HONGERA WAZIRI MKUU KUFANYA ZIARA MWANZA
Antony Sollo Misungwi
Ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Kassim Majaliwa Jijini Mwanza imekuwa ya mafanikio,hii ni baada ya
kubaini mambo uozo lakini haya ni kwa uchache kutokana na siri kubwa iliyofichika
kutokana uozo mwingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya
Misungwi Mkoani Mwanza.
Historia ya kuwepo kwa Uozo Misungwi.
Wilaya ya Misungwi ni moja kati ya Wilaya
kongwe nchini ambazo zimekuwa zikiongoza kwa kupata hati chafu na imekuwa
bahati kwa Mawaziri Wakuu wa awamu ya Nne na ya tano ambao wote wamebahatika
kukumbana na uozo jambo lililopelekea kuwatumbua watumishi wachache wa
Halmashauri hiyo huku vinara wakiachwa kutokana na kuwepo kwa mnyororo mkubwa
ambao umetengenezwa maalumu kwa ajili ya upigaji dili.
Katika ziara yake hivi karibuni,Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Khassim Majaliwa amemsimamisha
kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Alphonce
Sebukoto, na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.
Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada
Mwanasheria huyo kuonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni
pamoja na kushindwa kuishauri vyema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya
sh. milioni 279.
Majaliwa alimsimamisha kazi Sebukoto 19februari
mwaka huu wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa
katika ziara ya siku tano ya kikazi mkoani Mwanza ambapo waziri Mkuu alisema.
“Mwanasheria utasimama kazi kuanzia
leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo husika na uchunguzi
ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. hatutakuonea lakini hatuwezi
kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya,” alisema Majaliwa.
Imeelezwa kuwa Novemba 2017 wakati
alipokuwa anakaimu nafasi ya Ukurugenzi Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo ya
sh. milioni 279 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo, Antony Bahebe.
Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Mkuu Bahebe
aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya
ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya
Seekevim ambapo alisema mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa
ukamilike 2015,ambapo Mwanasheria huyo
aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa
imekwisha tangu Desemba 2015.
“Mwanasheria amemlipa Mwenyekiti wa
Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha Halmashauri
yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na
aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho Mkurugenzi hayupo, ”alisema Majaliwa huku akiwakumbusha watumishi wa umma
kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa
majukumu yao.
Akifafanua Majaliwa alisema fedha
alizolipwa Bahebe zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya
maendeleo katika halmashauri hiyo.
Katika
ziara hiyo Waziri Mkuu alifungua mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu
katika shule ya msingi ya Mitindo iliyoko wilayani Misungwi na pamoja na kukagua
ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Ukiacha na kipande hicho cha uozo
uliofichwa,Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imekuwa na historia mbaya kwa
watendaji wa Wilaya hiyo kutafuna fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo
ambapo baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo wamekuwa wakibuni mbinu
mbalimbali kuwahadaa wananchi.
Mwaka 2016 Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sanjo Charles Bulugu,alimchongea
kwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Eliud Mwaiteleke kwa
kutoa taarifa za uongo katika mkutano wa Serikali ya Kijiji cha Sanjo
akisema kuwa,Mkurugenzi huyo alishindwa kufika katika mkutano wa kijijinihicho
kwa kukosa gari la kumpeleka kusikiliza kero za wananchi hao.
Katika mkutano huo Bulugu
alidai kuwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi alitoa agizo akimtaka Mkurugenzi kufika
katika kijiji hicho kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha
Sanjo kwa kuuomba Uongozi wa Wilaya ya Misungwi ufike hapo kusikiliza kero zao.
Katika taarifa hiyo iliyotengenezwa ili kuwahadaa wananchi wa
Kijiji cha Sanjo Bulugu alimsingizia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi Eliud
Mwaiteleke kuwa eti
amekwama kufika
katika mkutano huo kutokana na kukosa usafiri kufuatia gari lake kuwepo
katika usimamizi wa mitihani ya Taifa kwa wanafunzi wa Darasa la Saba.
“Ndugu zangu
wananchi kwa niaba ya Mkurugenzi napenda kuwaomba radhi kwa kuchelewa
kufika hapa mgeni wetu sasa ni saa tano asubuhi ,ni kwamba mgeni wetu
hataweza kufika kutokana na kukosa usafiri wa kumleta hapa,gari lake liko
kwenye shughuli za Mitihani ya Darasa la saba”alisema Bulugu huku miguno na
maswali toka kwa wananchi vikitawala.
“Hivi Mtendaji huoni
kuwa huu ni uzembe wa makusudi,magari yote ya Halmashauri hayapo kweli? hata
gari lake liko kwenye mitihani?mbona hawa watu wanataka kuturudisha
tulikotoka? Sasa tunakuagiza Mtendaji ukamwambie Mkuu wa Wilaya kuwa agizo
lake limepuuzwa! kwa nini Mkurugenzi asitumie hata Hiece?” alihoji mmoja wa
wananchi waliokuwepo katika mkuitano huo.
Yaliyojiri baada ya Uchunguzi
Uchunguzi uliofanywa
kipindi hicho Tanzania Daima lilibaini kuwa, taarifa hizo hazikuwa za kweli
kwani Mkurugenzi huyo alikuwa safari ya kikazi Mjini Dodoma.
taarifa hiyo iliwakera
wananchi na kuahidi kugomea mikutano ijayo iwapo hawatapata maelezo ya
kutosha juu ya tukio hilo ambapo hadi leo hii wananchi hao hawajawahi
kusikilizwa kutokana na kwamba mkutano huo ulikuwa kama kiini macho kuficha tuhuma
zilizokuwepo kwa watumishi kipindi hicho.
Mwandishi wa
Tanzania Daima alimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ili kutolea ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa
na Afisa Mtendaji huyo ambapo Mkurugenzi alisema kuwa hazina ukweli.
“Mimi kwa sasa niko
Mbeya,nimeshtushwa sana na taarifa hizo mimi nikose usafiri si ningeenda na
pikipiki? Sisi kazi yetu ni moja tu nayo ni kuwatumikia wananchi na si
vinginevyo sijui Mtendaji huyo kapata wapi maelekezo hayo ngoja
nifuatilie”alisema Mwaiteleke.
Wakizungumza na
Tanzania Daima kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kuwa wamekwazwa na
kitendo cha Mkurugenzi kushindwa kufika kijijini jambo walilosema bila
kumung’unya maneno kwamba ni uzembe.
Akiweka wazi siri
zilizokuwa zimefichika katika maandalizi ya taarifa za uongo zilizotolewa na
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sanjo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyasubi
Meni Lutandula aliliambia Tanzania Daima kuwa kuna udanganyifu mkubwa
katika ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Sanjo ambapo walibaini
matumizi mabaya ya fedha za wananchi kiasi cha shilingi milioni 20,828,502;60 katika
ujenzi wa mradi wa maji.
“Inasikitisha kuna
ujenzi wa shule ambayo hata hivyo ilikuwa haijaanza kufanya kazi lakini
tayari vyumba vimechakaa kutokana na kujengwa chini ya kiwango wananchi kulazimishwa
kuchangia shilingi 6500 kila familia kwa ajiri ya ukarabati wa vyumba
hivyo”.alisema Lutandula.
Mwenyekiti wa Kijiji
cha Sanjo Bukali John alipotakiwa kutolea ufafanuzi sakata la ujenzi wa
madarasa chini ya kiwango alisema alikiri na kumuonya mwandishi asiripoti
taarifa hizo.
“Nisingependa uendelee
kufuatilia jambo hilo kwa kuwa wananchi tayari tumeshawashawishi
wananchi na wamekubali kuchangia fedha kwa ajiri ya kurekebisha vyumba hivyo ni
kweli kuna mapungufu yaliyojitokeza katika ujenzi wa vyumba hivyo lakini
sitaki ufuatilie suala hilo maana tayari tumeshafanya vikao na wananchi na tumekubaliana
wachangie fedha kiasi cha shilingi 6500 kila familia ili tuweze kukarabati
vyumba hivyo” alisema Bukali.
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda alipotafutwa kuzungumzia kama alitoa agizo
kwa Mkurugenzi ambapo alisema kuwa hana taarifa zozote juu ya agizo hilo na
kwamba yeye hajawahi kufanya ziara katika kijiji cha Sanjo.
“Mimi sijawahi
kufanya ziara yoyote katika kijiji hicho isipokuwa nilishiriki kikao cha Kamati
ya Maendeleo ya Kata ya Fela hivyo sijui Afisa Mtendaji huyo alitoa wapi
maelekezo hayo nitafuatilia kujua zaidi juu ya jambo hilo”alisema Sweda.
Baraza la Madiwani kuwapa Siku 30 kwa
watendaji
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya
ya Misungwi, limewapa muda wa siku 30 watendaji kushughulikia suala la
makusanyo ya mapato ya ndani na utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji
cha Fela uliokwama tangu 2013.
Azimio hilo lilipitishwa na baraza hilo wakati wa kikao kilichofanyika mjini Misungwi juzi, baada ya kubainika kuwa hadi Desemba 2017 halmashauri hiyo imekusanya Sh734.9 milioni pekee kati ya malengo ya kukusanya Sh2.06 bilioni.
Katika Baraza hilo Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga aliwacharukia watendaji na kuwataka watoe maelezo juu ya kusuasua kwa ukusanyaji mapato, hali inayokwamisha utekelezaji wa miradi.
Akitolea mfano wa kusuasua alisema kuwa katika mwalo huko Mbarika vitabu vya halmashauri vinaonyesha hakuna mapato yanayokusanywa, lakini hivi karibuni kamati ya uchumi na mipango ilipotembelea eneo hilo ilifanikiwa kukusanya Sh15,000 kwa muda mfupi, hali inayodhihirisha udhaifu katika ukusanyaji wa mapato.
Kuhusu mradi wa maji wa Fella ambao utekelezaji wake ulianza Juni 2013 na kutakiwa kukamilika Desemba mwaka huo, baraza limempa siku 30 mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke kuhakikisha unakamilika na kutoa maji au uwekwe chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Mradi huo ambao tayari umegharimu zaidi ya Sh644 milioni, unatarajiwa kunufaisha wakazi 6,473 wa vijiji vya Fella, Ngeleka na Bujingwa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, mhandisi wa maji wa halmashauri hiyo, Ali Mruma alisema tayari maji yameanza kutoka na zinahitajika zaidi ya Sh3.8 milioni kununulia mashine ya kuyasukuma ili kuongeza usambazaji wa huduma kwa wananchi.
Diwani wa viti maalum, Christina Nyanda alisema maji hayo kata ya Mamaye yanatoka kwa kusuasua na kutaka wataalamu kutoa maelezo sahihi.
Mkandarasi wa kampuni ya COWI Tanzania Ltd inayotekeleza mradi huo, Ernest Tinka alikiri kuwapo upungufu na kuahidi kurekebishwa.
Siri
zilizofichika nyuma ya miradi Misungwi.
1.
Kuna maslahi binafsi katika utekelezaji
wa Miradi mbalimbali Wilayani Misungwi kutokana na baadhi ya viongozi wa
Serikali na kisiasa kudaiwa kuwa ndiyo wamiliki wa makampuni yanayotekeleza
miradi hiyo ambapo kwa haya aliyokutana nayo Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Suluhisho
kuinusuru Miradi ya maendeleo dhidi ya Mchwa.
inatakiwa
kuunda Tume Maalumu kwa ajiri ya kuchunguza ufujaji wa mali za Umma lakini
pia watumishi wa Wilaya ya Misungwi wahamishwe kutokana na Mtandao wao unaokwamisha
kujulikana kwa uozo kupitia kwa Kaimu Afisa Habari wa Wilaya ya Misungwi
Thomas Lutego ambaye hata akiwa na shughuli hubagua Waandishi wa Habari kwa
lengo la kuficha maovu hayo.
No comments: