WANAUME WAASWA KUTOJIMILIKISHA MAENEO YA FAMILIA
Na Antony Sollo
WANAUME
katika halmashauri ya mji wa Kahama Mkoani Shinyanga wametakiwa
kuachana na dhana ya kujimilikisha hati miliki za viwanja vyao, ili
kutoa kipaumbele kwa akinamama ili nao waweze kumiliki
ardhi hali ambayo itaepusha migogoro katika familia.
Akizungumza
kabla ya kutambulisha mradi wa upimaji wa viwanja 4,000 katika kata ya
Mhongolo afisa ardhi wa halmashauri ya mji wa Kahama
Mashiri Magasa alisema kuwa wanaume wilayani Kahama wamekuwa na
tabia ya kujimilikisha maeneo yote yenye hati miliki jambo ambalo siyo
haki na kwamba hali kama hiyo pindi mwanaume anapofariki dunia humwacha
mwanamke katika wakati mgumu.
Magasa
aliyasema hayo februari 8 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa
vitongoji vya sofi, bomani na Nyamhela vilivyoko katika Mtaa wa Mhongolo ambapo
aliwaasa wanaume kuachana na dhana ya kujimilikisha maeneo ya familia kwani
hali hiyo ndiyo chanzo cha mifarakano katika familia pindi baba wa familia
anapoamua kuchukua hati hizo na kuomba mkopo katika taasisi za fedha na
kushindwa kurejesha.
“Ifike wakati wanaume muwape
fursa ya kumiliki ardhi wanawake kwani kufanya hivyo kunatoa usawa katika
familia lakini pia kuna wakati mmoja wa familia hiyo akifariki hasa baba
mwanamke hawezi kuhangaika kutokana kuwa tayari anakuwa ana mali halisi
inayomfanya aendeleze familia, wanaume wakiachana na mfumo dume mwanamke
akashirikishwa ipasavyo katika umiliki huo hakutakuwepo na migogoro baina
yao,” Alisema Magasa.
Katika
hatua nyingine Afisa ardhi aliwataka wakazi wa mji wa Kahama kuhakikisha
wanapima viwanja vyao kabla ya kufanya ujenzi au shughuli zozote za kimaendeleo
na upimaji huo uende sambamba na utafutaji wa hati miliki ili kupunguza
migogoro isiyokuwa na tija kwa jamii na kuwafanya waweze kukopesheka kirahisi
katika taasisi za fedha.
“Kwa
mujibu wa sheria ya Ardhi na mpango miji hakuna mwananchi yoyote hapa nchini
anayeruhusiwa kufanya ujenzi wowote wa nyumba za makazi katika kiwanja chake
bila ya kupimwa au kujenga nyumba bila ya kufuata ramani za mpango miji
tukikuta unajenga kwenye eneo bila kibali tunasitisha ujenzi na kukupiga faini”
alisema Magasa.
Kwa
mujibu wa mpima ardhi kutoka kampuni ya Total Geo
survey Co.Ltd
Emmanuel William ambaye anayeshughulikia upimaji wa
viwanja katika kata hiyo alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuchangia gharama
za upimaji ili kazi iweze kuendelea na kwamba mpaka sasa viwanja
4,000 vimepimwa na viwanja 1000 vimepitishwa na wizara
ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuwatafutia
hati miliki wananchi.
Akizungumzia zoezi hilo William
alisema kuwa lengo ni kupima viwanja 12,000 katika Kata hiyo na kuwataka
wananchi kuongeza kasi ya kuchangia gharama ya upimaji ambayo ni shilingi elfu
tisini 90,000 na kwamba gharama hiyo ni ndogo ukilinganisha na bei elekezi ya
serikali ya kuanzia ambayo inaanzia shilingi laki tatu, 3,000,000. Kwa kila
kiwanja.
Kwa
upande wake Afisa Mtendaji wa mtaa wa Mhongolo Denis Diocles
alisema kuwa lengo la kampuni hiyo ni kupima viwanja elfu 12, lakini viwanja
vilivyofikiwa ni 4021, vilivyopewa namba ni 1335, ambavyo havijapewa namba ni
2686 na kutaja mradi wote unagharimu kiasi cha shilingi milioni 361 kati ya
hivyo vilivyolipiwa ni 1192 na ambavyo havijalipiwa ni 2828.
Akizungumza
katika zoezi la kutamburisha mradi huo Mwenyekiti wa mtaa wa Mhongolo Emmanuel
Nangale alisema kuwa kukusanya shilingi milioni 361 kwa wakazi hao siyo
kazi ndogo na kudai kuwa kiasi kilichokusanywa hadi sasa kinapswa kupongezwa
licha ya watu kutohamasika kikamilifu na kwamba katika halmashauri hiyo ni Mtaa
wa Mhongolo pekee umejitutumua katika zoezi hilo.
Mwisho.
No comments: