ALIYEKUWA WAZIRI MKUU NCHINI TANZANIA NA MGOMBEA WA URAIS KATIKA CHAMA CHA UPINZANI CHADEMA KATIKA UCHAGUZI ULIOPITA EDWARD LOWASSA AMEWATAKA WAKENYA KUVUMILIANA WAKATI HUU AMBAPO TAIFA HILO LINAKARIBIA UCHAGUZI
Aliyekuwa waziri
mkuu nchini Tanzania na mgombea wa urais katika chama cha upinzani
Chadema katika uchaguzi uliopita Edward Lowassa amewataka Wakenya
kuvumiliana wakati huu ambapo taifa hilo linakaribia uchaguzi.
Akizungumza
nchini Kenya katika mazishi ya aliyekuwa waziri wa usalama nchini humo
marehemu Joseph Nkaiserry, Lowassa amesema kuwa kenya inapaswa kujifunza
kutoka kwa machafuko ya uchaguzi ya mwaka 2007.
Matamshi yake yaliungwa mkono na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
aliyewataka wafuasi wake na wale wa kiongizi wa upinzani Raila Odinga
kuvumiliana.
Uhuru alisema kuwa hakuna haja ya kupakana tope za matusi akiongezea kuwa matusi hayasaidii.
''Sisi
sote ni Wakenya , hatuna taifa jingine la kujenga baada ya uchaguzi
,tunaomba amani, amani amani'', alisema rais Uhuru Kenyatta.
Matamshi
ya Uhuru na Lowassa yanajiri wakati ambapo wafuasi wa upinzani na wale
wanaounga mkono serikali wamekuwa wakiwazomea viongozi wanaotoka pande
pinzani katika mikutano ya kampeni na hata kusababisha mikutano hiyo
kusitishwa.
Lowassa amesema kuwa Kenya ni tegemio la kiuchumi
katika mataifa ya Afrika mashariki hivyobasi inafaa kuwa mfano kwa
kuhakikisha kuwa taifa hili halijiingizi tena katika jinamizi la
machafuko yalioonekana miaka 10 iliopita.
''Ombeni musirudi katika
mapigano yaliotokea mwaka 2007, Kenya iko mbele kushinda taifa lolote
lile Afrika mashariki na tunataka muendelee kusonga mbele.
Lowasa alisema kuwa marehemu Nkaissery aliamini sana
Umoja wa Afrika mashariki na alijitolea kufanya kazi na akawataka
viongozi wengine kuiga mfano wake.
Naye rais Uhuru aliongezea
kwamba Kenya na Tanzania ni pacha na zitaendelea kuimarisha ushirikiano
wao kwa lengo la kurahisisha biashara na usalama kati ya raia wa mataifa
hayo mawili.
Miongoni mwa wale waliohudhuria mkutano huo ni
pamoja na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga na naibu wa
rais William Ruto
No comments: