Askari wa Kikosi Maalumu cha Anga (SAS) cha Uingereza, ameonekana shujaa katika tukio la uvamizi lililotokea katika jengo la maduka la Westgate jijini Nairobi Kenya baada ya kufanikiwa kuokoa watu 100 waliokuwa ndani ya jengo hilo.
Mmoja wa majeruhi akiokolewa
Askari huyo ambaye jina lake halikutajwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni sababu za kiusalama, wakati wavamizi hao wanavamia jengo hilo siku ya Jumamosi, naye alikuwemo ndani ya jengo hilo akinywa kahawa.
Kwenye baadhi ya mitandao, askari huyo ameonekana 
akiwasaidia wanawake wawili huku akiwa ameweka bastola kwenye suruali 
yake, ingawa sura yake imefichwa.
Habari zinasema kuwa, askari huyo ameonekana 
shujaa kwani licha ya hali tete iliyokuwa ndani ya jengo hilo, aliweza 
kuingia na kutoka zaidi ya mara 12 akiwaokoa baadhi ya watu waliokwama 
ndani ya jengo hilo lenye maduka na migahawa mbalimbali.
“Alichofanya ni kitendo cha kishujaa sana, alikuwa akinywa kahawa na baadhi ya rafiki zake wakati wavamizi walivyoingia.
Alirudi ndani mara 12 na kufanikiwa kuokoa zaidi 
ya watu 100. Fikiria kuthubutu kurudi ndani huku akijua kabisa jinsi 
hali ilivyo ndani ya hilo jengo,” baadhi ya mashuhuda walinukuliwa.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, askari huyo wa 
Uingereza  anafanya zaidi shughuli zake Kenya na nje ya nchi hiyo ikiwa 
ni pamoja na kuwafuatilia raia wa nchi yake wanaojishughulisha na mambo 
mbalimbali.
Agosti mwaka huu, gazeti la Daily Mirror 
liliripoti kuwa kikosi maalumu cha SAS na askari maalumu wa kupambana na
 ugaidi,  wameanza kumtafuta Samantha Lewthwaite, Mwanamke anayetajwa 
kuwa ni raia wa Uingereza anayedaiwa kuwa gaidi ambaye pia anashirikiana
 na kundi la  Al-Shabaab.
Mwanamke huyu mjane anayetajwa kuwa ni gaidi, inasemekana pia alishiriki kupanga na kutekeleza uvamizi mjini Nairobi.
Kikosi hicho cha SAS, kinaelezwa kuwa kinafanya 
kazi kwa ukaribu na vikosi vya ulinzi vya Uingereza, Kenya na vile vya 
nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Habari juu ya askari huyo zimekuja wakati milio ya
 risasi ikizidi kusikika ndani ya jengo hilo, huku maofisa wa usalama wa
 nchi hiyo wakisema kuwa wamedhibiti sehemu kubwa ya jengo hilo. Habari 
zaidi zinasema kuwa, bado zaidi ya watu 10 wanashikiliwa ndani ya jengo 
hilo kama mateka.
                
              ‘Tumeshadhibiti sehemu yote ya jengo, tuko hapa 
kuhakikisha tunawaadhibu vya kutosha hawa watekaji,” Mkuu wa Jeshi la 
Polisi wa Kenya, IGP David Kimaiyo aliandika kwenye mtandao wake wa 
Twitter 
Licha ya maelezo hayo, mpaka jana saa 12 asubuhi bado milio ya risasi ilikuwa ikizidi kusikika ndani ya jengo hilo.
Kundi la Al-Shabaab, lililodai kuhusika na tukio 
hilo, juzi liliweka ujumbe wa sauti kwenye baadhi ya mitandao likidai 
kuendelea kushikilia sehemu kubwa ya jengo hilo. “Licha ya juhudi 
zinazofanywa, bado tunaendelea kushika sehemu ya jengo la Westgate,” 
Msemaji wa Al-Shabaab Sheik Ali Mohamud anasema.
Mtandao wa Daily Mail unasema kuwa, Waziri wa 
Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed anasema raia watatu wa Marekani na 
mmoja wa Uingereza, ni kati ya watu waliovamia jengo hilo la Westgate.
“Mvamizi kutoka Uingereza ni mwanamke ambaye 
amekuwa akijaribu kutekeleza uvamizi kama huu mara nyingi,” anasema 
Mohamed akimlenga Samantha Lewthwaite, anayedaiwa kuwa gaidi wa 
kimataifa.
Marekani imesema kuwa, inaendelea kufanya 
uchunguzi ili kubaini kama kuna raia wake yeyote aliyehusika kwenye 
tukio hilo ambalo mpaka sasa limegharimu maisha ya watu zaidi ya 60.
Makala haya yameandikwa na Fredy Azzah kwa msaada wa vyombo vya habari.
No comments: