Mmoja wa majeruhi katika shambulizi la risasi lililotokea Ilala Bungoni, Dar es Salaam juzi, Rubani Francis Shumila amefariki dunia jana katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), alikokuwa akitibiwa.
Wakati hilo likitokea, mama mzazi wa Christine Alfred, binti anayedaiwa kuwa chanzo cha shambulizi hilo, Hellen Alfred amekana kutambua uchumba baina ya marehemu Gabriel Munisi na mtoto wake huku kaka wa marehemu huyo akieleza kwamba alitambulishwa na mdogo wake, kwa binti huyo kwamba ni mchumba wake.
Katika shambulizi hilo, Munisi anadaiwa
kuwashambulia marehemu Shumila, Hellen, Christine na mdogo wake Alpha
ambaye alifariki dunia papo hapo katika shambulizi hili linaloelezwa
kuwa lilitokana na wivu wa mapenzi. Baada ya shambulizi hilo, Munisi
naye alijiua kwa kujipiga risasi kichwani.
Ofisa Uhusiano wa taasisi hiyo, Patrick Mvungi
alisema jana kwamba Shumila alifariki dunia saa 12.40 asubuhi akiwa
katika Chumba cha Wagonjwa wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Hellen amelazwa katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) na hali yake inaendelea vizuri na Christine aliruhusiwa
kutoka hospitali juzi hiyo hiyo.
Taarifa ya daktari
Mvungi alisema kuwa taarifa za awali za daktari
zinaonyesha kwamba Shumila alipoteza damu nyingi kutokana na majeraha ya
kupigwa risasi tatu.
Alisema alipigwa risasi kichwani, mkononi na tumboni.
Ndugu zake Shumila ambao walibainika wanatoka Kenya waligoma kuzungumza lolote kuhusu tukio hilo.
Ofisa wa Ubalozi wa Kenya nchini alisema jana
kwamba wamesikia taarifa hizo kwenye vyombo vya habari lakini akasema ni
mapema kulizungumzia.
Utata wa uhusiano
Ofisa Uhusiano wa MNH, Jacqueline Msuya alisema
kuwa amezungumza na mama yake Christine ambaye alimweleza kwamba
anatambua kwamba Shumila na mwanaye anayesoma huko Cyprus walikuwa
wachumba na kusema kwamba binti yake huyo aliwahi kumwambia kwamba
Munisi alikuwa rafiki yake wa kawaida tu
Hata hivyo, maelezo hayo yanatofautiana na yale ya Kaka wa
Munisi, Edward Mgaya ambaye alisema jana kwamba marehemu Munisi
alimtambulisha kwa Christine Juni mwaka huu kuwa ni mchumba wake na
kwamba kabla ya hapo hakuwahi kufanya hivyo kwa msichana mwingine
yeyote.
“Naamini Christina ndiye alikuwa chaguo lake,
lakini sielewi ni jambo gani limejitokeza kati yao. Mdogo wangu hakuwahi
kunilalamikia juu ya uhusiano wao,” alisema Mgaya huku akitiririkwa na
machozi na kuongeza:
“Gabriel alikuwa na miaka 31 na wa tatu katika
familia yetu. Alijishughulisha na kuuza magari ambayo aliyachukua hapa
Dar es Salaam na kuyasafirisha hadi Mwanza.”
Mgaya alisema mazishi ya Munisi yamepangwa kufanyika kesho katika Kijiji cha Masama mkoani Kilimanjaro.
Hali ya Christine
Christine, ambaye alijeruhiwa miguuni, aliruhusiwa kurudi nyumbani juzi baada ya kufikishwa Hospitali ya Ilala Amana.
Mmoja wa wanafamilia ambaye alikataa kutaja jina
lake, alisema ndugu yao kwa sasa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya
Regency lakini hajalazwa.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa familia ya Christine
na ile ya Shumila walikuwa wamepanga kukutana jana kwa pamoja na kuandaa
mipango ya mazishi ya Alpha na Shumila.
Polisi yashtuka
Jeshi la Polisi limesema litaanzisha operesheni
kuwabaini baadhi ya watu waliomilikishwa silaha kihalali huku wakitumia
silaha hizo kinyume na malengo.
Taarifa ya iliyotolewa jana na Msemaji wa Polisi,
Advera Senso ilisema watakaobainika kutumia silaha kinyume cha taratibu
zilizowekwa, watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya.
“Katika siku za hivi karibuni, imebainika kuwa,
baadhi ya watu wamekuwa wakitoa vitisho kwa wananchi kwa kutumia silaha
hizo bila sababu za msingi wanapokuwa katika maeneo mbalimbali, kama
vile kwenye baa, kumbi za starehe na hata kulipizana visasi, jambo
ambalo ni kinyume cha sheria na malengo ya umilikishwaji.”
No comments: