushirikiano katika kutekeleza shughuli za maendeleo kwa
wananchi kwa madai kwamba yeye ndiye kiongozi sahihi kutokana na kwamba ana
nashahada ya elimu ya juu,kwa kweli nakuomba Mkurugenzi uunde tume ya uchunguzi
dhidi yake,kama hutafanya hivyo tubadilishane ofisi wewe uwe diwani na mimi
nikae kwenye kiti chako cha ukurugenzi ili uone vitendo ninavyofanyiwa na
Mtendaji huyo,” alisema Makashi kwa uchungu.
Makashi alisema
kuwa,kabla ya ujio wa Afisa Mtendaji huyo katika Kata ya sabasabini, kulikuwa
na mahusiano mazuri na wananchi kutokana na ushirikiano mzuri kati yake
na kaimu afisa mtendaji aliyekuwapo kipindi cha 2013 /2015 ambapo walifanikisha
kutimiza agizo la Rais Magufuli juu ya kutengeneza Madawati mashuleni kwa
kuchonga madawati 74 yaliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 8.8
Makashi alisema kuwa
katika kipindi hicho alijitolea katika ujenzi wa matundu ya choo cha shule kwa
kuchangia fedha kiasi cha shilingi 150,000 na kuongeza kuwa kiasi cha shilingi
milioni 5.3 kilitumika kujenga nyumba ya mganga katika Zahanati ya Kata
huku nguvu ya wananchi ni shilingi milioni 1.2.
Makashi alibainisha
kuwa katika kipindi cha mwaka 2017 alifanikisha ujenzi wa barabara ya
Sabasabini kwenda Iponyang’holo kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa
kilometa 9 kwa gharama ya shilingi milioni 2.5 kwa ushirikiano na diwani wake
wa viti maalum Felista Nyerere ambaye alichanga shilingi 300,000 kati ya fedha
hizo,na sasa Afisa mtendaji huyo ameathiri shughuli za maendeleo katika Kata
hiyo kutokana na mgogoro walio nao.
“Mtendaji huyo alianza
kazi katika kata hii tangu mwaka 2016, na alinikuta nikiwa vizuri na wananchi
wangu lakini tangu aanze kazi nimeshindwa kumuelewa labda anaitaka hii
nafasi ya Udiwani wa Kata! , maana anachofanya Mtendaji huyu ni uvunjaji wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ninaona anapingana Mheshimiwa Rais baada ya
kuamua kuamua kukwamisha shughuli za maendeleo kwa makusudi kinyume na agizo la
Rais la kuwatumikia wananchi!,mimi naomba Mkurugenzi aunde Tume ili kuweza
kutatua mgogoro huu vinginevyo Kata hii haitaweza kupata maendeleo”alisema
Makashi.
Akichangia hoja hiyo
Diwani wa Kata ya Bulungwa Joseph Masaluta alilieleza baraza hilo kuwa wote
wawili Diwani pamoja na Afisa mtendaji huyo wa Kata wapelekwe kwenye kamati ya
maadili kwa lengo la kuhojiwa kwa kina ili kubaini chanzo cha mgogoro wao na kuongeza
kuwa wawili hao wamekutana wote ni jeuri.
Katika majibu yake kwa
diwani huyo Makamu mwenyekiti wa baraza hilo Gagi Lala ambaye ndiye alikuwa
akiongoza baraza hilo alisema,
“Mkurugenzi haiwezekani
mtu alalamike kiasi hiki tena hadharani inaonekana kuna tatizo linalopaswa
kushughulikiwa, pamoja na kwamba kanuni za baraza haziruhusu kuingiza taarifa
zilizo nje ya shughuli za baraza , mheshimiwa diwani ujumbe umefika kuwa
mtulivu tutalishughulikia suala hili,” alisema Lala.
Tanzania Daima lilimtafuta
Afisa Mtendaji wa Kata ya Sabasabini Christopher Rwagasanga Lyogelo kupitia
simu zake mbili za mkononi 0687 937 103 na 0765 192 263 ili kuzungumzia tuhuma
hizo lakini simu zilizimwa hivyo juhudi za kumpata ali kutolea ufafanuzi wa
tuhuma hizo zinaendelea, hata hivyo Afisa kilimo Kata hiyo Rwegasira Thobias
ambaye pia amekuwa akikaimu nafasi hiyo mara kwa mara ambaye alikiri kuwepo kwa
mgogoro wa viongozi hao na kusema, “Ni kweli viongozi hao wamekuwa na mvutano
lakini kama unavyojua siasa na utaalamu haviendani sasa sijui watamalizaje
maana kila mmoja anavutia upande wake” alisema Rwegasira
Kwa upande wake kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Benjamin Onesmo ambaye
pia ni afisa maendeleo ya jamii katika Halmashauri hiyo alisema kuwa kutokana
na hali hiyo ofisi yake imelichukua suala hilo na italitafutia ufumbuzi wa
haraka.
“Mheshimiwa Mwenyekiti
ofisi yangu inalibeba suala hilo na litashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi wa
Haraka,” alisema Onesmo”.
No comments: