RIPOTI YA UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU MKOANI KAGERA.
Ripoti
hii ni jumla ya matukio mbalimbali pamoja na vitendo vya ukiukwaji wa
Haki za Binadamu ambavyo vimeshamiri katika maeneo ya Mkoa wa Kagera
pamoja na haya niliyoyashuhudia kwa macho na kuyasikia kwa masikio
yangu,napenda kutoa Ripoti hii ili Uongozi wa Kituo cha sheria na Haki
za Binadamu pamoja na waangalizi wa Haki za Binadamu kwa pamoja,tuweze
kuunda timu maalumu itakayoenda Mkoani ikiwa ni pamoja naWanasheria ili
kuyapatia ufumbuzi matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi wa
Tanzania waishio katika maeneo ya Mpakani mwa nchi yetu kama ifuatavyo:-
Kabla
ya kuyataja mambo ambayo yanapaswa kushughulikiwa naomba kuainisha
matatizo sugu niliyoyaona kuwa haya ndiyo chanzo cha ukiukwaji wa Haki
za Binadamu Mipakani mwa nchi yetu hususani Mikoa ya Kigoma na Kagera:
A: Watumishi wa Serikali kukaa muda mrefu katika vituo vyao vya kazi
B: Rushwa kubwa wanazoshiriki kwa asilimia 100 viongozi wa Serikali.
C: Ukabila
D: Mawasiliano Duni katika maeneo yanapofanyika matendo ya ukiukwaji
Wa Haki za Binadamu katika maeneo mbalimbali nchini.
E: Kutokuwa na Viongozi wazalendo wanaosimamia dhamana Watanzania
F: Katika mipaka ya nchi yetu ambapo kuna vitendo vingi vya uporaji
Vinavyofanywa na watumishi wa Serikali kwa manufaa yao kupitia
Mwamvuli wa Oporesheni ya kuwabaini wahamiaji Haramu.
G: Uwepo wa Mtandao wa watumishi wa umma unaoshirikiana na
Wahalifu kwa kuwapa nafasi ya kuishi katika nchi isivyo halali.
Kufuatia sababu nilizozitaja hapo juu naomba kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo :-
A: Watumishi wa Serikali kukaa muda mrefu katika vituo vyao vya kazi :
Kwa kawaida mtu akifanya kazi katika kituo chake kwa
zaidi ya miaka 30 ni lazima kutatokea madhara makubwa sana kwa vile
mtumishi huyo atakuwa hana tofauti na wanafamilia wa maeneo hayo na
hatokuwa tayari kuwajibika ipasavyo ili kulinda maslahi ya Taifa na
matokeo yake ataanza kufanya kazi kwa mazoea na kujinufaisha zaidi
kupitia shida zinazowasumbua wananchi kama ilivyo kwa watumishi wa idara mbalimbali za Serikali Mkoani Kagera.
Wanaotuhumiwa
kukaa muda mrefu ni watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamuro
ambapo hata baada ya kufanya mahojiano na Mkurugenzi wa Halmashauri
alikiri kuwepo kwa tuhuma mbalimbali alizowahi kuzisikia na baada ya
kuzifanyia kazi zilionekana kuwa ni za kweli ambapo tayari kulikuwa na
Afisa mmoja katika Idara ya Elimu ambaye tayari amehamishwa kitengo
baada ya kubainika kuwa alikuwa akiwajibu vibaya wananchi kwa ajili ya
kukaa na kufanya kazi kwa mazoea.
B: Rushwa kubwa wanazoshiriki kwa asilimia 100 viongozi wa Serikali:
Upande
wa Rushwa hiki ni kikwazo kikubwa cha kupatikana kwa Haki katika maeneo
mbalimbali nchini hususani Mkoani Kagera kwa kuwa nimeshuhudia kwa
macho yangu Idadi kubwa ya Raia wanchi za Burundi,Rwanda, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo wakimiliki uchumi mkubwa katika maeneo hayo na
wala hakuna kiongozi anayediriki kuwaeleza lolote kwa kuwa inaelezwa
kuwa viongozi mbalimbali wanahusika kuwapa hifadhi na kuwahakikishia
ulinzi kwa gharama yoyote na hali hii nimeishuhudia
Nyegezi Mkoani Mwanza baada ya kutukanwa kwa Serikali ya Tanzania kuwa
Serikali haipo na kama ipo imelala usingizi kwa kuwa watu hawa yaani
wahamiaji haramu hupelekwa lakini hurudi baada ya kuwahonga viongozi wa
serikali yetu ya Tanzania kiasi kikubwa cha fedha.
C: Ukabila:
Suala
la ukabila limepandikizwa kandokando ya mipaka hii mpaka inafikia
wananchi sasa kutambuana kwa Makabila yao ambapo kwa sasa kabila la
wasukuma na baadhi ya makabira yaliyoko Mkoani Kagera wameanza
kushambuliana kwa kutumia lugha za ukabila.
D: Mawasiliano Duni katika maeneo yanapofanyika matendo ya ukiukwaji:
Inaonyesha
kuwa kuhusu suala la mawasiliano ni moja ya matatizo makubwa ambayo ni
kikwazo kwa ajili ya usalama wanchi yetu kwa vile hakuna hata waandishi
wa habari wanaoweza kufuatilia taarifa mbalimbali na kuzitoa katika
vyombo vya habari ili jamii iweze kusikia matukio hayo isipokuwa kama
kuna mwandishi anayeweza kufanya hivyo si mwandishi wa kawaida bali ni
mmoja wa Wanaharakati kwani upo ugumu wa utumaji wa taarifa na ripoti
mbalimbali kufuatia mazingira ya maeneo hayo kuwa magumu.
E: Kutokuwa na Viongozi wazalendo wanaosimamia dhamana Watanzania:
Kuna
viongozi kweli ambao hawana uzalendo kabisa na zaidi wanafanya kazi kwa
mazoea na wao kuwa watu wakisubiri kuletewa taarifa badala ya kwenda
kujifunza na kuzibaini shida na matatizo yanayaikabili jamii matokeo
yake inashangaza sana kusikia kiongozi akisema hana taarifa na jambo
nyeti kama ukiukwaji wa Haki za raia na mali zao na kwa kweli iwapo
tunataka kuwa na taifa lenye viongozi walio tayari kushughulika na kero
za wananchi hatuna budi kuishauri serikali kuwaondoa
viongozi wote walioko mipakani kwa kuwa wako huko kwa ajili ya kufanya
kazi kwa maslahi yao na si kwa ajili ya kuwatumikia watanzania kama
yalivyokuwa malengo ya aliyewateua
F: Katika mipaka ya nchi yetu ambapo kuna vitendo vingi vya uporaji
Vinavyofanywa na watumishi wa Serikali kwa manufaa yao kupitia
Mwamvuli wa Oporesheni ya kuwabaini wahamiaji Haramu.
Katika
hili sasa kuna tuhuma zinawalenga viongozi mbalimbali wa Serikali
wakiwamo Viongozi wa Matawi,Vitongoji,Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa,
Viongozi wa Jeshi la Polisi,Wanyama Pori,Mgambo, Mahakama na baadhi ya
Wanajeshi wa JWTZ ambao wameshafanya uporaji wa mali za wananchi na
ikiwemo kutoza faini ya Mamilioni ya shilingi,kuchangisha fedha kiasi
cha mpaka kufikia 200,000/= 600,000/= hadi kufikia 6,000,000/=ambapo
walioweza kusalimika katika zoezi hili na kuachwa salama ni makundi ya
wahamiaji haramu kutoka nchi jirani kama nilivyozitaja katika kipengele
kilichopo hapo juu ambapo baadhi ya Wananchi ambao ni raia wa Tanzania
waliposhindwa kutimiza matakwa ya viongozi hawa kilichotokea ni
kuchomewa nyumba zao na kuachwa wakiwa hawana chakula na wala hakuna
mahitaji mbalimbali muhimu kwa jamii jambo
ambalo hadi sasa kina mama wanajifungulia nje hususani vichakani na
hawana msaada wowote.
Wapo
wafugaji walioporwa mifugo yao na sasa wamefunguliwa kesi mbalimbali
kuhakikisha wana
shindwa kupeleka madai yao mbele ya sheria ili waweze
kurejeshewa mali zao ,wapo pia wananchi waliopoteza familia zao akiwemo
Mzee Numbu Yihorogo ambaye mpaka sasa Mke na watoto wake hawajulikani
walipo na baadhi ya mifugo yake imeporwa na maafisa wa Wanyama pori na
matokeo yake hadi sasa anaishi kwa wasamalia wema zipo ng’ombe zenye
thamani ya mamilioni ya shilingi zimefyatuliwa risasi na kuuawa na sasa
wafugaji hawa hawana pa kuanzia kudai fidia ya mali zao na sasa wanaomba
msaada wa Wanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ili waweze
kusaidiwa kufungua kesi ya madai dhidi ya serikali kwa kuwaachia
watumishi wake kuwafanyia unyama mkubwa na kuwaita
WAHAMIAJI HARAMU NDANI YA
NCHI YAO KINYUME NA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.
G: Uwepo wa Mtandao wa watumishi wa umma unaoshirikiana na
Wahalifu kwa kuwapa nafasi ya kuishi katika nchi isivyo halali.
Katika hili pia kuna uhakika wa madai haya kwa kuwa mimi nikiwa ndani ya Basi la Kampuni ya Bunda Bus nikitoka Bukoba Jeshi la Polisi Mkoani
Geita walikamata madawa ya kulevya aina ya mirungi na kuniomba kuwa
shahidi wa tukio hilo ambapo zipo taarifa zinazodai kuwa mmoja wa
watuhumiwa wa kusafirisha dawa hizo ni mke wa askari mwenye cheo kikubwa
ndani ya jeshi hilo Mkoani Geita na sasa imepelekea kuachiwa huru kwa
mtuhumiwa huyo.
MAPENDEKEZO:
Baadhi ya mambo ambayo mimi binafsi naomba yafanyiwe marekebisho ya haraka nia kama ifuatavyo:
· Watumishi mbalimbali wa
Serikali walioko mpakani wakiwemo Askari polisi,Wanyama Pori,Mgambo,
JWTZ ,Wakuu wa Wilaya,Mikoa, na baadhi ya Wananchi wanaotuhumiwa
kushirikiana na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani nilizozitaja hapo
juu na viongozi wa Mamlaka ya Mapato,Uhamiaji, wachukuliwe hatua kali za
kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi kwa kuwa wameinajisi Serikali kwa
kuwanyanyasa wananchi ambao ni Raia halali na matokeo wameingiza makundi
makubwa ya wahamiaji haramu huku wakiwahalalisha baada ya kupewa rushwa
jambo ambalo ni kinyume na taratibu za nchi yetu.
· Kwa
kuwa uwepo wa viongozi wasio waadilifu katika mipaka ya nchi yetu upo
uwezekano wa kuwa na raia wa kigeni wengi ambao watakuja kupatiwa
vitambulisho vya taifa na kuondoa maana ya zoezi zima la kuratibu orodha
ya watanzania ambao pia ni raia halali wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania hivyo kutumia gharama nyingi katika zoezi ambalo hakutakuwa na
tija.
· WANAHARAKATI
WOTE TUUNGANE NA KUELEKEZA MACHO YETU MIPAKA YOTE ILI KUHAKIKISHA
TUNAWAMULIKA VIONGOZI WASIOWAJIBIKA KATIKA NAFASI ZAO NA PIA TIMU KUTOKA
LHRC NA THRD ZIKAPIGE KAMBI KWA MUDA MKOANI KAGERA KUWEKA AMANI KWA WANANCHI WANAOTISHIWA USALAMA WAO KILA WAKATI NA LITOLEWE TAMKO RASMI KUHUSU MATATIZO YALIYOPO MAENEO HAYO ILI KURUDISHA IMANI KWA WANANCHI WANAOHAMISHWA KWA KUONEWA MAANA HADI SASA WAKO NJIA PANDA NA HAWAJUI HATMA YAO:
RIPOTI HII IMEANDALIWA NA :
ANTONY JOHNSON SOLLO
S.L.P 1288 – KISHAPU
SHINYANGA
Mob: +255 787 565533 Email antonyjilala@yahoo.com
No comments: