BARUA YA WAZI KWA RAIS JOHN POMBE MAGUFULI.
Ndugu Mhariri ,
Kwa heshima na taadhima sisi wananchi wakaaji
wa Kitongoji cha Mnyamasi Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi tunaomba kuwasilisha malalamiko yetu kwa
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
kufuatia unyama na manyanyaso tuliyofanyiwa na wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na
Usalama Wilaya na Mkoa waKatavi.
Mheshimiwa Rais kwa masikitiko makubwa
tunakumbuka kauli ulizowahi kuzitoa mara
kwa mara hata wakati wa mikutano ya kampeni zako ukiomba nafasi hii uliyo nayo
ambapo ulijipambanua kuwa Serikali yako itakuwa ni ya kutetea wanyonge.
Ni kweli tumeshuhudia ukishughulikia masuala
mbalimbali ikiwemo kutatua migogoro kati ya raia na watendaji wa
Serikali,viongozi wa Kisiasa papo kwa papo,tumekuwa tukipata faraja kubwa
kutokana na mafanikio wanayopata wahanga wa aina yetu ambao wameweza kutumia
njia mbalimbali kuwasilisha malalamiko kwako na kuyapatia suluhu na kwa umakini
mkubwa.
Mheshimiwa Rais sisi wananchi wakaazi wa
Kitongoji cha Mnyamasi Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi,tumefanyiwa ukatili
wa kutisha na viongozi uliowaamini na kuwapa nafasi ya kukuwakilisha katika
Mkoa wetu wa Katavi lakini tumesikitishwa na usiri mkubwa uliodumu takribani
miezi minne sasa bila mafanikio.
Mheshimiwa Rais,tumekuwa na mgogoro mkubwa na
wa muda mrefu kati yetu na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda Mji
ambao wameamua kutunyang’anya maeneo yetu kwa kutumia vyombo vya dola huku
wakisababisha majeruhi na mauaji kwa baadhi ya wananchi.
Mheshimiwa
Rais ukatili tuliofanyiwa na watendaji waSerikali Mkoani Katavi umetufanya
tushindwe kuelewa iwapo na sisi ni raia wa nchi hii tena tuliopiga kura zetu
kuchagua viongozi wa kututetea katika masuala ya maendeleo katika nyanja mbalimbali
ikwemo Elimu,Afya pamoja na ulinzi na usalama.
Tunatambua
kuwa,katika vipindi mbalimbali,Serikali imekuwa na mipango mizuri hasa katika
masuala ya mbalimbali ikiwemo Sera ya Taifa kuhusu Uchumi,kilimo,ufugaji na
Tanzania ya Viwanda na Biashara huku kukiwa na ushirikishwaji wa wananchi
katika maeneo yao.
Kilichotuumiza
ni watendaji wa Serikali Mkoa wa Katavi kuamua kuendesha zoezi la kutuondoa kwa
nguvu katika maeneo yetu tuliyoishi kwa muda mrefu wakitumia vyombo vya dola
tena bila hata kuandaa mpango shirikishi zoezi lililopelekea mauaji na majeruhi
kwa vijana wetu ambao hawataweza kufanya kazi tena kutokana na kushambuliwa kwa
risasi za moto na Askari wa Jeshi la Polisi bila huruma.
Mheshimiwa Rais tumeshangazwa na matumizi ya
nguvu yaliyofanywa na jeshi la Polisi kwa maelekezo ya wateule wako ambapo
mpaka sasa hali ya maisha ya wananchi tuliotendewa ni mbaya kwani hatuna mahali
pa kuishi kwa miezi minne sasa huku tukilala nje na watoto wetu wadogo na
hakuna hata msaada wowote tuliopewa.
Mheshimiwa
Rais ,tunapenda kukutaarifu kwambahuku kwetu umefanyika Ukiukwaji mkubwa wa
Sheria na Haki za Binadamu pamoja na matumizi mabaya ya madaraka toka kwa
viongozi wa Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya na Mkoa wa Katavi ikiwemo
Mkurugenzi wa Halmashauri ambao kwa pamoja waliendesha zoezi la kutuondoa kwa
nguvu katika maeneo yetu huku kamati wakitumia Askari wenye silaha za moto
yakiwemo mabomu ya machozi zoezi lililosababisha mauaji na ulemavu wa kudumu
kwa raia ambapo baada ya kufanya mauaji Jeshi la Polisi lililazimisha kufanyika
kwa mazishi ya raia aliyeuawa kwa kupigwa risasi bila kufanyika uchunguzi jambo
ambalo ni kinyume na Sheria.
Mheshimiwa
Rais ni wazi kwamba Viongozi wa Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya ya
Tanganyika Mkoa wa Katavi walitumia vibaya madaraka yao ambapo walifanya
vitendo vya kikatili kwa kupiga raia,kuchoma moto nyumba,kuchoma vyakula kujihusisha na uporaji wa mali mbalimbali
zikiwemo fedha taslimu katika vibanda na maduka ya wafanyabiashara,kupora simu,kuchoma
moto mali za wananchi zikiwemo mashine za kusaga nafaka,kupora
mifugo,baiskeli,pikiki na kutuzuia kufanya kazi za kilimo,uharibifu
unaokadiriwa kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.
Mheshimiwa
Rais tangu Oktoba 7 na 8 mwaka 2017 mpaka sasa wananchi tunaishi maisha magumu huku
tukilala nje na hatuna huduma mbalimbali za kijamii kutokana na Kamati hizi
kufanya uharibifu na sasa tumelazimishwa kulipia maeneo mapya kwa gharama ya
shilingi laki moja (100,000) kwa nguvu bila kutushirikisha.
Kabla ya kufanyiwa ukatili huu hapo Septemba 9
mwaka 2017 tuliandika barua ya kuomba kuonana na Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi ili kupata msaada na mwongozo kuhusu Sheria ya Ardhi
inavyoelekeza ambapo barua yetu ilipokelewa na Katibu wa Waziri septemba 12 mwaka
2017,tulielezea jinsi tulivyofanyiwa ukatili na Kamati za Ulinzi na Usalama
iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Saleh Mhando.
Mheshimiwa
Rais sisi wananchi kwa pamoja tunapinga kitendo cha kuondolewa katika maeneo
yetu kwa madai ya kupisha uwekezaji bila kushirikishwa na kwamba kwa mujibu wa
Sheria ya Ardhi namba 4 na 5 ya 1999,Ardhi ni mali ya Serikali lakini
imefafanuliwa vizuri pale Ardhi inapotaka kutwaliwa na Serikali kwa ajili ya
matumizi maalumu ya kijamii kwamba Kanuni na taratibu na Sheria lazima zifuatwe
ikiwemo kufanyika majadiliano pamoja na kufanyika tathmini ili Serikali au
mwekezaji aweze kulipa fidia kwa wananchi waliokuwa wakimiliki maeneo hayo.
Kufuatia
hali hii tunapinga pia kitendo kuhamishiwa Luhafwe pamoja na kulazimishwa kulipa shilingi 100,000 kwa heka moja ambayo hata
hivyo haitoshi kukidhi mahitaji ya kilimo,na kwamba hatujaridhishwa na Kitendo
cha Viongozi wa Serikali uliowateua kukuwakilisha kutufanyia ukatili kwa
kutumia nguvu ya dola bila kufanya majadiliano na maridhiano katika jambo hili.
Zipo
taarifa kuwa kwamba viongozi wa Serikali
wanawaleta wafugaji kutoka katika vijiji vingine ambao wameshatoa fedha kiasi
cha shilingi mil 100 kwa viongozi wa Serikali ili tuondolewe katika maeneo yetu
jambo ambalo linatupa picha kwa nini kuwe na matumizi makubwa ya nguvu ya dola
kiasi hiki.
Tumelalamika kwa muda mrefu katika Ofisi mbalimbali ambapo Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Magharibi pekee ndiyo iliyoonyesha kutupa ushirikiano mkubwa baada ya kuandika barua yenye kumb Na LD/WZ/0023/25 kwenda kwa Katibu Tawala Mkoa wa Katavi akitaka kupatiwa taarifa juu ya ushirikishwaji wa wananchi wa maeneo hayo wakati uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya Ardhi ya vijiji huku akitaka kujua kama kulikuwa na ukweli wa madai ya baadhi ya maeneo kutengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo huku sisi wakulima na wafugaji wa kijiji hicho tukinyimwa fursa ya kuyatumia.
Kitendo cha Kamishna wa Ardhi kilitutia moyo na
faraja kubwa sana kufuatilia suala hili na hasa pale Mh Naibu Waziri wa Ardhi
alipoomba taarifa juu ya ushirikishwaji wa wananchi wa maeneo hayo wakati wa
uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya Ardhi ya vijiji,ambapo pamoja na barua
hiyo viongozi wa Wilaya na Mkoa walionyesha dharau kwa kuendelea kufanya
vitendo vya ukiukwaji wa Sheria na Haki za Binadamu kwa kukaidi maelekezo toka
Ofisi ya Naibu Waziri jambo lililotufanya tujiulize kwamba hivi katika nchi
yetu kuna Serikali ngapi.
Baada ya kufika katika Ofisi ya TAMISEMI Mkoani
Dodoma 18 Desemba 2017 tulifanya mazungumzo na Wakurugenzi wa Idara wakati
tukifuatilia majibu yetu baada ya kuhitaji taarifa za upande wa pili yaani toka
kwa Viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Katavi,tukiri wazi kwamba tulipata maelekezo
mazuri pamoja na ushauri ambapo tukiwa hapo Ofisini tulipokea taarifa kwamba
kulikuwa na watu walienda kufanya kazi siku za jumamosi na jumapili huku
wakifanya uharifu pamoja na uporaji wa mali za wananchi pamoja na vipigo.
Baada
ya majadiliano na viongozi wa TAMISEMI tulishauriwa tuwasilishe malalamiko yetu
tukipitia marejeo mbalimbali ya barua za malalamiko pamoja na matukio ya
ukiukwaji wa Sheria na Haki za Binadamu ili yaweze kufanyiwa kazi na kuona
hatua za kuchukua dhidi ya walengwa
(Viongozi wa Serikali Katavi).
Mheshimiwa Rais,Kwa kuwa Ofisi za Mkuu wa
Wilaya na Mkuu wa Mkoa ndizo zenye jukumu la kutoa Taarifa mbalimbali kuhusu
Maafa,sisi wananachi hatuamini kama taarifa zitakazowasilishwa TAMISEMI
zitakuwa na uhalisia wa Malalamiko
yetu,na kwamba viongozi walioombwa kutoa taarifa hizi kwa upande wa pili ndiyo
watuhumiwa hivyo tuna mashaka kuwa taarifa zitakazotolewa na viongozi hawa siyo
sahihi na za kweli kwa kuwa wao ndiyo watuhumiwa.
Kufuatia
hali hiyo sisi wananchi (wahanga) wa zoezi hilo tunakuthibitishia kuwa, Mkuu wa
Wilaya ya Tanganyika,Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Mkurugenzi viongozi (wateule
wako hawa)wameonyesha utovu mkubwa wa nidhamu na matumizi mabaya ya Ofisi.
Hivyo ombi letu kwako Mheshimiwa Rais ,uunde
timu ya Maalumu ya Wataalamu watakaofika katika maeneo yetu kufanya Uchunguzi
wa kina bila kuwashirikisha viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Katavi pamoja na Halmashauri ili kuepuka upotoshaji unaoweza
kufanyika ili kuharibu Uchunguzi.
1. Tume
hiyo ifike katika maeneo husika na kuzungumza na wananchi kwa uhuru badala ya
kuja na kufanya mazungumzo kwa kutumia hila na vitisho wakati wa kukusanya
taarifa kwa kuwa kufanya hivyo taarifa hizo hazitaweza kuleta mabadiliko chanya
kwetu kutokana na hasara kubwa pamoja na madhara yaliyosababishwa na uendeshaji
wa zoezi hili.
2. Serikali
kupitia Tume hiyo ipitie upya na kwa kina Taarifa na malalamiko na Vielelezo
vilivyowasilishwa ili kuweza kubaini namna kanuni na Maadili ya Viongozi
yalivyokiukwa ili Tume hiyo iweze kuchukua hatua stahiki kwa wahusika kwa kusababisha
hasara kubwa na usumbufu kwa raia kufuatia kuendeshwa kwa zoezi hili bila
kuzingatia kanuni taratibu na Sheria .
3.Serikali
ichunguze kuwepo kwa harufu za ukabila na Rushwa katika uendeshaji wa zoezi
hili kwani lengo la kupisha maeneo haya si uwezeshaji bali ni harakati za wazi
za uporaji wa haki kwa kuhakikisha wananchi ambao si kabila la wabende
tunaondolewa na kunyang’anywa mali zetu pasipo kuzingatia Sheria na Haki.
4. Tunavyo
vielelezo vya kuporwa kwa mali zetu,mauaji yaliyofanyika,risiti zinazotumika
kulazimisha kwa nguvu kulipa kiasi cha shilingi 100,000 kila raia pamoja na
usumbufu ikiwemo kutishiwa kunyang’anywa mashamba yetu ambayo tumeyamiliki
kihalali kwa muda mrefu na kwamba kama hatutalipia tunanyang’anywa mashamba
yetu ambayo tayari tumeshalima katika msimu huu wa 2017.
5. Tunaomba
kutoa ufafanuzi juu ya hofu iliyoibuka katika Ofisi ya Msajili wa vijiji hapo
awali baada ya kuhofia ujio wetu hapo TAMISEMI bila kuwa na Mwenyekiti wa
Kijiji kwamba ndiye alama inayotambulisha Serikali ya Kijiji na kuleta uhalali
wa madai yetu kuwa kwamba Mwenyekiti wa Kijiji,Diwani na Mbunge wetu Mheshimiwa
Kakoso ndiyo wahusika wakuu katika zoezi
hilo na ndiyo waratibu wakuu wa zoezi la kutuondoa katika maeneo yetu huku
sababu kubwa ikiwa ni ukabila kama ambavyo tumeeleza katika aya ya (3) kwamba
zoezi hili limetawaliwa na ukabila.
Kufuatia hali hii tunaomba Serikali itupatie msaada
wa hali na mali pamoja na wadau ili tuweze kupata huduma mbalimbali za
kibinadamu maana hadi sasa hatuna chakula,pamoja na mahitaji muhimu ya
kibinadamu ikiwemo huduma za Afya,miundombinu,Mahema magodoro na vitu vingine
vinavyohitajika kwa ajili ya kujikinga na mvua ambapo hadi sasa kuna kaya
zipatazo elfu moja (1000) hazina mahala pa kuishi
Ni mimi Said Seif Kikobe
Kwa niaba ya Wananchi wahanga wa zoezi la
kuondolewa kwa nguvu katika maeneo yetu Mkoani
Katavi.
No comments: